*Wananchi wanakunywa maji na ng’ombe visimani
Na Clement Magembe, Handeni
Wananchi wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, wamesema tatizo la maji limezidi kuwa sugu huku baadhi ya maeneo yakipata maji iwapo viongozi wa kitaifa wanapofanya ziara zao wilayani humo, JAMHURI imebaini.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI kwa miezi sita sasa umebaini kuwa tatizo la maji wilayani humo, limekuzwa na baadhi ya viongozi tangu nchi ilipopata uhuru ambao wamekuwa wakijinufaisha na tatizo hilo kwa kujiingiza katika ulanguzi wa maji. Wanawauzia wananchi ndoo moja kati ya Sh 700 na 1,000.
Viongozi ambao kwa kipindi kirefu wamejikita katika ulanguzi wa maji akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mkata, Hassan Msami, aliyechangia wananchi kuamua kufunga barabara kwa kulala juu ya madumu ya maji waliyoyatandaza barabarani, kwa ukosefu wa maji ni neema. Tukio hilo lilitokea miaka mitano iliyopita wilayani Handeni.
Uamuzi wa wananchi kufunga barabara ulitokana na Msami kuuza maji kwa bei kubwa kati ya Sh 700 hadi Sh 1000 kwa dumu moja lenye lita 20, tofauti na bei ya wafanyabiashara wengine wanouza kati ya Sh 300 na Sh 400 kwa dumu (ndoo). Alitumia mamlaka yake kuzuia wafanyabiashara hao kuendelea kuuza maji kwa bei ya chini hali iliyozua vurugu kubwa.
Kutokana na mzozo huo, uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ulimwondoa Msami katika nafasi hiyo tangu mwaka 2010 ambako kwa sasa hajishughulishi na biashara hiyo ya kuuza maji.
Mwenyekiti wa kijiji
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkata Magharibi, Musa Ngana, ambako ulitokea mzozo huo baada ya Msami kuwalangua wananchi maji, anasema tatizo la maji limeshindwa kupatiwa ufumbuzi kwa muda mrefu na kusababisha wananchi kuishi katika mazingira magumu.
Anasema maeneo yaliyo mbali kijijini humo hali imekuwa ngumu kwani wananchi wanalazimika kununua maji kati ya Sh 2,000 na 2,500 kwa dumu moja lenye ujazo wa lita 20, na kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wanashindwa kupata maji yanayoweza kukidhi mahitaji yao.
Ngana anasema ufumbuzi wa tatizo unaweza ukapatikana kama Serikali itajenga upya miundombinu ya maji kutoka katika mradi wa maji wa Handeni (HTM), ambao kwa sasa miundombinu yake imechakaa na kushindwa kutosheleza mahitaji ya wakazi wa maeneo hayo.
“Kitendo cha kushangaza kwa muda mrefu huduma ya maji haipatikani, lakini anapokuja kiongozi wa kitaifa wananchi wanaofanya biashara ya kuuza maji hapa Mkata wanaamriwa kuondoa madumu yao kando ya barabara kwa lengo la kuwaficha viongozi wa kitaifa kuhusu tatizo la maji,” anasema Mwenyekiti huyo na kuongeza: “Huu ni unafiki wa viongozi waliokuwapo awali ambao ndiyo wamelikuza tatizo hili la maji, mimi na wajumbe wangu hatuwezi kufanya uhuni huu kamwe wa kuficha matatizo mazito kama haya.”
Hata hivyo, anasema kufichwa kwa madumu hayo kunaambatana na upatikanaji wa maji ya bomba kutoka katika mradi wa maji wa HTM ambayo hupatikana hadi mwishoni mwa ziara za viongozi wa kitaifa wilayani humo na tatizo linaendelea tena.
Pamoja na hayo, anasema tatizo la maji lililodumu kwa muda mrefu limegeuka mtaji kwa baadhi ya wanasiasa ambao hawana nia ya kweli kulipatia ufumbuzi.
Wananchi wa Handeni
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Handeni wameieleza JAMHURI kwamba eneo la bwawani ambalo ndilo linalotegemewa na wananchi wengi waishio maeneo ya katikati ya mji kwa maji ambayo chanzo chake kinategemea mvua nyakati za kiangazi hukauka.
Licha ya maji ya bwawa hilo kukauka, maji yanayopatikana yana uchafu wa kila namna unaosombwa na mvua kutoka maeneo yenye miinuko ikiwa ni pamoja na vinyesi vya binadamu kutokana na wananchi wengi kukosa vyoo na kujisaidia vichakani.
Salome Mhando (30), mkazi wa kwa Msisi wilayani humo, anasema wakazi wengi hawana vyoo na kwa muda mrefu wamekuwa wakijisaidia vichakani ikiwa ni tabia iliyojengeka kwa kipindi kirefu na hii inachangiwa na tatizo la maji linalowakabili.
“Maji ni tatizo kubwa sana hapa Handeni na tunachotegemea ni mvua kipindi cha masika, na vipindi vingine ni visima ambavyo maji yake ni chumvi kali sana na tukipikia baadhi ya vyakula kama maharagwe haviivi,” anasema Mhando.
Ramadhan Ndevu, mkazi wa Handeni mjini na mfanyabiashara wa maji kutoka katika bwawa hilo, anasema maji yanayopatikana ni machafu, lakini ndiyo tegemeo kubwa kwa wananchi wengi.
