Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewakaribisha wawekezaji kutoka Umoja wa Ulaya kuwekeza nchini katika sekta za Kilimo, Usafirishaji, Nishati,Tehama,Utalii na katika Viwanda vya kuongeza thamani kwa kuwa serikali inahitaji kufungua zaidi sekta hizo ili kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 23 Februari 2023 wakati akifungua Jukwaa la Kwanza la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya linalofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Amesema Tanzania imedhamiria kuvutia uwekezaji katika kutumia rasilimali zilizopo kwa kuzingatia eneo la kimkakati iliopo ambalo ni fursa katika kuhakikisha usalama wa chakula pamoja na ukuzaji wa kilimo kwa ujumla.

”Kwa sasa Tanzania ipo katika maandalizi ya Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka mingine 25 ambayo inalenga kubadilisha uchumi wa Taifa kutoka katika hali ya uchumi wa kati wa chini hadi kufikia uchumi wa kati wa juu ambapo kwa kiasi kikubwa unahitaji biashara na uwekezaji.”

Pia Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji mazingira mazuri na salama ya uwekezaji na biashara hapa nchini kwa kuzingatia juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ikiwemo kuweka sera imara na zinazotabirika pamoja na sheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, kuendeleza miradi mikubwa ikiwemo ya nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.

Makamu wa Rais amesema Jukwaa hilo linapaswa kuwa chachu ya kuongeza uwekezaji wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania na kuwa sehemu ya kujenga imani na uaminifu kwa pande zote mbili. Amesema ushirikiano huo unaambatana na matarajio ya Tanzania ya kuwa sio tu kitovu cha biashara cha kikanda bali pia ghala la chakula ulimwenguni. Ameongeza kwamba uwekezaji utanufaika na soko kubwa la ndani la watu milioni 61.7, soko la kikanda la JUmuiya ya Afrika Mashariki la watu wasiopungua milioni 177, Soko la Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC) la zaidi ya watu milioni 300 pamoja na Eneo la Biashara Huria la Bara la Afrika (AfCFTA) linalojumuisha nchi 55 za Afrika zenye soko lisilopungua watu bilioni 1.4.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa Jukwaa hilo kuwa mwanzo wa mengine mengi yajayo na kuwa na mijadala ya wazi juu ya fursa, hofu na vikwazo vinavyozuia maendeleo ya haraka katika kuchochea uwekezaji na biashara baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya. Pia amewahimiza wafanyabiashara nchini Tanzania kutumia fursa ya Jukwaa hilo kujifunza, kubadilishana uzoefu, kufahamiana na wawekezaji mbalimbali na kutafuta fursa za kushirikiana na kuingia makubaliano ya kibiashara.

Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji amesema Jukwaa la Uwekezaji na Biashara Baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya limelenga kuonesha fursa mbalimbali zilizopo nchini Tanzania na faida kwa wawekezaji wa Umoja wa Ulaya. Ameongeza kwamba wafanyabiashara wa Tanzania na Ulaya watapata nafasi ya kutumia Jukwaa hilo katika kujadili njia sahihi ya kutumia fursa za uwekezaji ambazo hazijatumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo Kilimo, Utalii, Nishati, Madini, Tehama, Usafirishaji, Ujenzi na Fedha.

Pia amesema Jukwaa hilo litatoa nafasi kwa majadiliano baina ya sekta binafsi na sekta umma katika kuimarisha zaidi mazingira ya biashara na uwekezaji nchini Tanzania.

Akitoa salamu kutoka Umoja wa Ulaya Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uchumi wa Ufaransa Olivier Becht amesema ushrikiano uliopo Baina ya Umoja wa Ulaya na Mataifa ya Afrika ni nyenzo muhimu wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya Mabadiliko ya Tabianchi.

Ameongeza kwamba ushirikiano wa Tanzania na Umoja wa Ulaya ni wenye tija kutokana na Tanzania kuwa nchi inayokua kwa haraka kiuchumi hivi sasa. Amesema Tanzania inafaida mbalimbali katika uwekezaji kutokana na uwepo wake kama lango la nchi zaidi ya sita zisizo na bahari, utulivu wa kisiasa pamoja mageuzi ya kidemokrasia ndani ya muda mfupi wa Rais Samia Suluhu Hassan sio tu inasifika katika jumuiya za kimataifa bali pia katika sekta binafsi kwani serikali imekuwa ikionesha utayari katika kuondoa vikwazo mbalimbali.

Waziri Becht amesema ipo haja ya kuifanya Tanzania kama mahali pa biashara na uwekezaji kwa wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Umoja wa Ulaya.

Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya linashirikisha washiriki zaidi ya mia nane kutoka mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya pamoja na kampuni 150 za kitanzania. Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni “Changamkia Fursa za Uwekezaji za Tanzania ambazo hazijatumika”