Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Viongozi wa Taasisi na Mashirika wanawajibika kuchangia juhudi za Serikali katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuandaa na kutekeleza mikakati itakayosaidia kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi na Biashara ya Kaboni unaofanyika katika Ukumbi wa APC – Mbweni Jijini Dar es Salaam. Amesema Mikakati itakayoandaliwa ni vema ijielekeze katika kuhimiza matumizi bora ya rasilimali, uwekezaji katika nishati mbadala na teknolojia rahisi na nafuu, na kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.

Kuhusu Biashara ya Kaboni, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuwepo kwa uratibu madhubuti katika utekelezaji wa biashara ya kaboni kwa kuwa biashara hiyo inahusisha wadau wengi. Ameongeza kwamba ni vema Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Serikali za Mikoa kukutana kwa ajili ya kujadili na kupata mwelekeo wa pamoja katika uendeshaji wa biashara hiyo.
Pia Makamu wa Rais amesema ni muhimu kupata uzoefu kuhusu uendeshaji wa biashara ya kaboni kutoka nchi nyingine ili kuona namna zinavyokabiliana na changamoto zinazojitokeza.
Makamu wa Rais amesema uwazi katika mikataba ya biashara ya kaboni utasaidia uendeshaji wa biashara hiyo na kuondoa hali ya kutoaminiana. Amesema kwa sehemu kubwa, uendeshaji wa biashara hiyo umetawaliwa na Madalali ambao pia utaratibu wa upatikanaji wao hauko wazi. Ameongeza kwamba kutokana na hali hiyo, imekuwa vigumu kufahamu kilicho ndani ya mikataba kati yao na wanunuzi na kama kiasi kinacholipwa ndicho kilichotolewa na wanunuzi.
Makamu wa Rais amesema taratibu za jinsi biashara ya kaboni inavyofanyika zinapaswa kuwekwa wazi kwa wadau wakuu, yaani Wanavijiji na Halmashauri, ambao ndiyo wamiliki wa misitu. Amesisitiza Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais na TAMISEMI kuongeza kasi ya kufanya programu maalum ya kufikisha elimu katika ngazi ya wilaya na vijiji. Pia ameviagiza Vyombo vya Habari na Taasisi za Teknolojia kuongeza jitihada katika kutoa elimu ya biashara ya kaboni.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza taasisi na mashirika kutekeleza mipango ya kutumia vifaa vyenye matumizi kidogo ya umeme na kuhamia kwenye magari yanayotumia umeme na gesi. Amewasishi Wakuu wa Mikoa kuahamasisha vyombo vya ulinzi na usalama katika mikoa kuanza kutumia magari yanayotumia nishati ya umeme na gesi. Amesema ni muhimu taasisi na mashirika yawe na vitengo vya mazingira na kutenga bajeti za utekelezaji wa miradi na shughuli za kuhifadhi mazingira.
Makamu wa Rais amesema Serikali ya awamu ya Sita imedhamiria kukuza mchango wa biashara ya kaboni katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo kiuchumi. Amesema kupitia Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (National Carbon Monitoring Centre) hadi mwishoni mwa mwezi Februari 2025, kimesajili miradi 72. Amesema pia miradi mikubwa katika sekta ya usafirishaji kama mradi wa Treni ya Mwendokasi (SGR) na Mabasi ya Mwendo kasi kwa Jiji la Dar es Salaam, miradi ya Mionzi ya Jua, nishati safi ya kupikia na hata wa bwawa la umeme la Mwalimu Julius Nyerere ambayo inachangia katika utekelezaji wa michango ya taifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, inaweza kusajiliwa katika fursa ya biashara ya kaboni kwa kufuata taratibu na miongozo husika. Aidha amesema ipo fursa ya kutumia taka ngumu katika biashara ya kaboni ili kunusuru hali ya uchafuzi wa mazingira na kukuza uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Masauni amesema uwepo wa Kituo cha Kusimamia na Kuratibu Kaboni kisheria (NCMC) utaleta manufaa mbalimbali ikiwemo kutoa fursa kwa nchi kushiriki katika masoko ya kaboni kimataifa na kuchochea uwekezaji katika sekta zingine.

Amesema manufaa mengine ni kuongeza pato la Taifa, kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira pamoja na kuimarisha ushirikiano na Taasisi, Mashirika na Sekta Binafsi katika kuibua fursa za uwekezaji za biashara ya kaboni nchini. Ameongeza kwamba, kwa sasa kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kuingia mikataba mbalimbali itakayoleta faida kwa Taifa bila kipingamizi cha kisheria.
Waziri Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman amesema Mkutano huo ni muafaka katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuwa Zanzibar kama ilivyo kwa maeneo mengine, inaendelea kuathirika na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaikumba Dunia. Amesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri mashamba ya kilimo kuingia maji ya chumvi, kuharibika kwa ubora wa maji ardhini unaotokana na visima vya maji kuingia maji ya chumvi, kupanda kwa kina cha maji ya bahari kunakopelekea kuongezeka kwa mmonyoko wa fukwe na kupotea kwa makaazi ya baionuai.
Aidha Mhe. Harusi ameongeza kwamba Zanzibar tayari imepitisha kanuni ya biashara ya kaboni hivyo Mkutano huo unatoa fursa ya kujifunza na kupata uzoefu kuhusiana na biashara hiyo.

