Tetemeko la ardhi lililotokea wiki iliyopita Mkoani Kagera, limeacha vilio na simanzi kubwa, huku baadhi ya familia zikiwapoteza wapendwa wao, uharibifu wa mali na wengine wakiachwa na ulemavu wa kudumu.

Mpaka sasa, hofu bado imetenda. Kama wanavyosema kwa aliyeng’atwa na nyoka huhofia hata mjusi, ndivyo hali ilivyo Kagera. Siku hizi hata upepo wa kawaida, unawafanya watu kukimbilia nje ya nyumba kwa hofu kuwa tetemeko limerejea.

Walioripotiwa kufariki kutokana na tukio hilo wamefikia 17, huku mpaka Jumamosi walau majeruhi wengine zaidi ya 20 wakiendelea kupata matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Kagera, iliyoko Bukoba.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wahanga John Mkurasi kutoka Kijiji cha Rugazi, wilayani Misenyi, anasema hatasahau tukio hilo, lilomwachia majonzi makubwa. Anasema mbali na kupoteza mali amepoteza sehemu ya familia yake.

“Nimempoteza mwanangu mwenye umri wa miaka tisa…aliangukiwa na ukuta wa nyumba yangu wakati wa tetemeko la ardhi, najisia uchungu sana…lakini siwezi kuhoji maana Mungu ndiye alinipa mtoto na yeye amemchukua,” anasema Mukurasi huku akigugumia kwa uchungu.

Anakumbuka wakati tetemeko hilo linatokea yeye hakuwa nyumbani, alikwenda kujishughulisha na kutafuta riziki, hata wakati tetemeko la ardhi linaacha vishindo vikubwa hakuhisi kama linaweza kusababisha maafa makubwa hasa kwenye familia yake.

“Kwangu tetemeko lile lilikuwa ni jambo la ajabu kabisa…nimekua nikisimuliwa kuhusu ‘omusisi’ (tetemeko la ardhi), ila sikuwahi kudhani kwamba siku moja nitakuja kuathiriwa na tetemeko,” anasema Mukurasi.

Mkazi wa kijiji cha Kihanga wilayani Karagwe, Yusitina Rukwalakwala anasema tetemeko hilo limemtenganisha na mumewe Marko Bigirwamungu ambaye amefariki kutokana na kuangukiwa na ukuta huko Misenyi, ambako alikuwa akifanya kazi wakati wa uhai wake.

“Nimempoteza mume wangu ambaye aliondoka hapa nyumbani kwenda kutafuta kazi Bukoba, tangu tumeoana sasa ni miaka miwili… Tukio hili la tetemeko litabaki akilini mwangu maisha yangu yote, maana limesababisha mwanangu kubaki yatima,” anasema Yustina

Anasema bado amepigwa na butwaa na haelewi maisha mapya bila mumewe yatakuwaje, huku akitakiwa kumlea mtoto yatima.  

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu, Salum Kijuu tetemeko hilo lenye ukubwa wa 5.7 katika vipimo vya richa, limegharimu maisha ya watu 17 na kujeruhi 253.

Mkuu wa Mkoa anasema, janga hilo limeangusha nyumba za makazi 840, nyumba zilizopata nyufa ni 1,264 na majengo ya taasisi yaliyoripotiwa kuanguka ama kupata nyufa ni 44.

“Katika Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wagonjwa waliokuwa wamelazwa toka siku ya janga lilipotokea walikuwa 150, hadi kufikia Jumanne ya wiki iliyopita, wagonjwa walioruhusiwa ni 76 na wagonjwa 74 wanaendelea na matibabu.”

Anasema, hatua kadhaa zimechukuliwa na serikali baada ya tetemeko kutokea kwa Kamati ya Maafa ya Mkoa na Kamati ya Maafa ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, wamefanya tathmini ya pamoja na kubainisha mahitaji yote ya haraka kwa ajili ya wananchi waliopatwa na janga la tetemeko.

Meja Jenerali (Mstaafu) Kijuu anasemakatika uchunguzi uliofanywa na wataalam kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania kuhusu tetemeko lililotokea mkoani humo,   walibainisha chanzo cha tetemeko kuwa limetokana na misuguano ya mapande makubwa ya ardhi kwenye Bonde la Ufa.

“Serikali ya Mkoa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hasa wataalam kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania inaandaa vituo mbalimbali katika mkoa ili kutoa elimu jinsi ya kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari kabla ya tetemeko, wakati wa tetemeko na baada ya tetemeko kutokea ili kujizoesha, kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga kama hayo watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru na kujiuliza kwanza wafanye nini,” anasema Kijuu.

Katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, anasema Septemba 13, mwaka huu, Serikali iliwasilisha bungeni taarifa ya masikitiko kuhusu maafa makubwa yaliyoikumba nchi tarehe 10 Septemba, kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa ya Kagera, Geita, Mwanza na Mara.

Waziri Mkuu anasema, tukio hilo ambalo liliathiri zaidi Mkoa wa Kagera lilitokea siku ya Jumamosi majira ya saa 9.27 alasiri, ambapo Mji wa Bukoba ulikumbwa na tetemeko la ardhi, lenye nguvu ya mtetemo wa kipimo cha 5.7, kwa kutumia skeli ya “Ritcher”.

“Tetemeko hilo limesababisha vifo vya watu 17 na majeruhi253. Napenda nitumie nafasi hii kwa mara nyingine kuwapa pole wafiwa wote na wale waliopata majeraha mbalimbali.

“Tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa sana wa nyumba, vituo vya afya, shule pamoja na miundombinu ya barabara. Shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na mabweni. Nyumba 840 zimeteketea kabisa, na nyingine 1,264 kupata nyufa.” anasema Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu anasema, uongozi wa Mkoa wa Kagera, Kamati ya Maafa ya Mkoa, wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, wataalamu wa masuala ya matetemeko, na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya kiasi cha hasara iliyopatikana.

Anasema serikali imefanya mambo yafuatayo, wananchi wenye mahitaji ya chakula wameendelea kupatiwa chakula kama vile, unga, mchele na maharage, sukari na chumvi pamoja na mafuta ya kula. Tathmini ya kubaini mahitaji halisi ya chakula inaendelea.

Kuhusu Matibabu, Waziri Mkuu, Majaliwa anasema Serikali imeimarisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera kwa kupeleka dawa na vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Anasema timu ya wataalam na madaktari 12 wamepelekwa Bukoba kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

Waziri Mkuu anasema, Serikali imetoa hifadhi ya makazi na wananchi wamepewa maturubai na mahema kwa ajili ya makazi ya muda. Anasema waathirika ambao nyumba zao zimebomoka kabisa, kwa kuanzia kila mmoja ametengewa mabati 20, saruji mifuko mitano, blanketi na mikeka. Pia wapangaji waliokuwa katika nyumba hizo kila mmoja ametengewa kodi ya pango ya miezi sita ili apate mahali pa kujihifadhi.

“Serikali imeshiriki katika kuwafariji wafiwa na pia kushiriki mazishi kwa kusaidia kutoa jeneza, sanda, usafiri na kutenga fedha Shilingi milioni 20 za rambirambi kwa wafiwa ambazo zitatolewa kwao muda wowote kuanzia sasa,” anasema Waziri Mkuu Majaliwa.

Red Cross washiriki kikamilifu

Wafayakazi wa shirika la Msalaba Mwekundu, wamekuwa wakitoa huduma ya kwanza kwa waathirika wa tetemeko la ardhi huko Bukoba. Wafanyakazi hao wamekuwa wakitoa huduma hizo kwenye maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko pamoja na hospitali ya Mkoa wa Kagera. Shirika hilo limefanikisha kupatikana kwa dawa za kutosha walau kuweza kuwahudumia wahanga wa tetemeko hilo.

“Wafanyakazi pamoja na wale wanaojitolea wanafanya kila linaowezekana kuwasaidia wahaga wa janga hili…ofisi ya Msalaba Mwekundu inaendelea kufuatilia na kushiriki kwa karibu katika janga hili kubwa,” anasema Andreas Sandin, kiongozi wa shirika hilo kwa Afrika Mashariki na Visiwa vilivyoko Bahari ya Hindi.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti viongozi wa serikali kutoka Kagera wamesema tetemeko hilo limeacha uharibifu mkubwa wa maisha na mali na kuomba Watanzania kujitokeza kwa wingi kutoa misaada ya hali na mali kwa wahanga kipindi hiki kigumu.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Augustine Ulomi anasema Jeshi la polisi lipo imara katika kipindi hiki cha matatizo kuhakikisha linatoa ulinzi katika maeneo yote yaliyokumbwa na matatizo.

“Tangu kutokea kwajanga hili tumeimarisha ulinzi mara dufu hasa katika maeneo yote yaliyokumbwa na tetemeko hili. Ulinzi huu unalenga kuwalinda wananchi na mali zao dhidi ya vibaka wanaoweza kutumia hali hii kuiba,” anasema Ulomi.

