*Serikali yafungua mlango uwekezaji katika viwanda
*Mbowe ataka elimu, gesi itumike kuzalisha umeme
*Zitto apendekeza kodi ya maji Sh 160 kama umeme REA
*Wabunge wapendekeza tozo ya maji miamala ya simu
Na Waadishi Wetu, Dodoma
Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii, Serikali na vyama vya upinzani wameungana kifikira kutafuta mwarobaini wa kuondoa umaskini kwa Watanzania.
Serikali kwa upande wake, imeacha kuongeza kodi katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2018/2019 kwenye sigara, soda, bia, mafuta na bidhaa nyingine kama ilivyozoeleka, inaamini katika ujenzi wa viwanda kuwa vitaongeza ajira, mauzo ya ndani na nje hivyo kuongeza fedha za kigeni.
Pia Serikali imechukua hatua za makusudi kulinda viwanda vya ndani suala ambalo kimekuwa kilio cha muda mrefu, huku ikishusha kodi kwa bidhaa zinazozalishwa ndani kama njia ya kuvutia na kuhamasisha uwekezaji wa ndani.
Serikali inachukua hatua hizi kutokana na changamoto inazokabiliana nazo, ambazo imeamua kuzisema bila kificho, likiwamo bomu la ajira kwa vijana wanaohitimu mafunzo katika ngazi mbalimbali za elimu.
“Ukosefu wa fursa za ajira hasa kwa vijana, ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 10.4 ya Watanzania hawana ajira. Vile vile kati ya vijana wanaohitimu masomo ya vyuo vikuu wapatao 800,000 kila mwaka, uwezo wa Serikali kuajiri ni wastani wa watu 40,000 tu,” amesema Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango wakati anawasilisha bajeti kuu ya Serikali bungeni, Alhamis iliyopita.
Amezitaja changamoto nyingine zinazoikabili nchi kuwa ni; kiwango kikubwa cha umaskini ambapo taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kuwa ingawa kiwango cha umaskini kimepungua kidogo kutoka asilimia 28.2 (2011/12) hadi asilimia 26.4 (2015/16), bado kiwango hicho ni kikubwa.
Sekta ya kilimo (inayojumuisha mazao, mifugo na uvuvi) ambayo inaajiri asilimia 66 ya Watanzania na kuchangia asilimia 30 ya Pato la Taifa, bado inaendelea kukua kwa kasi ndogo ya wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita kutokana na uwekezaji mdogo, tija ndogo na kutegemea mvua, sambamba na mchango mdogo wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa wa asilimia 5.5.
Mahitaji makubwa ya upatikanaji wa huduma muhimu za jamii (hasa maji, afya na elimu bora) na yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu (asilimia 3.1 kwa mwaka). Aidha, hali ya miundombinu ya umeme, usafiri na usafirishaji (barabara, reli, usafiri wa anga na majini) bado haikidhi mahitaji ya uchumi kukua kwa kasi zaidi na kugusa wananchi wengi.
“Mathalani, mtandao wa barabara nchini ni kilomita 86,472 ambapo ni asilimia 9.7 tu ndiyo za kiwango cha lami. Aidha, mahitaji ya umeme kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani bado ni makubwa ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji. Mitambo iliyopo kwa sasa ina uwezo wa kuzalisha Megawati 1,424.6 ikilinganishwa na mahitaji ya zaidi ya Megawati 3,000 ili kuweza kuhimili mahitaji ya uchumi wa viwanda,” amesema.
Pia amesema wigo mdogo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo uwiano wa mapato ya ndani na Pato la Taifa ni takriban asilimia 15.0 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 17.0 kwa nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Fursa zilizopo
Serikali imeeleza fursa zilizopo katika taifa ambazo ni nguvukazi kubwa ya Taifa ambao ni vijana; rasilimali na kilimo (mazao, mifugo, na uvuvi); madini; gesi; vivutio vya utalii; viwanda vya huduma za kilimo (agri-business); vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa umeme; biashara na huduma za usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.
Malengo ya nchi
Lengo kuu la Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ni kuondoa umaskini nchini. “Bajeti hii vile vile imeandaliwa kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21) na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020. Malengo makuu ni kuondokana na umaskini na kuibadilisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda na kuingia kwenye kundi la nchi zenye kipato cha kati (Middle Income Countries) ifikapo mwaka 2025.
