Ernest-ManguJeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewaondoa maofisa wake 32 kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (CID) na kuwapeleka katika vitengo vingine. Wamehamishwa kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kwenda kinyume cha maadili na mwenendo wa Jeshi hilo.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani, ambaye amehamishiwa Dar es Salaam kuwa Mkuu wa Chuo cha Polisi, amesema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha utendaji kazi wa Jeshi hilo.

Amesema walichokifanya ni sawa na timu ya mpira wa miguu kufanya usajili kwa kuondoa baadhi ya wachezaji na kusajili wapya ili kuleta ufanisi. Lakini amekiri kuwa utendaji kazi wa baadhi ya askari wa idara hiyo umeshuka.

JAMHURI imethibitishiwa kuwa miongoni mwa walioondolewa katika Idara ya Upelelezi ni Koplo Ally Kaburu, aliyekuwa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi (OC-CID) wa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Moshi.

Kaburu ametajwa mara kwa mara katika kashfa ya kuibwa kwa majalada ya kesi ya mauaji ya meneja wa baa ya Mo-Town, James Massawe, aliyeuawa mwaka 2009 na wafanyabiashara wanne ndugu.

Majalada yaliyoibwa yana ripoti ya madaktari walioufanyia uchunguzi mwili wa marehemu na kubaini chazo cha kifo.

Kaburu amekiri kuondolewa katika kitengo hicho na pia amekiri kuhusishwa na tuhuma hizo za kupotea kwa jalada, lakini anasema waliohusika na upotevu huo ni wakubwa wake.

Kaburu amehojiwa kwenye tume iliyoundwa na Jeshi hilo kuchunguza kupotea kwa majalada hayo. Maofisa sita walihusishwa na tuhuma hizo.

  

Malakamiko yafikishwa kwa Rais

Novemba 13, mwaka huu, familia ya marehemu James Massawe ilimwandikia barua Rais Dkt. John Magufuli, ikimuomba  aingilie kati sakata la mauji ya ndugu yao baada ya kukosa msaada kutoka kwa mtangulizi wake, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais Magufuli ameombwa aingilie kati ili watuhumiwa wanne wa mauaji hayo ambao hadi sasa wanatamba mitaani, waweze kukamatwa na kushitakiwa. Massawe aliuawa Juni 9, 2009 katika Kijiji cha Kindi, Wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.

Katika barua yao kwenda kwa Rais Magufuli, ndugu wa marehemu – Beda Massawe na Peter Massawe – wanamwomba Rais aagize uchunguzi wa mauaji hayo uanze upya bila kuwashirikisha askari wa upelelezi kutoka Ofisi ya RCO Kilimanjaro.

Chanzo cha barua hiyo kwenda kwa Rais Magufuli ni kutokana na familia hiyo kushindwa kupata msaada kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Watuhumiwa hao ambao hadi sasa hawajakamatwa ni John Joseph Kisoka (Magazeti), Mussa Joseph Kisoka, Deo Joseph Kisoka na Lucas Joseph Kisoka; ambao walitoroka baada ya mauji hayo, hivyo kesi hiyo kufutwa mwaka 2012.

“Tunakuandikia barua hii tukiwa wanyonge na tuliokata tamaa kutokana na namna watuhumiwa wanne tuliowashuhudia wakimuua ndugu yetu James Massawe Juni 9, 2009 wakiwa mitaani, huku jalada la Polisi la uchunguzi likipotea au kuibwa,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Familia hiyo imehoji nguvu waliyonayo watuhumiwa hao hadi kuweza kula njama na kuweza kuiba majalada yote yanayohusiana na mauaji hayo.

Inadaiwa kuwa jalada hilo lilikuwa limesheheni maelezo ya mashahidi muhimu sita ambao ni  Alfonsina John, Ludovick Munisi, Lelo Selengia, Peter Gerald, Boniface Munishi na Fulgence Gerald, lakini maelezo hayo yote yalinyofolewa kwa lengo la kuwalinda watuhumiwa.

Familia ya ndugu wa marehemu imemwomba Rais Magufuli afanye mambo matatu ya kuliagiza Jeshi la Polisi nchini kuwakamata wafanyabiashara hao ili kuepusha kuvuruga upelelezi; kuunda tume kuchunguza mazingira ya kuibwa kwa jalada la Polisi la uchunguzi pamoja na majalada madogo ya shauri hilo; na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliofanya hujuma hiyo.

Wameomba uchunguzi huo usihusishe askari wa Kilimanjaro ambao ndiyo watuhumiwa kama ilivyofanyika wakati wa uchunguzi wa mauji yaliyofanywa na mfanyabiashara Abubakar Jaffar (JJ) mwaka 2002