Wananchi wa Halmashauri ya Manispaa Songea, Mkoa wa Ruvuma wamo hatarini kupata ugumba na saratani kutokana na kutumia maji yenye kinyesi cha binadamu kwa miaka 16 baada ya kuchimba visima karibu na vyoo, JAMHURI limebaini.
Uchunguzi wa gazeti hili uliohusisha, pamoja na mambo mengine, kuwahoji wananchi 123 wa kata mbili, Ruvuma, yenye wakazi 15,706 ambako Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA) imefikisha huduma ya maji kwa watu 3,650 sawa na asilimia 23 na wanayatumia, na Kata ya Lizaboni yenye wakazi 23,500, wanaopata huduma ya maji ni 17,188 sawa na asilimia 73, wananchi wake bado wanakunywa, kupikia, kuoga na kudekia maji yenye kinyesi cha binadamu, tindikali na nitrate kwa miaka 16 tangu mwaka 2003.
Baadhi ya waliohojiwa na gazeti hili, Jean Chipa na Mgeni Ramadhani, wakazi wa Kata ya Ruvuma, wamesema wanayatumia maji hayo ya visima kwa sababu hawana mbadala, ingawa wanapata tatizo la kuugua mara kwa mara pamoja na watoto wao ugonjwa wa typhoid, na kuhara bila kujua hatima yake.
Mmiliki wa duka la dawa muhimu za binadamu Mtaa wa Ruvuma Chini, Loisi Namtapika, anasema kero ya maji safi Kata ya Ruvuma ni kubwa, kwani visima zaidi ya 20 anavyovifahamu vipo jirani na vyoo, choo kikiwa juu na kisima chini.
Namtapika anaeleza kwamba hali za wananchi katika eneo analoishi si salama kiafya, ukizingatia kuwa wananchi hawana utamaduni wa kuchemsha maji na watoto chini ya umri wa miaka mitano wanaathirika sana na kwamba, kwa siku amekuwa akipokea wagonjwa watano wa typhoid, kuhara na magonjwa yanayohusiana na vyakula.
Shani Marijani, mwenye umri wa miaka mitano akiwa na mama yake dukani hapo, anasema kwa huruma: “Naumwa tumbo, naharisha,” huku akitokwa machozi wakati mama yake mzazi, Arafa Hamisi, akieleza kuwa magonjwa hayo yamekuwa ya kawaida kwao na yanawarudisha nyuma kiuchumi, kwani gharama ya kutibiwa ni kati ya shilingi 13,000 hadi 18,000, na kwa hali hiyo, anatafakri akisema: “Utakuta ndani ya nyumba mnaugua watatu mara kwa mara.”
Diwani wa Kata ya Ruvuma, Msosa Msosa, amethibitisha kuwa hali ya wananchi wake si nzuri kutokana na kuugua mara kwa mara magonjwa hayo na anaamini kwa Manispaa ya Songea, kata yake inaweza kuongoza kwa magonjwa hayo kutokana na uwepo wa visima 186 vilivyochimbwa jirani kabisa na vyoo kwa sababu ya kukosa mtandao wa maji safi kutoka SOUWASA.
Kevin Njozi, mkazi wa Mtaa wa Madizini, Kata ya Lizaboni, ambako mtandao wa maji safi upo kwa asilimia 73 anasema wanaendelea kutumia maji ya visima kwa sababu ya gharama kubwa ya bili (ankara) kwa mwezi na kuingiza maji ndani ya nyumba, kwani mwaka 2015 ilimgharimu shilingi 500,000 kuingiza maji ikiwa ni pamoja na kuchimba mtaro wa urefu wa mita 86 kwa shilingi 86,000, kununua mabomba mita 86 kwa shilingi 172,000, alilipia mita shilingi 60,000, kununua bomba la kukalia mita ‘offset’ shilingi 25,000, gharama ambazo mwananchi wa kawaida hawezi kuzimudu.
Felistas Mapunda, anasema mara ya mwisho kutumia maji ya SOUWASA ni Februari mwaka jana alipokatiwa kutokana na bili kuwa kubwa ya shilingi 32,000 wakati alikuwa anatumia maji machache kwa ajili ya kunywa na kupikia tu, ingawa alikiri yalimsababishia kuugua mara kwa mara tumbo na kuhara, lakini alisema hana namna.