“Mheshimiwa Spika, changamoto, fursa mafanikio na malengo niliyoyaeleza sasa hivi lazima yaende pamoja na wajibu upande wa Serikali, sekta binafsi, wadau wengine na mwananchi mmoja mmoja, wa kuzipatia majibu changamoto hizo na kuchangia ipasavyo katika jitihada za kulipeleka Taifa letu mbele.
“Tutafanya hivyo ikiwa kila mwananchi atafanya kazi na kutumia uwezo wake wote kwa ajili ya maendeleo yake na ya Taifa. Aidha, ni muhimu pia tuendelee kujenga na kutumia ubia wa kimkakati (harness strategic partnerships). Ujumbe wangu kwa Watanzania kupitia bajeti hii ni kuwa, lazima tuendelee kufanya chaguo gumu (tough choices) katika kuelekeza rasilimali kidogo tunazokusanya ili tuweze kuzishinda changamoto hizo zilizoko mbele yetu.
“Ukweli ni kuwa, mabadiliko ni magumu na mara nyingi yanapingwa! Hivyo, lazima tuwe imara, tukusudie kufanikiwa na tutumie vizuri fursa na uwezo wa Watanzania, sekta binafsi na Serikali ili kufikia azma yetu,” amesema Dk. Mpango.
Mazingira bora ya kujenga viwanda
Kama sehemu ya kuboresha mazingira ya uwekezaji katika viwanda, Serikali imetangaza msahama wa kodi kwa walipakodi waliokuwa wanadaiwa siku za nyuma kwa asilimia 100 ndani ya miezi sita ijayo kwa watakaojitokeza kulipa kodi kuanzia Julai 1, hadi Desemba, 2018.
Mara nyingi wawekezaji wamekuwa wakilia na mazingira ya biashara nchini kutotabirika, lakini sasa katika bidhaa za mafuta Serikali haikuongeza kodi, hivyo kuwa na gharama za uwekezaji zinazotabilika kwa mwaka mzima wa fedha ujao.
Pia Serikali haikuongeza ushuru wa barabara, kodi mbalimbali katika mafuta, na katika kulinda viwanda vya ndani imeongeza asilimia 5 ya ushuru wa forodha kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje. Hii ina maana kuwa mtu anayetaka kufungua kiwanda Tanzania atapata faida zaidi kuliko kuagiza bidhaa nje ya nchi.
Kupitia bajeti hii, Serikali imechukua hatua za kulinda viwanda vya ndani kwa mfano katika eneo la mafuta: “Kutoza Ushuru wa Forodha wa asilimia 25 badala ya asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ghafi ya kula ya mawese (Crude Palm Oil) yanayotambulika katika HS Code 1511.10.00 kwa mwaka mmoja,” amesema Dk. Mpango. Aina zote za mafuta zimewekewa ushuru. Soma bajeti ndani ya gazeti hili kuanzia ukurasa wa 9.
Mara kadhaa Rais John Magufuli amewataka Watanzania kuwekeza katika viwanda vya dawa na vifaa tiba, na zamu hii kupitia bajeti yake amethibitisha nia hiyo. “Kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato ili kupunguza kiwango cha Kodi ya Mapato ya Makampuni (Corporate Income Tax) kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 20 kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2018/19 hadi mwaka 2022/23 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya madawa ya binadamu na viwanda vinavyotengeneza bidhaa za ngozi.
“ Aidha, Serikali itaingia mkataba wa makubaliano (performance agreement) na kila mwekezaji ambao utaainisha wajibu wa kila upande. Lengo la hatua hii ni kuongeza uwekezaji katika sekta ya madawa ya binadamu na usindikaji wa ngozi ambao kwa sasa haufanyiki nchini na pia kuongeza ajira na mapato ya Serikali.
“ Aidha, hatua hii itapunguza matumizi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza dawa hizo kutoka nje na kuhamasisha uzalishaji wa madawa mengi zaidi hapa nchini,” amesema Dk. Mpango.
Katika kuhakikisha kuna umeme wa uhakika kufanikisha uwekezaji katika viwanda, Serikali imeamua kwa vitendo kutenga Sh bilioni 700 kujenga mradi wa Stiegler’s Gorge katika Bonde la Mto Rufiji ambao utazalisha megawati 2100 na hivyo kuziba pengo la upungufu wa umeme kwa mara moja.