Anasema  tangu kutokea kwa tetemeko hilo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wilaya zimehakikisha ulinzi unaimarishwa katika maeneo yaliyokumbwa na janga hilo, huku akisisitiza kwamba Jeshi la Polisi limefanikiwa kwa asilimia kubwa.

“Kwa kuwa watu ni wengi inatokea katika kutafuta namna ya kujiridhisha kujua yupi anaenda kwa kutoa huduma na nani anaenda kwaajili ya kukwapua ama kuchukua vile ambavyo vimezagaa zagaa, kwahiyo ndio maana utaona mwingiliano wa aina hiyo,” anasema Ulomi.

Anasema kwa ujumla Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mamlaka husika ziko imara kukabiliana na aina yoyote ya uhalifu inayoweza kutokea katika kipindi hiki kigumu kilichowapata wananchi wa Kagera.

“Siku zote jeshi la polisi limekuwa imara kukabiliana na janga la aina yoyote…tunachoweza kuomba kutoka kwa wananchi ni ushirikiano katika kipindi hiki kigumu ndani ya mkoa wetu,” anasema Ulomi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk. Herman Kabirigi anasema walipokea majeruhi wengi zaidi ya 200 na kufanyiwa uchunguzi  wa afya zao na wengi kuruhusiwa kuondoka wengine ilibidi walazwe na kuwafanyia uchunguzi zaidi kutokana na kuwa katika hali mbaya.

“Wengi wao walipata zaidi mshtuko ndiyo maana tukaamua kuwalaza ili tuendelee kuwapa uangalizi wa karibu mmoja tu ndiye amevunjika mkono wa kulia, lakini wengine walipata michubuko miguuni, mikononi na usoni,” anasema Kabirigi.

Anawataja waliolazwa wakiwa katika hali mbaya baada ya tukio kuwa  ni Deogratius Nandi (31), Paulin Masolwa (27), Omary Hussein (24), Hamisi Haji (29) ambao wote ni wanaume. Majeruhi wa kike ni Cecilia Mussa Kabona (28) na Mwazanije Hassan (23) ambaye amevunjika mkono wa kulia. Waliopata matibabu kuruhusiwa ni Mashaka Shabani (42), Khalifa Rashid (26) na Joel Cheja (21).

Anasema kulikuwa na majeruhi wengine, lakini hao aliowataja walikuwa na hali mbaya kiasi cha wengine kulazimika kufanyiwa upasuaji kwa lengo la kuokoa maisha yao.

Anasema pamoja na kupata misaada ya kitabibu kutoka Hospital ya Rufaa ya Bugando, bado wameendelea kupata misaada kutoka kwa madaktari wasiokuwa na mipaka na tayari wametoa dawa zenye thamani ya Sh milioni 11.

Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, anayeshughulikia uokoaji, Brighton Monyo anasema jeshi hilo limeshiriki kikamilifu katika janga hilo pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Vijana wangu kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi walijitahidi kupambana kadri walivyo weza kutoa uduma muhimu kwa majeruhi wa janga hilo pamoja na changamoto za ukosefu wa vifaa unaotukabili hasa mikoani,” anasema Monyo.

Anasema pamoja na upungufu huo wa vifaa, lakini jeshi la zimamoto limekuwa imara siku zote kupambana na janga lolote linaloweza kutokea hapa nchini hili limekuwa likiwezekana kwa ushirikiano wa wananchi.

“Kusema ukweli jeshi letu linakabiliwa na uhaba wa vifaa hasa katika vituo vyetu vya mikoani hali ni mbaya…hali hii imesababisha sisi kutokueleweka kwa wananchi yanapotokea majanga,” anasema Monyo.

 

Matetemeko ya ardhi yaliyotikisa Tanzania

Desemba 2002 kulitokea tetemeko la ardhi mkoani Mbeya nyumba nyingi zikabomoka na nyingine kupata nyufa na eneo lililoathirika zaidi ni Wilaya ya Rungwe. 

Desemba, 2012 yalitokea matetemeko mfululizo na kuibua hofu kwa wananchi wa Wilaya ya Kyela na Mji wa Karonga ulioko Kaskazini ya Malawi ambao uko jirani na wilaya hiyo.

Taarifa kutoka kituo cha Dodoma kinachofuatilia matukio ya matetemeko nchini zilionesha kuwa tetemeko la kwanza lililotokea siku ya Jumapili Desemba 6, mwaka huo na kufuatiwa na jingine saa 11 Alfajiri, siku ya Jumanne Desemba 8 na jingine lilitokea saa 11:27 alfajiri, Desemba 12, mwaka huo.

