Katika kikiji cha Bambari, katikati mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati, msafara wa wanajeshi wa Urusi kutoka kundi la Wagner waliwashambulia kwa gari watu walipokuwa wakifanya mazoezi ya gwaride kwa ajili ya sikukuu ya kitaifa, Desemba 1.

Wakiwa na hasira, baadhi ya wakazi waliurushia mawe msafara huo, na vikosi vya usalama vya ndani vya Afrika ya Kati viliingilia kati na kufyatua risasi hewani kuwatawanya watu hao waliokuwa na hasira.

Kisa hicho kilitokea mwendo wa saa 4 asubuhi siku ya Ijumaa, Novemba 29, kwenye barabara kuu ya Bambari. Mamia kadhaa ya watu walikusanyika kwa ajili ya mazoezi ya gwaride wakijiandalia sikukuu ya Desemba 1, siku ya kutangazwa kwa Jamhuri, mwaka wa 1958.

Ili kuzuia kutokea kwa ajali yoyote, eneo hilo lilizingirwa na magari yalielekezwa kutumia barabara nyingine. “Wakati zoezi hilo likiendelea, msafara wa wanajeshi wa Urusi kutoka kundi la Wagner haujatii amri.

Vikosi vyetu vya usalama vilijaribu kukengeusha msafara wao, lakini walikataa, wakiendelea moja kwa moja kuelekea kwa watu hao waliokuwa wakifanya mazoezi na kuwagonga,” anaeleza Abel Matipata, meya wa Bambari.

Hali hii iliukasirisha umati ambao awali ulizuia njia kabla ya kurusha mawe kwenye msafara huo: “Ili kuzuia hali hii, vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Afrika ya Kati vilijaribu kutawanya raia hao waliokuwa na hasira kwa kufyatua risasi hewani” , anabainisha Abel Matipata.

Hakuna waliopoteza maisha
Hakuna watu waliopoteza maisha, lakini hospitali ya wilaya ya Bambari iliwatibu watu 77, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, ambao walipoteza fahamu kufuatia milipuko ya gruneti na milio ya risasi.

Shughuli zilianza tena kama kawaida wakati wa mchana. Serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) wala kundi la Wagner hawasema kuhusiana na tukio hilo.