MAGUFULIKwanza nakushuruku Mhariri kwa kuipa nafasi makala yangu iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho: “Ndani ya Dk. Magufuli, namuona Mwalimu Nyerere”, iliyochapishwa katika toleo namba 211 la Gazeti la JAMHURI.

Nimepata wasomaji wengi sana walionipigia simu na wengine walioniletea ujumbe mfupi wa maandishi. Wote nawashukuru sana. Kitu kimoja nilichokibaini ni kwamba Watanzania kwa sasa wanasoma sana habari za uchaguzi, hii ni kuonyesha kuwa elimu ya uraia inapanuka kwa kasi. Hongereni sana.

Nimepata ujumbe mwingi wa pongezi, lakini pia nimepata mwingine wa kunibeza, na hata kufikia hatua ya kutumiwa kwa lugha isiyo na staha.

Mmoja wa wasomaji ameniandikia ujumbe huu: “Nimestushwa na makala yako ndani ya Gazeti la JAMHURI kumwona Nyerer ndani ya Magufuli. Naomba unijuze uliyoandika kwa maagizo ya mtu au from your heart? U leaves a lot to be desired! Unalinganisha kichwa na miguu.”

Mwingine akaandika: “Nakupongeza sana kwa makala yako katika Gazeti la JAMHURI toleo 211 Uk. 3 ‘Ndani ya Magufuli namwona Mwalimu Nyerere”. Kuhusu barabara Kyabakari hadi Butiama naomba tuongee nikupe undani wake maana mimi kama Mshauri na Msaidizi Mkuu wa Hayati J. K. Nyerere niliyeishughulikia kwa kuwasiliana na Mwalimu na hata baada ya J.K Nyerere  kufariki. Hongera kwa yote ila tuwasiliane tafadhali…”

Hawa wawili ni kati ya wasomaji wengi sana waliowasiliana na mimi, ama kwa ujumbe mfupi wa maandishi, au kwa kunipigia simu.

Wale walionipinga, wanasema Dk. Magufuli hamkaribii wala hawezi kuwa na sifa za kumlinganisha na Mwalimu. Wanatoa sababu kadhaa za kuhalalisha kauli zao.

Mimi sipendi malumbano na kwa sababu hiyo nilidhani baada ya kuandika makala ile mambo yangeishia pale, lakini kwa kuwa baadhi ya ujumbe na simu zimekuwa na msimamo tofauti, nimeona niombe nafasi tena ili niweke wazi msimamo wangu.

Sioni aibu wala sitasita kusema kuwa kati ya wagombea urais hawa wanane waliojitokeza, Dk. Magufuli ndiye kiongozi anayestahili kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama. Dk. Magufuli ndiye anayestahili kuwa Rais wa wa Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wale wanaonipinga, naomba wanipinge kwa hoja. Wanaompinga au kumchukia Magufuli, naomba wafanye hivyo kwa hoja badala ya hisia au jazba zisizokuwa na mahali pa kujiegemeza.

Wapo wanaosema Dk. Magufuli ana uamuzi wa kukurupuka, wapo wanaosema eti haambiliki; wengine wanasema ni dikteta anayefanya kile anachoamini, na wengine wanasema maneno ya kila aina.

Kwa bahati nzuri kati ya wale wachache wanaomchukia Dk. Magufuli, ukiwauliza sababu zinazowafanya wamchukie, utabaini kuwa hawana sababu za msingi, isipokuwa ni wale ambao wameathiriwa kwa namna moja au nyingine na mkono wa chuma wa Dk. Magufuli wa kuongoza kwa kusimamia misingi ya sheria.

Miongoni mwao ni wale wakazi wa Ubungo-Mlandizi ambao walivamia hifadhi ya barabara, lakini wakaondolewa na Magufuli ili kupanua barabara ya Morogoro. Kuna msemo wa kwamba “kutojua sheria si kigezo cha kutohukumiwa kwa kuivunja sheria hiyo”. Wale waliojenga barabara ndani ya Hifadhi ya Barabara ya Morogoro, na kwingineko nchini, iwe kwa kujua au kwa kutokujua sheria, walistahili kuondolewa. Kabla ya mtu kununua kiwanja mahali popote, wajibu wake wa msingi kwanza ni kwenda kwenye mamlaka husika ili kujiridhisha kama eneo husika ni halali kwa ujenzi au kwa shughuli anayokusudia kuifanya.