Taarifa ya Wakala wa Jiolojia nchini (GST) ilieleza kuwa matetemeko hayo matatu yalianzia Kaskazini mwa nchi ya Malawi na kusambaa hadi Kusini Mashariki mwa Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wakala wa Jiolojia, tetemeko la kwanza lililotokea Desemba 6, mwaka huo lilikuwa na ukubwa kipimo cha 5.2 ritcher, lililofuata lilikuwa na kipimo cha 4.8 na la mwisho lilikuwa kishindo kikubwa zaidi cha 5.9 ritcher.

Kutokana na matetemeko hayo Wilaya ya Kyela iliathiriwa zaidi kwa upande wa Tanzania kutokana na kuwa karibu na nchi ya Malawi na kwamba baadhi ya nyumba zilibomoka.

Wilaya nyingine zilizokumbwa na matetemeko mkoani humo ni Mbozi, Mbeya Vijijini na Mbeya Mjini, Rungwe, Chunya, Mbarali na Ileje.

Tetemeko jingine ambalo ni kubwa kutokea nchini ni lile lililotokea Oldonyo Lengai, Mkoa wa Arusha mwaka 2007 likiwa na kipimo cha ukubwa wa kishindo cha 5.9 ritcher.

 

Wanataaluma

Jumuiya ya Wanataluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na majanga ya asili yanayotokea katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutoa msaada wa kitaalam na kuwasaidia waathirika wa majanga hayo.

Mtaalam wa Jiologia wa chuo hicho, Dk.Elisante Mshihu anasema jumuiya itaendelea kutoa elimu na taarifa sahihi kwa umma kupitia tafiti mbalimbali zinazohusu matetemeko ya ardhi kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na majanga hayo.

“Matetemeko ni hali ya kawaida duniani na kwa hapa kwetu yamekua yakitokea katika mikoa ya Dodoma, Arusha, Kagera na Singida, hivyo ni vyema wananchi wakafahamu namna ya kukabiliana nayo pindi yanapotokea,” anasema Dk. Mshihu.

Dk. Mshihu amesema elimu na taarifa sahihi ni nyezo madhubuti ya kukabiliana na majanga ya asili kokote duniani na kuongeza kuwa uwekezaji katika elimu ni jambo linalohitajika kwa sasa nchini.

“Itabidi elimu ya juu na vyombo vya habari vijengewe uwezo wa kifedha na kitaaluma ili kutimiza majukumyu yake wakati wa kukabiliana na majanga haya ya asili,” amesisitiza Dk.Mshihu.

Anasema Jumuiya ya Afrika Mashariki inapaswa kuelekeza nguvu zake katika eneo hilo kwani kijiografia na kijiolojia inaonyesha nchi zote wanachama ziko katika hatari ya kukubwa na majanga ya asili.

 

Maafa mengine yaliyowahi kutokea Mkoani Kagera

 Vita ya Kagera 1978/1979

“Historia inaonesha kwamba mkoa huo ulikumbwa na vita, ndugu, jamaa na wanafamilia wetu wakapoteza maisha, lakini haikuwa tu kuutetea mkoa huo bali ilikuwa ni kurudisha heshima ya nchi yetu.”

 

Utawala wa hayati J.K. NYERERE

 Maradhi ya Ukimwi 1980

Historia inaonesha kuwa Mkoa wa Kagera uligubikwa na janga sugu la Ukimwi, vilio, majonzi na misiba ikawa kila familia. Maeneo yaliyoathirika zaidi yalikuwa ni kata za Kanyigo, Kamachumu na Muleba.

 

Mei 21, 1996

Historia inaonesha kwamba watu zaidi ya 1,000 walipoteza maisha katika tukio la ajali ya meli ya MV Bukoba, tukio ambalo Wahaya walisema historia yake haitafutika akilini wala vinywani mwao (Tikiliwa Igamba).

 

Mwaka 1997

Mkoa wa Kagera ulikumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua za Elnino.

 

Mwaka 2012-2014

Kimbunga kiliutawala mkoa huo ikaandikwa kuwa historia tena, nyumba ziliezuliwa, migomba ikaanguka, watu wakakosa malazi, chakula hata miundo mbinu ikaharibiwa.  

 

 Julai 2015

Takribani watu 600 walinusurika kifo baada ya meli ya MV Serengeti kushindwa kutia nanga Kemondo kwa saa 6 ikipepesuka.