Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amesema kuwa uchimbaji wa makaa ya mawe hususan katika mkoa wa Ruvuma umeendelea kuipaisha Sekta ya Madini kutokana na wawekezaji wengi kuendelea kujitokeza yakiwa ni matokeo ya mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na Serikali kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini.
Mhandisi Samamba ameyasema hayo leo tarehe 16 Januari, 2023 jijini Dodoma kwenye mahojiano maalum na waandishi wa habari kutoka kituo cha Imaan TV ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kipindi maalum chenye lengo la kuangalia mchango wa Sekta ya Madini katika kuwawezesha watanzania kiuchumi pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii katika mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mtwara.
Akielezea mabadiliko katika uzalishaji wa makaa ya mawe, Mhandisi Samamba amesema katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha tani milioni 1.5 za makaa ya mawe yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 211 kilizalishwa ambapo zaidi ya tani laki nane ziliuzwa nje ya nchi huku zaidi ya tani laki sita zikiuzwa ndani ya nchi na kutumika katika viwanda vya saruji.
Ameendelea kusema kuwa, kutokana na Serikali kuweka nguvu kubwa kwenye usimamizi wa uzalishaji wa makaa ya mawe, katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2022/2023 (Julai hadi Desemba, 2022) kiasi cha tani milioni 1.56 zimezalishwa na kusisitiza kuwa zaidi ya tani milioni tatu zinatarajiwa kuzalishwa ifikapo Juni mwaka huu.
Akielezea mchango wa kampuni za uchimbaji wa makaa ya mawe katika mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Samamba ameeleza kuwa kutokana na maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko kwenye mkutano wake na wadau wa madini wakiwa ni pamoja na watafiti wa madini, wachimbaji wa madini, wachenjuaji wa madini na wafanyabiashara mkoani Ruvuma mwaka jana kumekuwepo na mwamko mkubwa wa kampuni za madini ambapo ajira na huduma kwenye migodi zimekuwa zikitolewa na wazawa na huduma za jamii kuboreshwa.
“Hapo awali kampuni za madini zilikuwa zinatoa huduma za jamii kulingana na vipaumbele vyake lakini baada ya maelekezo ya Waziri wa Madini sambamba na elimu ambayo imekuwa ikitolewa na wataalam wa Tume ya Madini kuhusu ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini, matokeo makubwa yameanza kuonekana ambapo sasa kampuni za madini zinashirikisha Serikali kwa niaba ya wananchi kwa ajili ya kubaini miradi ambayo ni kipaumbele cha wananchi kabla ya utekelezaji wake,” amesema Mhandisi Samamba.
Amesema pia Serikali kupitia Tume ya Madini imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa makaa ya mawe ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu kama vile barabara, umeme kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Serikali.
Aidha, ameongeza kuwa makaa ya mawe yamekuwa yakisafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara kwenda nchi za nje huku mnunuzi mkubwa akiwa ni India, Poland na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Katika hatua nyingine Mhandisi Samamba amewataka wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini hususan katika mkoa wa Njombe ambapo yanapatikana madini aina ya shaba, dhahabu na manganese.