Tafadhali rejea mada yangu ya “Serikali za Mitaa ndio Injini ya Maendeleo”uliyoitoa katika Gazeti la JAMHURI la tarehe 6 – 12, 2016. Nilipata maoni kutoka kwa wananchi na wasomaji wako kadhaa. Wengi wao walikubaliana na fikra za mada husika.

Hata hivyo, mmoja wa wasomaji wako, Ndugu Itogile, hakukubaliana na baadhi ya maelezo hayo. Nimshukuru sana Ndugu Itogile kwa kunipa fursa ya kuendelea kuelimishana kuhusu mfumo wa Serikali za Mitaa. Kutokana na umuhimu wa masuala aliyohoji nasukumwa kutoa ufafanuzi wa ziada kwa faida ya wasomaji na wananchi kwa ujumla.

Lengo la ufafanuzi huu ni kutaka kujikumbusha tulikotoka ili kutambua wapi tulikokosea tuweze kujisahihisha. Yeye anasema: “Mheshimiwa Kilembe, hakika huko sahihi. Mheshimiwa tunakuelewa. Lakini iweje mapigano ya wafugaji na wakulima. Iweje uchafu uliokithiri. Iweje umbumbumbu kwa wananchi kutokuwa na mwamko wa elimu ya uraia. Iweje sisi tuliostahili kuyarekebisha haya tusiweze wakati tu wataalamu tunangojea bajeti za Serikali Kuu. Na kile kidogo kilichokuwa kinapatikana kinaishia katika shughuli za uendeshaji badala ya kujikita katika mipango endelevu kuondosha yanayozuia ustawi wa jamii.

“Kutoka Bukoba hadi Dar es Salaam ni takribani kilometa 1,400 wakati ni takribani kilometa 900 kwenda Dodoma. Je, huoni kuna unafuu katika bajeti ya Halmashauri ya Bukoba endapo italazimu kwa kuokoa muda na gharama ya usafiri. Tukiwa makini katika madogo ndio mwanzo wa kuyaweza makubwa. Hatua ya kuhamia Dodoma hakika ina mahusiano na Serikali kuwa karibu na wananchi kwa kupunguza mvuto wa rasilimali kulimbikizwa mahali pamoja.

“Historia yasema hata miji karibu na mji mkuu itanukia u-mji mkuu ati. Mstaafu mwenzangu tusipende kubeza maamuzi (uamuzi) yaliyotafitiwa, vinginevyo maendeleo tutayasikiaga kwa wengine”.

Sasa niruhusu kutoa ufafanuzi kwa kipengele kimoja kimoja cha maoni ya hapo juu.

Kwanza kabisa nataka niseme niko sahihi kutokana na maelezo ya ziada ya hapo chini ili Ndugu Itogile anielewe.

Hebu na tutafakari kuhusu Mapigano ya wafugaji na wakulima.

Waanzilishi wa mfumo wa Serikali za Mitaa Tanganyika (Muungano wa Mataifa (League of Nations) 1922 na Gavana Cameron 1925) waliamini na kuazimu kwamba Tanganyika ingeendelea kuwa nchi ya upendo, tumaini, mshikamano na umoja miongoni mwa makundi ya makabila yake tofauti tofauti. Imani yao ilitokana na historia ya wahenga wetu kwamba walikuwa jamii yenye umoja, upendo na mshikamano pevu kwa kuwa makundi ya mbari mbalimbali za nchi hii yalikuwa yametangamana na kuishi kwa pamoja bila migogoro.

Mshikamano huo ulitokana na mfumo-jadi wa demokrasia-shirikishi ya kweli ya kiserikali za mitaa (mwafaka) ambayo wenyeji wa Tanganyika (na penginepo Bara la Afrika) walikuwa wakiitumia kusimamia na kuendesha shughuli zao mbalimbali za kimaisha.

Ushahidi mzuri sana wa upendo, umoja na mshikamano uliokuwapo miongoni mwa makundi hayo nchini Tanganyika ni jinsi wenyeji kutoka maeneo tofauti tofauti walivyoshirikiana kuendesha vita takribani sita dhidi ya Wajerumani walipojidukiza nchini bila ridhaa yao. Kilele cha mapigano hayo kilifikiwa kwa Vita (Kuu) ya Maji Maji mwaka 1905 – 1907. Katika Vita hiyo makundi ya makabila ya wenyeji tokea kwa Wandengereko (Kinjekitile), kupitia kwa Wangoni (Chabruma) hadi kwa Wahehe (Mkwawa) yalishikamana na kushirikiana kupambana kwa ujasiri na adui wa wote; kwa zaidi ya miaka miwili.

Umoja na mshakamano huo wa ajabu ulisababisha taharuki kubwa kwa Wajerumani. Katika historia ya Tanzania mapokeo ya moyo wa umoja na mshakamano adimu wa aina hiyo yalikujaibukia na kujirudia tena baadaye sana na wanaharakati wa TANU- mwaka 1954 wakati makabila mbalimbali ya Tanganyika yalipoungana kwa uzalendo kupambana na Serikali ya Uingereza wakipigania uhuru.

