Na Mussa Augustine,JamhuriMedia
Serikali imesema imeandaa mjadala wa Nishati Safi ya Kupikia ili kuwepo na Sera, Sheria, Kanuni na Mifumo ya Udhibiti wa Nishati Chafu ya kupikia ikiwemo mkaa na kuni na kutumia nishati safi,salama na endelevu ili kusaidia uhifadhi wa mazingira.
Hayo yamebainishwa na leo Novemba 2, 2022, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati January Makamba, katika mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia kwenye mada iliyokuwa ikihusu Sera, Sheria, Kanuni na Mifumo ya Udhibiti ya kuwezesha nishati hiyo.
“Hili jambo hatuwezi kwenda kulifikia kwa bila kuwa na Sera, Kanuni na Mifumo ya Udhibiti ya kuwezesha Nishati Safi ya Kupikia, Je ni mifumo ipi huwezesha upatikanaji wa Nishati Safi ya Kupikia,” amesema Makamba
Waziri Makamba amesema kuwa mjadala huo wa Nishati Safi yakupikia unaweza kuwa na mitazamo tofauti ya kifalsafa na kiitikadi,hivyo jambo muhimu ni kupata njia ya kutambua wapi tunapotaka na wapi tunakwenda nakufikia mwafaka wa mikakati ya pamoja kudhibiti Matumizi ya Nishati Chafu inayo haribu mazingira kutokana na ukataji holela wa misitu.
Hata hivyo Waziri Makamba amesema kuwa moja ya kazi ya kikosi kazi kitakachoundwa kama ilivyoelekezwa na Rasi Samia Suluhu Hassan ni kuja na dira ya kitaifa na kuweka mkakati endelevu ya namna ya kufanikisha suala hilo.
Awali mchokoza mada Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Romanus Ishengoma amesema Sera ya Nishati ya mwaka 2003 na 2015 zote zinalenga kuhama kutoka matumizi ya Nishati Chafu ya kupikia kwenda kwenye matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Aidha Ishengoma alibainisha kwamba moja ya mapungufu ya Sera hiyo haitoi ufafanuzi kwamba Nishati Safi ya kupikia ni ipi na kwamba imeshindwa kutoa mwelekeo wa namna ya kufanikisha jambo hilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akichangia mada kwa njia ya mtandao kuhusu wanawake na nishati safi ya kupikia alisema katika maeneo mbalimbali hususani vijijini Mkoani Shinyanga wanawake wazee walianza kutumia nishati chafu ya kupikia ya kuni tangu wakiwa na umri mdogo na kupekelekea kuathirika macho kuwa mekundu wakati wa uzeeni na kutuhumiwa kwa vitendo vya kishirikina
Hata hvyo ameshauri Wizara ya Nishati kupeleka jukumu hilo kuanzia ngazi za vitongoji hadi mkoa kutoa elimu kuhusiana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia inayosababisha athari za kiafya,kimazingira na kiuchumi kwa ujumla.