Watanzania kwa kupenda njia za mkato, na kwa kupenda vitu vyepesi vyepesi, wamekuwa hawajisumbui kupata ukweli wa mahali wanakokusudia kununua au kujenga. Wamekuwa wepesi wa kurubuniwa na kujikuta wakinunua maeneo ambayo kisheria ni makosa.

Barabara ya Morogoro inajulikana wazi kuwa tangu mwaka 1932 ipo sheria yake ya hifadhi. Sheria hiyo imeendelea kuhuishwa kila mara tangu wakati huo hadi sasa. Ni nchi ya wajinga tu wanaoweza kuamua kupungua upana wa barabara kama hiyo wakati wanaona idadi ya watu na magari ikiongezeka. Kama wakoloni walikuwa na akili ya upana wa barabara kiasi hicho, leo Watanzania wamelogwa na nani hata waone hifadhi hiyo ni kubwa sana?

Vibanda au nyumba zilizojengwa ndani ya hifadhi ya barabara havina thamani kubwa ikilinganishwa na adha wanazopata Watanzania na watumiaji wengine wa barabara kutokana na ukali wa foleni. Kwa maneno mengine ni kwamba ni jambo la busara kuwaondoa hao wachache ili watu wengi wapate kufaidika kwa huduma za kiuchumi na kadhalika.

Dk. Magufuli katika uongozi wake mara zote ameshasema wale wanaostahili fidia, watalipwa bila shaka yoyote, lakini wale ambao wapo ndani ya hifadhi kinyume cha sheria kwa matarajio kuwa watalipwa, wanajidanganya. Kwenye kampeni zake amelisema hilo kwa uwazi kabisa bila kuogopa kukosa kura. Angekuwa mnafiki wa aina yake kama ukweli huo angewaficha wananchi kipindi hiki anachoomba kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kitu kingine kinasemwa kuhusu Dk. Magufuli, ni uuzaji wa nyumba za Serikali. Kweli, ukiacha dosari za hapa na pale, suala la uuzaji nyumba za Serikali halikuwa na Dk. Magufuli. Yeye alikuwa mtekelezaji tu wa jambo lililoamuriwa na Baraza la Mawaziri. Hivi tujiulize, Magufuli ni nani hata aweze kuamua uuzwaji nyumba za umma?

Tukubaliane kuwa kuna dosari zimejitokeza kwenye mpango huo, kama vile kuuzwa kwa nyumba za watumishi zikiwa ndani ya maeneo ya hospitali, Mahakama, Polisi na kadhalika. Dk. Magufuli ni mtu mwenye akili timamu. Amesikia kilio na ameona dosari hiyo. Bila shaka akiwa Rais atazirejesha baadhi ya nyumba zilizouzwa kwa makosa. Hilo linawezekana.

Anazungumzwa kuhusu meli ile ya uvuvi. Wapo wanaosema kaitia hasara Serikali. Hii ni hoja mfu. Hapa ikumbukwe kuwa Mahakama Kuu iliwatia hatiani wale wavuvi, alini kwenye Mahakama ya Rufaa mambo yakawa tofauti.

Siyo siri kuwa Mhimili wa Mahakama, kama ilivyo Serikali na Bunge, nako kuna vitendo visivyo vya uadilifu. Inawezekana kupinduliwa kwa uamuzi wa Mahakama Kuu ni matokeo ya udhaifu wa utetezi ndani ya Serikali, au ni udhaifu katika Mhimili wa Mahakama. Lililo wazi ni kwamba wale wenye meli walikuwa wakivua katika eneo la Tanzania kinyume cha sheria, na hilo halikubariki kamwe.

Kwa kuwa Dk. Magufuli wiki ijayo anaweza kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atakuwa mkuu wa dola. Hapo anaweza kushirikiana na mihimili mingine kujenga uzalendo ili hata mahakimu na majaji nao wajione kuwa wana wajibu, si wa kutenda haki tu, lakini kulinda na kuweka mbele maslahi ya Taifa letu. Mahakimu na majaji si malaika. Miongoni mwao wapo wenye udhaifu kama ilivyo kwenye waendesha mashitaka, na kadhalika. Huu ni wakati wa mabadiliko. Mabadiliko yasiwe serikalini pekee, bali yafike hadi kwenye mihimili ya Mahakama na Bunge, ambayo kama ilivyo Serikali, nayo imekuwa ikinyoonyeshwa vidole kutokana na mienendo isiyo ya kizalendo.

Imani yangu ni kuwa Oktoba 25 Watanzania wengi watajitokeza kupiga kura, kwa bila shaka yoyote chaguo lao litakuwa Dk. Magufuli.

