Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es salaam
Katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefanikiwa kusimamia utekelezaji wa masuala ya Muungano kwa ufanisi mkubwa kwa kuimarika kwa utaifa, umoja, amani, utulivu na hali ya maisha ya wananchi.
Hayo yamesemwa leo Aprili 19, 2024 na Makamu wa Rais wa pili wa Zanzibar, Hemed Suleman Abdulla wakati akifungua Maonesho ya Miaka 60 ya Muungano yaliyofanyika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es saalam.
Amesema Taasisi za Muungano zimekuwa na ufanisi katika kuhakikisha usawa wa utoaji wa huduma kwa wananchi wa pande zote mbili ambapo hadi sasa Taasisi 33 zimefungua Ofisi Zanzibar kati ya Taasisi 39 za Muungano.
Amebainisha kuwa kuwepo kwa Muungano kumesaidia kuimarisha hali za wananchi na kuinua uchumi wa pande zote mbili, na hali hiyo imetokana kwa kuwepo kwa soko la pamoja lisilokuwa na vikwazo vya kiutawala na kiuendeshaji linalojumuisha ushirikiano na utengamano unaorahisisha mtiririko wa rasilimali na bidhaa, mitaji, watu na huduma baina ya Tanzania Bara na Zanzibar.
“Hivyo zipo fursa nyingi za kibiashara ambapo wafanyabiashara wadogo na wakubwa wanaweza kuwekeza pande zote mbili za Muungano katika sekta za viwanda, hoteli na kujenga nyumba za biashara na makazi.
“Kwa upande wa kijamii, mafanikio makubwa yamepatikana katika miaka 60 ya Muungano kwani huduma za jamii zimeimarika hususani katika sekta ya afya, maji, elimu, ustawi na maendeleo ya jamii na makazi. Fursa za kijamii na utamaduni ni nyingi na zinazogusa mtu mmoja mmoja, vikundi na au taasisi,” amesema na kuongeza:
“Udugu wa damu umeimarika sana kwani wananchi wa pande mbili za Muungano wameungana katika misingi ya ndoa na urafiki uliojengeka na kuimarika hali hii imechangia katika kupunguza migawanyiko ya kijamii na kuondoa hisia za ukabila na ubaguzi miongoni mwetu,”.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeendelea kuchukua hatua madhubuti za kutafutia ufumbuzi wa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa masuala ya Muungano.
Amefafanua kuwa, kuanzia mwaka 2006 hadi 2024, hoja 25 zilipokelewa na kujadiliwa ambapo kati ya hoja hizo, hoja 22 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano hivyo hoja zilizobaki zipo katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi na ni Imani yangu kuwa, kwa utashi na dhamira ya dhati ya pande zote mbili, hoja zilizobaki zitapatiwa ufumbuzi.
“Katika kipindi cha miaka mitatu, 2021 hadi 2024 hoja 15 zimepatiwa ufumbuzi kati ya hoja 18 zilizokuwepo. Utatuzi wa changamoto za Muungano umeongeza imani ya Watanzania kwa Serikali zetu na hivyo kuimarisha, kudumisha amani ya muda mrefu na utulivu wa Tanzania ambao ni Tunu muhimu na fahari ya nchi yetu.
“Kwa namna na umuhimu wa kipekee, naomba nitoe shukrani zangu za dhati viongozi wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambao wameendeleza kwa vitendo Mawazo na fikra za waasisi wa Muungano,” amesema Khamis.
Kwa upande wake Meneja ukuzaji Biashara, Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania (TANTRADE) Mohamed Tajin amesema lengo la maonesho hayo ya miaka 60 ya Muungano ni taasisi ziweze kushiriki kwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya huduma wanazozitoa ikiwemo Uhamiaji ,Benki Kuu, Zimamoto na Rita .
“Tantrade tumeshiriki katika maonesho haya na tunawakaribisha wananchi kutembelea ili kufahamu huduma tunazotoa ikiwemo ukuzaji biashara ndani na nje ya nchi kupitia Maonesho yanayofanyika kila mwaka na mwaka huu yanatarajia kufanyika Juni 28 hadi Julai 13,” amesema.
Itakumbukwa kuwa uzinduzi wa maonesho kama haya ulifanyika Zanzibar Aprili 14, 2024 na Rais Dk. Mwingi ambapo katika hotuba yake aliweka wazi umuhimu wa Muungano na fursa zilizopo kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.