Rosemary Mbilo (13), mkazi wa Madizini na mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Madizini, anasema wanatumia maji ya visima kwa kuwa kwao hawajaingiza maji ya SOUWASA na mara nyingi anasumbuliwa na ugonjwa wa tumbo na kuhara na hajui sababu ni nini.
Kaimu Meneja Maabara ya Ubora wa Maji Mkoa wa Ruvuma, Mkemia Philemon Kinyangadzi, anasema upimaji wa maji hayo waliufanya Agosti, 2018 kwa maombi ya SOUWASA kuchunguza kuchafuliwa maji visima 44, lakini matokeo yake kwa mujibu wa sheria yao hawaruhusiwi kuyatoa wao bali wateja ndio wenye mamlaka hayo.
Lakini alisema wananchi wakiyatumia maji yaliyochafuliwa na bakteria hao kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu, wanaweza kupata magonjwa hayo, ikiwemo saratani, ugonjwa wa ‘methemoglobinemia’ ambao unatokana na kuyatumia maji yaliyochafuliwa kwa ‘nitrate’, ambapo mzunguko wake unachafua damu na kuharibu mfumo wa vilinda mwili (antibodies na antigens), unaoweza kusababisha vifo kwa wanaoishi na virusi vya ukimwi au kuibuka ugonjwa wa ‘Blue Baby Syndrome’, yaani watoto kuzaliwa wakiwa na rangi ya bluu.
Alisema endapo maji yatachafuliwa na bakteria wajulikanao E.Coli na Fecal Coliform ambao wanapatikana kwenye kinyesi cha binadamu na kipimo chake ambacho ni ‘uniti’ ikaonekana wapo zaidi ya uniti moja, tindikali inayopimwa na kipimo kiitwacho PH ikawa chini ya tano, kwani inayotakiwa iwe 6.5 hadi 8.5 na nitrate kipimo chake kiwe miligramu kwa lita, inatakiwa iwe chini ya 45, lakini ikiwa juu ya 45, hiyo ni hatari sana kwa afya ya binadamu.
Mkemia Kinyangadzi amesema ingekuwa amri yao visima vingefukiwa lakini hawana mamlaka hayo bali jukumu la kisheria lipo kwa Mamlaka za Bonde na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kupitia idara yake ya afya.
Afisa Maji ofisi ndogo ya Ruvuma na Pwani ya Kusini, Malindisa Elias, amesema hawana mamlaka ya kufukia visima hivyo kwa kuwa jukumu hilo ni la Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na wao, SOUWASA na Maabara ya Ubora wa Maji Mkoa wa Ruvuma.
Malindisa amesema SOUWASA hawawezi kufukia visima hivyo kwa sababu na wao ni wateja kama wale waliowapatia vibali vya kuchimba na kutumia maji ya visima vyao kwa mujibu wa sheria namba 11 ya mwaka 2009 na SOUWASA kibali chao ni kusafirisha na kusambaza maji yenye viwango kwa mujibu wa sheria namba 12 ya mwaka 2009.
Malindisa ameeleza kuwa mamlaka yao inavitambua visima 61 na kati ya hivyo imetoa vibali kwa wateja wake 11, lakini 50 bado hawajafika ofisini kwao na kwamba kwa mwaka mteja anatakiwa kulipa shilingi 100,000 kwa matumizi ya nyumbani na wale wa hoteli, nyumba za kulala wageni, maeneo ya starehe shilingi 250,000 na taasisi shilingi 300,000 na kwamba umbali wa kisima hadi kisima lazima uwe mita 130, kwa sababu chini kuna mikondo ambayo inapeleka maji mtoni, hivyo kwa umbali huo wale bakteria wanaochafua maji hawawezi kutembea na kuongezeka, lazima wafe.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea, Tina Sekambo, amehoji akisema SOUWASA wasikwepe majukumu, kama uchunguzi umefanyika na matokeo yanaeleweka, kwa nini wasichukue hatua?
“Kama kuna sheria mbili zinakinzana kuhusu usimamizi wa rasilimali maji, itumike sheria inayotetea afya za wananchi kwa kuvifukia visima hivyo ambavyo vipo kwenye mtandao wa maji safi,” amesema Mkurugenzi Sekambo.
Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Songea, Mameritha Basike, amesema kuchafuliwa kwa maji ni hatari kwa afya ya binadamu, kwa sababu husababisha magonjwa ya typhoid, saratani, matumbo, kuwashwa mwili, ukurutu na kipindupindu, hivyo alishauri uamuzi wa kuvifukia visima hivyo ndiyo muafaka.
Daktari Basike amesema wagonjwa wanaougua typhoid, kuhara na magonjwa ya njia ya chakula ni zaidi ya 2,610 kwani mwaka 2016 walikuwa 1,265, mwaka 2017 walikuwa 916 na mwaka 2018 walikuwa 429. Pia ugonjwa wa ‘Blue Baby Syndrome’, yaani watoto wanaozaliwa wakiwa na rangi ya bluu unatokea katika Kituo cha Afya cha Manispaa ya Songea, kwani mwaka 2017 walizaliwa watoto sita na mara nyingi hufariki dunia.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Ruvuma (HOMSO), Magafu Majura, amesema endapo ugonjwa wa typhoid utajirudia kwa wananchi wa Manispaa ya Songea kutokana na kutumia maji hayo, kuna uwezekano wa kupata tatizo la ugumba, kwa kuwa bakteria wajulikanao kwa jina la ‘salmonella typhe’ wamekuwa na kawaida ya kutoboa utumbo, hivyo ni rahisi kuathiri mirija ya uzazi kwa wanaume na wanawake, kwa mfano, kuziba kwa mirija inayopitisha mayai kwa mwanamke (oviduct).
Meneja Ufundi wa SOUWASA, Mhandisi John Kapinga, amekanusha kuhusu kutoza ‘bili’ kubwa sambamba na gharama kubwa ya kuingiza maji kwenye nyumba, akisisitiza kuwa kilichopo ni uzembe wa baadhi ya wananchi, kwa kuwa ‘uniti’ moja ya maji kwa matumizi ya nyumbani haizidi shilingi 1,100 sawa na uchotaji wa maji ndoo za lita ishirini 50 na gharama hizo zinalingana na mamlaka za maji katika miji mingine kama Iringa ‘uniti’ moja shilingi 1,685, Njombe shilingi 950 na Mbeya shilingi 1,000, akahoji: “Wananchi wanalinganisha na wapi?”
“Cha kushangaza utakuta baadhi ya wananchi wananunua maji ya dukani lita moja kwa shilingi 1,000 kila siku na kwa mwezi anatumia shilingi 30,000, hasemi ni gharama kubwa, lakini akipelekewa bili ya maji shilingi 11,000 kwa kutumia maji ‘uniti’ 10 sawa na ndoo 500 kwa mwezi anasema gharama za maji zipo juu, kwa nini tusiseme uzembe?” amesema Mhandisi Kapinga.
Amefafanua kuwa gharama za kuingiza maji nyumbani hutegemea umbali kutoka kwa mteja na lilipopita bomba la kusafirisha maji ya SOUWASA na kwamba gharama zao ni shilingi 250,000, na mita wakati wa kuingiza maji kuanzia mwaka 2013 zimekuwa zikitolewa na SOUWASA, si mteja na kwamba gharama hizo zipo kisheria.
Amesema sheria hizo zipo kama ilivyo kwa sheria zinazosimamia rasilimali maji namba 11 ya mwaka 2009 inayotoa mamlaka kwa mwananchi kuchimba kisima chenye urefu kuanzia mita sifuri hadi 15 bila kibali na kama kitatolewa basi mamlaka za mabonde watahusika, wakati SOUWASA inapewa kibali na mamlaka hiyo kutekeleza sheria namba 12 ya mwaka 2009, ambayo inasimamia usafirishaji maji yenye viwango vinavyokubalika kwa matumizi ya binadamu.
Ameeleza kwamba, sheria hizo haziwapi nguvu kisheria ili kuvifukia au kuvifunga visima vya maji visivyofaa kwa matumizi ya binadamu, kwa kuwa SOUWASA ni wateja wa mamlaka za mabonde waliopewa dhamana ya kusimamia rasilimali maji hapa nchini kwa sheria yao namba 11 ya mwaka 2009.
Mhandisi Kapinga ameeleza ripoti ya maabara ya ubora wa maji Ruvuma ya mwaka 2018 baada ya kuvifanyia uchunguzi visima kwenye nyumba 34 za kulala wageni mjini Songea ilibaini wateja wanaoga maji yaliyochafuliwa, jambo ambalo linaweza kuwasababishia ugonjwa wa ngozi ukiwemo ukurutu.