Kati ya makundi ya makabila yaliyopambana na Wajerumani mwaka 1905-1907 na pia wanaharakati wa TANU mwaka 1954-1961 walikuwamo miongoni mwao wakulima na wafugaji. Kwa mila zao wakulima na wafugaji ni mahasimu kwa sababu wafugaji huwachokoza wakulima wakapeleka mifugo yao kula mazao ya mashambani kwao. Ili kuishi kwa upendo na mshikamano miongoni mwao; wakulima na wafugaji hao hutumia jadi ya mwafaka kuwekeana mipaka ya kila kundi kuendeshea shughuli zao za kimaisha. Siku Wajerumani walipovamia koloni lao la Afrika Mashariki, kutokana na jadi ya mwafaka makundi hasimu (wakulima na wafugaji) yaliungana kwenda kupambana na adui wa wote. Hapo baadaye jambo hilo liitokea vivyo hivyo kwa wakulima na wafugaji walipoungana enzi za TANU.  

Wajerumani walipojidukiza katika koloni la Ujerumani ya Afrika Mashariki walitumia msingi sawia na mwafaka kuzuia migongano na migogoro kati ya makundi mbalimbali ya koloni lao. Hima hima waliigawa Tanganyika katika mapande makubwa makubwa ya wilaya 22 ambazo zingine zilivuka mipaka ya kikabila. Katika harakati hizo walibaini hatari iliyokuwa ukingoni ambayo ingeliweza kusababisha mlipuko wa mapigano makali kati ya makundi hasimu mawili ya wafugaji na wakulima: wa-Nilotiki (Wamasai) kutoka Kaskazini na Wabantu (Wazulu – Wangoni) wakulima kutokea Kusini (Soma Judith Listowel – The Making of Tanganyika 1967).

Makundi haya mawili yenye nguvu za kivita yalikuwa njiani kukabiliana uso kwa uso kwenye eneo la katikati mwa mbuga za Tanganyika. Wamasai walikuwa wakisaka mbuga za malisho kutokea Kaskazini kusonga “Tanganyika” ya Kati ambako Wangoni walikuwa wakisonga Kaskazini kupanua himaya yao kwa kuteka makabila mbalimbali njiani walimopita. Mgongano huo ungelisababisha vita na umwagaji damu kwa makabila mengine madogo madogo yasiyohusika kadri ilivyowasibu wanambari mbili tofauti hao. Jambo walilofanya Wajerumani ili kuzuia na kukomesha mapambano tarajiwa ni kuunda mipaka ya wilaya za Umasaini (Monduli) na Ungoni (Songea) na zinginezo na hivyo kudhibiti kila kundi kubakia katika eneo lake.

Utawala-gandamizi na onevu wa Wajerumani dhidi ya wenyeji ulisababisha mlipuko wa Vita Kuu ya Kwanza ambako Wajerumani walipigwa vibaya mwaka 1916 na kurejeshwa makwao.

Ni dhahiri kuwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza wanachama wa Jumuiya ya Muungano wa Mataifa walivutiwa sana na mfumo wa umoja na mshikamano wa kipekee kabisa ambao uliwawezesha Wafrika nchi nzima kuungana kutokana na mfumo wa kiserikali za mitaa wa mwafaka. Wenyeji wasiokuwa na mkuu wa majeshi wa makabilia yote, bali wakiamini kimwafaka katika nguvu za pamoja huku wakitumia matambiko na mitishamba (maji maji); walitumia mikuki, mishale ya sumu na magobole yaliyojaa kutu (Mwalimu Nyerere Freedom and Unity 1956) wakapigana kishujaa na maadui waliokuwa na mfumo pevu wa Amiri Jeshi na Majenerali Wakuu kutoka Berlin walioamrisha matumizi ya mizinga na silaha kali kali na kubwa sana.

Kutokana na hali halisi hiyo wakati Jumuiya ya Muungano wa Mataifa ikiidhaminisha Tanganyika kwa Serikali ya Uingereza mwaka 1922 iliielekeza Serikali hiyo kuendesha himaya yao kwa kuoanisha (graft-in) mfumo wa demokrasia ya kisasa ya Uingereza na demokrasia-shirikishi ya kweli ya mwafaka ya Waafrika. Hivyo kungelitokea Mfumo wa Serikali Kuu za Kiafrika na Mfumo wa Serikali za Mitaa za Kiafrika. Kwa silika ya mwafaka mfumo huo hutokana na kizio cha makubaliano yanayoridhiwa na watu wa makundi mbalimbali yote kwa ujumla kama utaratibu wa kuendesha shughuli za maisha ya makundi yao tofauti.

 

>>ITAENDELEA>>

 

Mwandishi wa makala hii, Jeremiah Kilembe ni mtumishi mstaafu wa Serikali za Mitaa. Anapatikana kupitia barua pepe: [email protected]

Simu: 0685214691