Mbowe ataka gesi badala ya umeme wa maji
Kingozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema hakubaliani na uamuzi wa Serikali kuchepuka kutoka katika mpango wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi, ambao tayari bomba limejengwa na kujikita katika ujenzi wa mradi wa umeme wa maji wa Stiegler’s Gorge.
“Nchi imekopa dola bilioni 1.2 kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam. Tumezikopa kutoka Exim Bank China. Gesi inaweza kuzalisha megawati 10,000 pale Kinyerezi. Kwa sasa tunatumia asilimia 6 tu ya gesi inayopita katika bomba hili. Bomba la gesi tukitumia asilimia 25 tu, tunapata megawati 2,500. Sikubaliani na kutumia Sh bilioni 700 katika ujenzi wa Stiegler’s Gorge, bora fedha hizi tungeziwekeza katika elimu au kilimo,” amesema Mbowe.
Mbowe amesema nchi inaingia gharama kubwa kutibu magonjwa ambayo yangezuiwa kwa kuwapatia Watanzania maji, hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani wakati wa mjadala wa bajeti ndani ya wiki hii, itahakikisha suala la maji linapewa kipaumbele.
“Asilimia 35 ya magonjwa nchini yanahusiana na maji. Tuna uwezo wa kuzuia asilimia 35 ya malazi ya wananchi kwa kuwapa maji safi na salama… huko ndiko tunapaswa kuelekeza fedha na si kwingine,” amesema.
Mbowe amesema wapinzani wameomba kupewa mkakati wa uchumi wa viwanda kutoka serikalini, lakini hadi sasa hawajapewa mkakati huo. “Hoja ya kujenga uchumi wa viwanda ni hoja ya kibiashara, ni hoja inayopaswa kutekelezwa na sekta binafsi. Katika siku za karibuni yamekuwapo mazingira ya kukwamisha uwekezaji.
“Sisi tunasema fedha zinazotolewa katika elimu hazitoshi. Kwa sasa mwanafunzi anatengewa Sh 500 kwa siku tunasema kiasi hiki ni kidogo mno, hakitoshi. Elimu ndiyo msingi. Hakuna shortcut iwe kwa Chadema, CCM au yeyote, hatuwezi kurusha ndege kama hatujawekeza katika elimu… Ukiona elimu ni gharama, basi jaribu ujinga,” amesema Mbowe.
Tofauti na miaka ya nyuma ambapo hotuba za wapinzani zilitawaliwa na hoja za kisiasa, mwaka huu upinzani imehimiza uwekezaji, ukuzaji biashara, elimu na hasa uwekezaji katika kilimo na mnyororo wa thamani. Mbowe amesisitiza: “Vipaumbele vyetu ni elimu, kilimo, viwanda katika mnyororo wa thamani ya kilimo, huduma za afya, maji na uchumi.”
“Nchi zote zilizoendelea zimepitia kwenye agrarian revolution (mapinduzi ya kilimo, ufugaji na uvuvi). Mnyororo wa thamani wa kilimo (agricultural value chain). Watu wako wakiishapata kipato viwanda vya vigae, soda, bia, viberiti vitakutaja kutokana na mahitaji,” amesema.
Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani, amesema hapingi mpango wa ujenzi wa Reli ya Standard Gauge. “Hatuna tatizo nayo, ila namna mpango mzima unavyopelekwa unaacha maswali mengi sana ambayo hayana majibu. Rais amesema tutajenga kwa fedha zetu za ndani. Serikali bungeni inasema itakopa, hatujaandaa human resource, treni na mabehewa…
“Kenya wamejenga kutoka Mombasa hadi Kisumu kwa miaka miwili imeisha. Walijiandaa wakajua watajenga reli, wakaandaa watu wao, kina nani watasupply mabehewa, wakafundishwa jinsi ya kuendesha huduma za reli. Reli imeisha, mabehewa na watu wapo. Hapa kwetu tunaeleza nguvu katika ujenzi wa njia. Hatujaandaa watu wetu. Tutamaliza kujenga reli, hatuna vichwa vya treni, tukipata mabehewa tunajua ahaa, hatuna mainjinia…,” amesema.
