Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Uganda nchini Tanzania Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 13 Februari 2025.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Tanzania na Uganda zimekua na uhusiano sio tu wa kihistoria bali wa kindugu. Amesema Tanzania inafuraha kuendelea kushirikiana na Uganda kwenye masuala mbalimbali katika Jumuiya za Kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002502236.jpg)
Makamu wa Rais amesema Tanzania na Uganda ni muhimu kuendelea kushirikiana kiuchumi ikiwemo kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara pamoja na kuendelea kufanya kazi pamoja katika utafiti wa kilimo, kubadilishana maarifa kuhusu kilimo cha kisasa na mazao yanayohimili ukame pamoja na udhibiti wa magonjwa yanayovuka mipaka.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema Tanzania imeendelea na jitihada za kuboresha miundombinu na nishati ili kuimarisha biashara na uwekezaji ikiwemo ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kuboresha bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuimarisha mifumo ya kidigitali ya utoaji na usafirishaji mizigo ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Uganda nchini Tanzania Mhe. Kanali Mstaafu Fred Mwesigye ameishukuru Tanzania na viongozi wake kwa kuendeleza maono ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alijitolea kusaidia nchi za Afrika ikiwemo Uganda kujikomboa na kupata uhuru.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002502237.jpg)
Ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali kupitisha mafuta yaliyogunduliwa nchini Uganda kupitia bomba la mafuta linalotoka Hoima hadi Chongoleani mkoani Tanga. Amesema ujenzi wa bomba hilo la mafuta umekuwa msaada wa kiuchumi na kijamii katika maeneo linalopita kabla hata ya mafuta hayo kuanza kupitishwa.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002502250.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002502239.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002502238.jpg)
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1002502240.jpg)