Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla, amewaonya baadhi ya viongozi wa chama hicho wanaotoa ahadi za uteuzi kwa watia nia wa nafasi za ubunge na udiwani.
Aidha ametoa rai kwa viongozi hao kupunguza tabia ya kutoa ahadi zisizo na msingi na kuacha kuwabeba wagombea, bali waendeshe mchakato kwa haki, usawa, na kwa kufuata taratibu zilizowekwa na chama.

Akizungumza Aprili 23, 2025, na viongozi pamoja na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Kibaha Mjini, Mkoa wa Pwani, wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, Makalla alisisitiza umuhimu wa kuendesha mchakato wa uteuzi kwa haki na usawa.
Aliwataka kuacha mara moja tabia hiyo kwa kuwa si wao wenye mamlaka ya mwisho juu ya uteuzi.
Makalla alifananisha viongozi hao na watu wanaojihusisha na mchezo wa kubashiri (betting), akisisitiza kuwa ni rahisi “mkeka kuchanika” na kuwatia wagombea waliowahakikishia uteuzi kwenye sintofahamu endapo mambo yataenda kinyume.

“Safari hii tumejipanga kuhakikisha uratibu wa mchakato wa kura za maoni unazingatia ridhaa ya wananchi”
“Hivyo, viongozi msijipe mamlaka ya kuwaahidi watia nia nafasi ya uteuzi, kwa sababu maamuzi ya mwisho yako kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa,” alieleza Makalla.