Kuhusu kufufua Shirika la Ndege Tanzania, amesema inafurahisha nchi kuwa na ndege ila akahoji iwapo zinamnufaisha mwananchi wa kawaida. Serikali imenunua ndege mpya 3 tayari, ndege nyingine 3 zinatengenezwa, huku kupitia bajeti ya mwaka huu ikitangaza kuwa imetoa malipo ya awali kwa ndege ya pili kubwa aina ya Dreamliner Boeing 787-8.
Majibu ya Dk. Abbas
January 3, 2018 Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Reli (RAHCO) imetangaza mchakato wa awali wa zabuni ya ununuzi wa vichwa na mabehewa kwa ajili ya treni ya umeme itakayotumika katika reli ya kisasa (Standard Gauge) ambayo ujenzi wake unaendelea, amesema Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas.
Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa RAHCO, ambaye sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Masanja Kadogosa ameithibitishia Idara ya Habari (MAELEZO) kuanza kwa mchakato huo ambao unafuata taratibu za kimataifa za ununuzi kwa njia ya ushindani.
Kwa mujibu wa tangazo la zabuni, jumla ya vichwa 14 vya treni ya umeme kwa ajili ya kusafirisha mizigo na vichwa viwili vya treni ya mizigo inayotumia mafuta vinahitajika.
RAHCO pia imetoa zabuni ya ununuzi wa vichwa vitano vya treni ya abiria ya kisasa inayotumia umeme (Electric Multiple Units) ambapo kila kimoja kitakuwa na uwezo wa kuvuta mabehewa 60 yenye kuchukua abiria 1,800.
Katika mabehewa hayo ya abiria, mabehewa 15 yatakuwa ni ya kiwango cha daraja la kwanza na mengine 45 ni daraja la pili.
Mbali na mabehewa ya abiria, zabuni hiyo inajumuisha ununuzi wa mabehewa mengine zaidi ya 1,500 yenye muundo tofauti kwa ajili ya kubebea aina mbalimbali za mizigo.
Pamoja na sifa mbalimbali zilizoainishwa katika tangazo la zabuni, moja ya sifa za reli hiyo ya kisasa ni kuhimili treni ya abiria yenye uwezo wa mwendo kasi wa kilometa 160 kwa saa na mabaehewa yenye jumla ya urefu wa mita 2,000, wakati ile ya mizigo yenye uwezo wa kwenda kasi ya kilometa 120 kwa saa.
Kwa mujibu wa tangazo la zabuni, mwisho wa kuwasilisha nyaraka za zabuni iikuwa Januari 30, mwaka huu. Tayari awamu ya kwanza na ya pili ya ujenzi wa reli hii kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na Morogoro mpaka Makutopora Dodoma umeanza.
Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Habari – Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Abbasi amesema; “Sisi kama serikali hatutaki kusubiri kwamba reli imekamilika tunaanza kuhangaika treni ziko wapi mabehewa yako wapi ya kisasa na mkumbuke kuwa hii reli itakuwa yenye uwezo wa namna mbili kwanza zitapita treni za umeme, lakini kuna treni mpya za kisasa za aina ya diesel.
“Serikali tumeanza wa kununua treni kwa maana ya treni ni mabehewa kwa maana ya vichwa vya treni ya kisasa na tukumbuke kenye ujenzi wa hii reli kutakuwa kuna jengwa na line za umeme kabisa kwasababu ni reli itakayo ruhusu mwendo wa kasi.
“Tumeagiza mabehewa kwenye huu ununuzi tunanuanua jumla ya mabehewa 1,590 mabehewa ya kisasa na yatakuwa ya aina tofauti tofauti nataka kutolea mfano kuna haya mabehewa yaitwayo Double stack containers haya yanaweza kubeba container la juu na la chini na yakatembea na likafika linakopaswa kufika. Haya ya double tumeagiza mabehewa 50.”
Zitto ataka kodi ya maji
Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema katika bajeti yote ya maendeleo ya mwaka 2018/19, serikali imetenga Sh bilioni 698 tu kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya maji. “Hii ni sawa na asilimia 5.8% ya bajeti yote ya Maendeleo inayopendekezwa. Katika hatua za kikodi zinazopendekezwa hakuna hatua yeyote inayoonyesha kuwa maji ni kipaumbele.
“Hata bidhaa za maji zinazoagizwa kutoka nje hazijaondolewa kodi au viwanda vya kuzalisha bidhaa za miradi ya maji havijapewa vivutio,” amesema.
