Usikimbilie kuona kikwazo fulani kuwa ni
hatima ya mambo yote. Palipo na shida
pana ushindi. Wakati wengine wanaona
shida na kukwama, wewe tazama ushindi
katika kila shida. Vikwazo vinapoibuka si
kwamba vitukatishe tamaa. Vinaibuka
tuweze kuvishinda. Usiwe na utamaduni wa
kuyakimbia matatizo, bali kabiliana nayo.
Mazingira pingamizi ndiyo yanapaswa
kukujengea nia thabiti ya kupambana na
changamoto unazokutana nazo. Binadamu
bila mateso ya kiroho, kiuchumi, kimwili,
kisiasa, kifamilia hawezi kukua.
Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kama
kahaba alipoisoma makala yangu ya ‘Nguvu
ya sala katika maisha’
, iliyochapishwa na
Gazeti la JAMHURI, alibadilisha historia ya
maisha yake, aliacha ukahaba. Baada ya
kuisoma makala ile alinitumia ujumbe mfupi
kwa njia ya simu yangu ya kiganjani,
ujumbe wake ulikuwa unasomeka hivi:
“Leo imekuwa siku njema kwangu na ni siku
ambayo historia ya maisha yangu
itaandikwa upya. Nimeisoma makala yako
ya ‘NGUVU YA SALA KATIKA MAISHA’
,
kwakweli kazi yangu ilikuwa ni ukahaba,
lakini makala yako nimeisoma kwa umakini
na nimeamua kubadilisha historia ya
maisha yangu kuanzia leo. Sitakuwa tena
kahaba, asante sana William. Mungu
akubariki sana na akupe nafasi nyingine ya
kuwasaidia watu.”
Huo ndio uamuzi thabiti na sahihi, unasubiri
nini wewe ambaye bado haujachukua
uamuzi sahihi? Siku pekee uliyo nayo ya
kubadilisha historia ya maisha yako ni leo.
Fanya uamuzi leo, usisubiri kesho wala wiki
ijayo.
Siku yako ni leo. “Wakati uliokubalika ndiyo
sasa; tazama siku ya wokovu ndiyo sasa.”
(2Kor 6:2). Ya Mungu ni mengi huwezi
kujua kama kesho utakuwepo au la. Ratiba
yako ya kuishi hapa duniani anayo
Mwenyezi Mungu.
Tumruhusu Mungu ayaongoze maisha yetu,
mpe Mungu ratiba ya maisha yako.
Uliumbwa kwa ajili ya Mungu, si kinyume
chake, na maana ya maisha ni kumruhusu
Mungu akutumie kwa malengo yake, siyo
wewe umtumie Mungu kwa malengo yako.
Zawadi pekee tunayoweza kumpa
Mwenyezi Mungu ni kumpa nafasi ya
kufanya kazi ndani mwetu kwa kurekebisha
mambo yetu yawe kama tunavyotamani
yawe. Hii itatuwezesha sisi kuwa
wanadamu wenye utashi, badala ya wale
wasiotii maagizo ya Mwenyezi Mungu.
Naomba kukunong’oneza jambo
hili: “Mwenyezi Mungu anakupenda sana.”
Ni kweli, kuna watu katika maisha yao
wamejeruhiwa sana kiroho, kimwili, kiakili,
kiuchumi, kimahusiano hata katika uongozi.
Pole sana kwa kujeruhiwa, usihuzunike
sana wala usiogope. Usisononeke kama
umejeruhiwa na mke/mme wako, kumbuka,
‘Mungu hajakuacha’. Kama umejeruhiwa na
mtoto wako, kumbuka,
‘Mungu hajakuacha.’
Kama umejeruhiwa na rafiki yako, kumbuka,
‘Mungu hajakuacha.’ Kama umejeruhiwa na
jirani yako, kumbuka,
‘Mungu hajakuacha.’
Kama umejeruhiwa na serikali yako,
kumbuka,
‘Mungu hajakuacha.’
Kama umejeruhiwa na kiongozi wako wa
kiroho, kumbuka,
‘Mungu hajakuacha.’
Kama umejeruhiwa na mwajiri wako,
kumbuka,
‘Mungu hajakuacha.’ Narudia
kusisitiza kwa msisitizo uliojaa ukweli na
hekima kwamba: “Mungu hajakukataa.
Mungu hajakuacha. Mungu anakupenda
sana.”
Kumpiga chura teke ni kumwongezea
mwendo. Waliokujeruhi walifikiri
wanakukomoa, kumbe walikuwa
wanakupiga msasa. Kwa ufasaha kabisa
mwandishi, Sariajy Rathi, anasema: “Wakati
wowote maisha yanapodondosha pini na
sindano kwenye njia yako unayopita usikae
mbali.”
Badala yake zikusanye pini zilezile ili
zisikuumize tena. Na Muigizaji, Chris Colfer,
anasema hivi kuhusu kuumizwa: “Watu
wanaokuumiza mara nyingi wachukulie
kama msasa, wanakuumiza kidogo lakini
mwisho wa siku utang’aa.”
Pokea ushauri huu: “Wasamehe wote
waliokujeruhi katika maisha yako.” Tazama
mfano wa kuigwa kutoka kwa Yesu Kristo.
Yesu Kristo aliwapa maadui zake zawadi ya
msamaha akiwa msalabani.
Zawadi yake ilikuwa katika maneno haya:
“Baba uwasamehe.” Kwa nini
wasamehewe? “Kwa kuwa hawajui
walitendalo.”’ (Luka 23:34). Shinda ubaya
kwa wema. Usilipe kisasi.
Ni rahisi kwa mtu mwema kama wewe
kutendewa usiyoyapenda. Wakati mwingine
utajikuta unakosolewa hadharani hata kama
uko sahihi. Unachekwa isivyostahili.
Unadharauriwa na kutukanwa waziwazi.
Unaimbiwa taarabu za kila aina. Tafadhali
vumilia. Usilipe ovu kwa ovu. Chukia tabia
ya kuwa na maadui wengi.