Amesema uchunguzi huo kwenye visima 44 kati ya 314 vilivyopo kwenye eneo lililopitishwa mtandao wa maji safi, visima 10 vilikuwa salama na 34 maji hayafai kwa matumizi ya binadamu, kwani uchafu uliokutwa unasababisha ugonjwa wa typhoid, kuhara, madhara ya kuharibu mifumo ya mwili ikiwemo vimeng’enyo vya chakula tumboni kupata shida inayojulikana kitaalamu kama ‘gastric problems’ kutokana na maji hayo kuwa na kinyesi cha binadamu, tindikali iliyokuwa chini ya 5 na nitrate juu ya 45.
Eusebius Wella, mmoja wa wamiliki wa nyumba za kulala wageni mjini Songea amesema wateja walipokuwa wengi alitumia maji ya kisima kwa lengo la kupunguza gharama za maji lakini kwa sasa hayatumii.
Mkurugenzi wa SOUWASA, Mhandisi Patrick Kibasa, amebainisha kwamba wanajitahidi kusambaza maji lakini tatizo baadhi ya watu hawayatumii, kwa mfano, amesema Mtaa wa Madizini, Kata ya Lizaboni mwaka 2018 ulipelekwa mradi wa maji wa shilingi milioni 400 lakini bado wananchi wanatumia visima vyao 235, wakati waliounganishiwa maji ni 667, waliohai ni 595 na waliokatiwa ni 72, jambo ambalo linapunguza mapato kwa mwezi.
Amesema hadi Januari 2019 wateja katika manispaa walikuwa 15,406 kati ya wakazi 197,961 na wanaopata huduma ya maji ya SOUWASA ni 175,992 sawa na asilimia 85, lakini mapato kwa mwezi wastani ni shilingi milioni 260, wakati gharama za uendeshaji, matengenezo na uwekezaji mdogo wastani ni shilingi milioni 364, jambo linalosababisha kukosa uwezo kifedha ili kufikisha maji maeneo mengine kwa wakati lakini, hata hivyo, amesema wanaishukuru wizara husika kwa jitihada za uwekezaji, ambapo Manispaa ya Songea ni miongoni mwa miji 28 Tanzania inayotegemea kufanyiwa uwekezaji mkubwa kutokana na fedha za mkopo kutoka nchini India.
Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololeti Mgema, amesema ipo sababu ya kuvifukia visima hivyo katika maeneo yale ambayo yamefikiwa na mtandao wa maji safi na salama lakini SOUWASA wanapaswa kuharakisha kufikisha maji katika maeneo mengine ambayo wananchi wanahatarisha usalama wa afya zao kwa kunywa maji machafu.
Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Dk. Damas Ndumbaro, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, amesema matokeo ya uchunguzi huo lazima yafanyiwe kazi kwa kuvifukia visima hivyo haraka lakini pia kwa jitihada zake ameweza kufanikisha kupata mkopo wa mradi wa maji wa dola za Marekani milioni 50.889 sawa na shilingi bilioni 117.044 kutoka Serikali ya India, mradi ambao utatosheleza upatikanaji wa maji katika Manispaa ya Songea hadi mwaka 2034.
Amesema mradi huo utatoa kipaumbele cha kwanza Kata ya Ruvuma ili kuweza kuondoa kero yao ya kunywa maji kutoka katika visima vilivyochimbwa karibu na vyoo, ambayo yamechafuliwa kutokana na mwingiliano na kinyesi cha binadamu na uchafu mwingine (Fecal contamination).
Mwaka 2003 ulifanyika uchunguzi wa uchafuzi wa maji katika Manispaa ya Songea na shirika la kupima ubora wa maji la Ujerumani (DORSH CONSULT) kwa hisani ya Benki ya Maendeleo Ujerumani ‘Kreditanstalt Fur Wiederaufbau’ (KfW) na kurudiwa mwaka 2018 na Maabara ya Ubora wa Maji Mkoa wa Ruvuma na kubainika maji yalichafuliwa na hayafai kwa matumizi ya binadamu kutokana na visima kuchimbwa katikati ya makazi ya watu karibu na vyoo, mashimo ya kutupa taka na makaro ya kuhifadhi maji machafu.