Ameshauri kuongeza bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa azma ya “kumtua mama ndoo kichwani” na kuongeza uzalishaji wa chakula nchini. “Tunashauri ongezeko la shilingi 160 ushuru wa bidhaa mafuta ya petroli na dizeli. Ongezeko hili litaongeza zaidi ya shilingi bilioni 500 kwenye bajeti ya wizara hiyo.
“Mgawanyo wa nyongeza hii ya shilingi 160 ni kama ifutavyo; kila shilingi 100 itakayokusanywa ipelekwe kwenye mfuko wa maji ili kuongeza upelekaji na usambazaji wa maji kwa wananchi, hasa vijijini. Kwa hatua hii, jumla ya shilingi bilioni 316 zitaongezeka kwenye bajeti ya sasa ya mfuko wa maji, na kufanya bajeti yote ya maji kuwa shilingi 1.014 trilioni.
“Pili shilingi bilioni 190 zitakazokusanywa kutoka kwenye kila shilingi 60 kwa lita zipelekwe Tume ya Umwagiliaji ya Taifa ili kuongeza uwezo wa kuendesha miradi yake. Kwa sasa Tume ya Umwagiliaji ya Taifa imetengewa shilingi bilioni 29 tu. Mabadiliko haya ya kodi katika mafuta ya petroli na dizeli hayatachangia kuleta mfumuko wa bei kwa sababu kuu mbili zifuatazo:
“1. Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia juu ya mwenendo wa bei ya mafuta duniani, inaonekana bei zitaendelea kushuka ndani ya miaka miwili ijayo. 2. Kwa kuiwezesha Tume ya Umwagiliaji kufanya miradi mingi ya kilimo cha umwagiliaji, itakayozalisha chakula cha kutosha, na hivyo tutaweza kuondoa hofu ya kutokea mfumuko wa bei ya chakula nchini kwa kuwa vyakula huchangia kwa 48% katika kupanda kwa mfumuko wa bei,” amesema Zitto. Pia ametaka kilimo kikuzwe kwa kiwango cha asilimia 8 kila mwaka kuwezesha wananchi kuondoka katika umasikini uliokithiri.
Wabunge wataka asilimia 2 ya mawasiliano
Kwa upande wao, wabunge wa CCM waliozungumza na JAMHURI, wameomba suala la maji lipewe kipaumbele kwa kuongeza asilimia 2 ya gharama ya muamala katika kupiga simu na kutuma fedha kupitia simu za mkononi.
“Kujenga nchi ni kazi. Hapa tulipo Rais Mgufuli ametufungulia njia ya fikra. Tuitumie fursa hii. Sisi tutazungumza ndani ya chama. Nafahamu Rais hakutaka kuongeza kodi kwa nia ya kutoumiza wapigakura, ila kuna eneo la maji haliepukiki. Yapo mawazo ya kuongeza Sh 50 kwenye mafuta, lakini pia mimi nadhani kama mafuta ni ngumu, basi tuongeze Sh 100 kwenye kila muamala wa simu unaofanywa, iwe umetuma pesa au umepiga simu. Fedha hizi zipelekwe kwanye maji,” amesema mmoja wa wabunge wa CCM.
“Kwa kweli kama tunataka kumaliza tatizo la maji nchini tufanye kama ilivyofanyika katika suala la umeme vijijini-REA. Imetengwa Sh 50 kwenye mafuta, lakini mimi nadhani sasa tuweke asilimia 2 katika kila muamala unaofanywa kwenye simu iwe ni kutuma fedha au kupiga simu.
“Hapa simaanishi asilimia 2 ya muamala uliotumwa, bali asilimia 2 ya tozo ya gharama za kupiga au kutuma fedha, yaani ile gharama ya muamala. Hii itamfanya karibu kila Mtanzania kushiriki kujenga uchumi imara wa taifa letu na kila mwananchi kupata maji. Wachina walijichangisha kutujengea reli ya Tazara. Tukimaliza umeme na maji, asilimia hii tuipeleke kwenye elimu mbele ya safari,” amesema mbunge mwingine wa CCM.
Kimsingi JAMHURI limezungumza na wadau wengi wa uchumi, ambao wamepongeza moyo wa ushirikiano kati ya upinzani na serikali kuondoa umasikini kwa wananchi wanaodhani ukidumishwa uchumi wa Tanzania utakua kwa kasi kubwa kuelekea kwenye viwanda. Soma bajeti yote kuanzia ukurasa wa 9.