Nchi yetu sasa inamhitaji kiongozi mkweli na mchapakazi ambaye atakuwa na dhamira ya kweli ya kupambana na rushwa. Uongozi wa Awamu ya Nne umelea madudu mengi sana.

Rais Jakaya Kikwete anaelekea kumaliza ngwe yake. Anaondoka nchi ikiwa imelegea sana kwenye usimamizi wa sheria. Vyombo vya dola ni kama vile navyo vimepigwa ganzi. Tunamhitaji Rais wa aina ya Magufuli ambaye hatakuwa na simile na wala rushwa, wazembe, warasimu na viongozi wasiokuwa na maono ya kuwatumikia Watanzania.

Hatutakiwa kuwa na nchi ambayo mtu atakuwa na uhuru wa kuamua kuheshimu, au kutoheshimu sheria. Kila mmoja ajue kwenye uongozi wa Awamu ya Tano kila mmoja atapaswa kuzitii na kuzifuata sheria. Sioni mwingine zaidi ya Dk. Magufuli, katika kulifikia tamanio hilo.

Wale wanaodhani kuwa nimetumwa na Dk. Magufuli kuyasema haya wananionea, na pengine hawanijui. Hawanijui kwa sababu mimi si mtu wa kumung’unya maneno, hasa tunapokuwa tukijadili suala la nchi.

Wale wanaomwandama Dk. Magufuli ni wale waliokuwa wamezoea kufanya mambo kwa mazoea bila kuchukuliwa hatua zozote. Sasa wanajua anaingia mtu ambaye hana mjadala na wavunja sheria. Tayari wameshaingiwa na kihoro.

Rwanda tunayoiona sasa ni matokeo ya uongozi thabiti wa Rais Paul Kagame. Nchi hiyo imeshatupita kwa kila kitu, wakati tunajua miaka mkichache iliyopita wananchi wake waliuana kama kuku. Kama si uongozi madhubuti wa Kagame, Rwanda leo ingekuwa kwenye hali mbaya zaidi.

Wale wanaonipinga naomba wajitokeze hapa wanipe mfano wa Taifa moja au mawili ambayo yamewezxa kusonga mbele kimaendeleo kwa viongozi wake kuwachekea wavunja sheria, wakwepa kodi, majizi au watu wasiopenda kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Wajitokeze waseme Marekani imefikia maendeleo yake kwa sababu waasisi wake walikuwa viongozi wa kuchekacheka tu badala ya kuwahimiza watu kufanya kazi na kuheshimu sheria.

Wale wanaodhani kuwa Dk. Magufuli ni kiongozi dhaifu, wasubiri aapishwe ndipo watakapojua kuwa chaguo hili ni sahihi.

Juzi nilikuwa Kibondo. Nimewakuta baadhi ya wafanyabiashara wenyewe wakienda kukata leseni za biashara. Nilipowauliza wakasema wanafanya hivyo kwa sababu wanajua Dk. Magufuli, akiwa Rais hatakuwa na mchezo na wakwepa kodi na watu wasiotaka kufuata sheria.

Nami nawaambia wananchi wafuate mfano wa hawa wananchi wa Kibondo. Waanze kujiandaa kuwa raia wema maana kiongozi anayekuja hatakuwa na mzaha. Huyu ni mtu sahihi sana kwa wakati huu ambao Tanzania eti tunazidiwa nguvu za kiuchumi na nchi iliyokuwa na hali mbaya kabisa kama Ethiopia.

Kama ni Dk. Magufuli huyu ninayemfahamu, naapa kuwa miezi mitatu pekee inatosha kuiona Tanzania ikiwa mwenye mweleo mpya wa kimaendeleo. Huyu hatakuwa Rais wa safari za nje, ni Rais wa kazi tu, tena kazi za ndani. Hana sababu ya kwenda kuhemea-hemea nje. Anajua Tanzania ina kila kitu kinachoifanya isiwe na sababu ya kuongozwa na kiongozi ombaomba. Subiri mwanaume huyu na mwana mama yule mzaidizi wake waje kuinyoosha Tanzania. Muhimu hapa ni wananchi kuwa tayari kuyakubali mabadiliko anayotaka kuyaleta. Kwake Dk. Magufuli, ukifuata sheria utaishi mithili ya mtu aliye peponi. Ukifanya kinyume hutakosa kulalamika na kumuona kuwa ni dikteta. Karibu Dk. Magufuli.

 

Mwandishi wa makala hii amejitambulisha kuwa ni msomaji wa JAMHURI anayepatikana kupitia simu 0789 117 972