Maji ni anasa katika Jiji la Mwanza, hivyo ndivyo mtu anavyoweza kuelezea kulingana na ongezeko la bei ya maji katika Jiji la Mwanza.
Ongezeko la bei ya maji kwa ndoo moja ya lita 20 imepanda kutoka Sh 14 hadi kufikia Sh 24.50. Yaani imeongezeka Sh 10.50 kwa kila ndoo. Wachambuzi wa mambo wanatafsiri kuwa, hili ni ongezeko la zaidi ya asilimia 70 kwa mwananchi.
Baadhi ya wananchi jijini Mwanza wanaonyesha wasiwasi wao wa kushindwa kumudu gharama hizo. Wanadhani watalazimika kurejea katika matumizi yamaji yasiyokuwa safi na salama.
Ongezeko la bei ya maji lina baraka za serikali kupitia Wizara ya Maji, lakini uchunguzi umebaini pamoja na kupandisha gharama hizo baadhi ya maeneo ya jiji hilo hayapati huduma ya maji.
Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la JAMHURI umethibitishwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA), maeneo ya Buhongwa, Bujora, Kiseke, Kisesa Nyasaka Islamic, Nyasaka Riverside, Nyamhongolo, Buswelu, Ibanda, Kishiri, Ihila, Mwashi, Shadi na Nyegezi Kalifonia. Kwingineko ni Bugarika, Nyankurunduma, Mahina, Tambuka Reli pamoja na eneo la Mbugani jijini Mwanza.
“Watu vyuma vimekaza. Wanapunguzwa kazi, hakuna ongezeko la mishahara, lakini wao maji wanaongeza bei…wanataka tuishije?” Emmanuel Jackson amehoji.
JAMHURI imebaini kuwa ongezeko hilo la bei ya maji iliyoanza rasmi Julai Mosi, mwaka huu, limechapishwa kwenye Gazaeti la Serikali kwa notisi namba 486/2019 kwa lugha ya Kiingereza na GN Namba 490/2019, la lugha ya Kiswahili.
Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa, George Mhina, amesema ongezeko hilo la bei ni halali.
Neno la Bakwata
Kulingana na kizungumkuti hicho cha gharama ya maji, Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mwanza limeiomba serikali kupunguza bei ya maji misikitini.
Kuanzia Julai Mosi mwaka huu, bei ya maji imepanda kutoka Sh 925 kwa uniti 1, hadi 10 na kufikia Sh 1,620. Bakwata imesema ikiwa serikali imeweza kufuta kodi za ardhi kwenye taasisi za dini, haiwezi kushindwa kuwasaidia kwenye eneo hilo la maji.
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke, ametoa ujumbe huo wakati wa swala ya Idd el Haj, iliyoswaliwa Uwanja wa Nyamagana jijiniMwanza hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Sheikh Kabeke, asilimia 100 ya Waislamu wanaokwenda kuswali misikitini wanategemea maji katika kufanya ibada zao.
Kiongozi huyo wa kiroho amenukuriwa akisema kwamba kupanda kwa ankara za maji ni kikwazo kwa Waislamu kufanya ibada.
“Hakuna dawa zaidi ya maji,” Sheikh Kabeke amekaririwa akipeleka ujumbe serikalini akiomba gharama hizo mpya za bei ya maji zifutiliwe mbali na serikali kwa masilahi ya umma.
Amesema serikali inaweza kuondoa tozo hiyo mpya kama ilivyofanya kwa dawa ya kufubaza virusi vya ukimwi (ARVs).
“Bei imependa sana, kuna baadhi ya misikiti ilikuwa inalipa Sh 100,000 kwa mwezi. Ila tangu ankara zimepanda, imeletewa bili ya Sh 300,000 hadi Sh 600,000.
Akizugumza jijini Mwanza wiki iliyopita, Katibu wa Chadema Wilaya ya Nyamagana, Athanas Michael, amesema chama chake kinalaani ongezeko hilo la bei ya maji.
“Tunatoa siku 13 kuanzia leo (Agosti 20). Ikifika Septemba
2, mwaka huu, gharama ya maji haijashuka, tutaitisha maandamano. Sisi Chadema tupo kwa ajili ya kutetea wananchi,” amesema Michael.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mwauwasa, Mhandisi Anthony Sanga, amekiri kupanda kwa gharama za maji katika Jiji la Mwanza na viunga vyake.
Amesema ongezeko hilo la bei lilifuata taratibu mbalimbali zinazokubalika kisheria, kwa kuwahusisha wadau wa sekta hiyo ya maji.
Mhandisi Sanga amesema kabla ya MWAUWASA kuwasilisha EWURA mapendekezo ya kufanya mabadiliko ya bei ya maji, ilipewa kibali na Wizara ya Maji.
“Baada ya kupewa kibali na Wizara ya Maji, Januari 15, 2019, iliitisha kikao cha Wenyeviti wa Serikali za Mitaa jijini Mwanza, Baraza la Watumiaji Huduma za Maji (EWURA CCC) na makundi mbalimbali ya wateja.
“Wadau hawa walielezwa bayana, umuhimu na uhalisia wa kufanya mabadiliko ya bei za maji iliyolenga kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira jijini Mwanza,” amesema Sanga.
“Wadau wote walioalikwa walikubaliana na mpango wa MWAUWASA kufanya mabadiliko ya bei za maji,” Mhandisi Sanga amefafanua.
MWAUWASA iliwasilisha Ewura maombi ya kupandisha ankara za maji Januari mwaka huu. Machi, Ewura iliitisha mkutano na wananchi, madiwani, viongozi wa Serikali za Mitaa, watendaji wa mitaa na wateja wa makundi ya watumiaji wa maji, kufanya taftishi (Public Inquiry).