“Haya kama unavyoyaona ni maji machafu sana, yamekusanya kila aina ya uchafu, ndiyo tumaini letu kwa maeneo yote ya Kwenjugo na Kwediamba na kama unavyoona wengine tunakunywa bila hata kuchemsha, tumezoea hali hii kwa muda mrefu,” anasema Ndevu.
Kutokana na tatizo la maji linavyowaathiri kwa kiasi kikubwa wakazi wa wilaya hiyo, wengine wamejipatia ajira ya kuuza maji baada ya kuchimba visima vya kuchuja maji kando ya bwawa hilo. Wanauza kwa Sh 200 kwa dumu lenye ujazo wa lita 20 na kupelekwa kwa watumiaji majumbani ambao huuziwa kati ya Sh 500 na 700.
Anasema amefanya biashara ya kuuza maji kutoka katika bwawa hilo kwa miaka 20 na hivyo kumudu mahitaji ya familia yake licha ya kukauka nyakati za kiangazi. Bwawa hilo lilichimbwa na wakoloni mwaka 1952, ambapo lilihifadhi mahitaji ya wakazi wote kabla ya kupanuka kwa mji na kuongezeka kwa idadi ya watu wilayani Handeni.
Jambo linaloshangaza ni wengi wao kutumia maji yaliyojaa uchafu na tope nyingi kwa kunywa bila kuyachemsha kuua vijidudu, lakini ni wachache wanaopata maradhi.
Asia Salim, anayemiliki visima vinne vya kuchuja na kuuza maji kando ya bwawa hilo, anasema miradi ya maji inayoanzishwa wilayani humo haitoshelezi mahitaji ya wananchi na wakati mwingine hayapatikani.
“Tumejipatia ajira ya kuuza maji katika eneo hili kwa wafanyabiashara wanaowapelekea watu majumbani, na maji ya mvua tunauza kati ya Sh 700 na Sh 1000 kwa dumu,” anasema Salim.
JAMHURI imeshuhudia uchafuzi wa mazingira kando kando ya bwawa hilo ambako vichaka vimegeuzwa vyoo na wafanyabiashara wa maji bila kujali madhara yanayoweza kujitokeza yakiwamo magonjwa ya mlipuko.
Baadhi ya wananchi wameonekana wakinywa maji hayo machafu yanayotoa harufu mbaya bila kuchemsha, kwa madai kwamba hali hiyo wameizoea kwa miaka mingi na pale wanapokunywa maji salama hupata magonjwa.
Mhandisi wa maji
Mhandisi wa Maji wilayani Handeni, Richard Macha, ameiambia JAMHURI kuwa tatizo la maji limedumu kwa zaidi ya miaka 50 huku wilaya hiyo ikikosa chanzo chochote cha maji cha kudumu na tegemeo kubwa hasa kipindi cha kiangazi ni visima ambavyo maji yake ni ya chumvi (hard water).
Macha anasema maji yanayotegemewa kwa matumizi ya majumbani ni maji ya mvua kutoka maeneo yenye miinuko na yanayojikusanya kwenye mabwawa yaliyochimbwa kwa lengo la kuyahifadhi na kuyasambaza kwa wananchi.
Pamoja na vyanzo vikuu vya maji kuwa ni visima na mabwawa, anasema Wilaya ya Handeni ina mabwawa 66 yakiwamo mabwawa makubwa, madogo na malambo ambayo hutegemea maji ya mvua hasa kipindi cha masika.
Anasema Bwawani ni bwawa linalotegemewa na wakazi wengi waishio katikati ya mji na maeneo mengine ya pembezoni, ambalo lilichimbwa na wakoloni wa Kijerumani mwaka 1952 kabla nchi haijapata uhuru. Bwawa jingine ni la Misima ambalo liko umbali wa kilomita 16 kutoka Wilaya ya Korogwe.
Kwa mujibu wa Mhandisi wa huyo wa maji, Bwawa la Misima lenye ujazo wa mita za ujazo 900,000 ujenzi wake umegharimu Sh 295 milioni na Bwawa la Kijiji cha Gendagenda umegharimu Sh 62.5 milioni kutokana na ruzuku za Serikali na wahisani kutoka Shirika la Chakula na Misaada la Japan (JFCA).
“Bwawa la Misima linakidhi mahitaji ya wakazi 13,366 kutoka katika vijiji vinne vya Mbagwi, Malezi, Kibaya na Misima, hata hivyo mahitaji ya maji ni changamoto kubwa wilayani humo”, anasema Macha.
Anasema mradi wa maji wa Handeni Trunk Main (HTM), uliojengwa mwaka 1974 na Wajerumani, utendaji wake hautoshelezi mahitaji na mtandao wake ni chakavu, wakati gharama ya kujenga upya miundombinu yake ni Sh bilioni 140 ambazo hadi sasa hazijapatikana.
Hata hivyo, anasema kama Serikali itaendelea kuchelewesha utoaji wa kiasi hicho cha fedha kilichokisiwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na upanuzi wa mradi huo wa maji wa HTM, gharama zinaweza kuongezeka zaidi na kuondoa matumaini ya upatikanaji wa maji safi kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Bwawa la Kwenkambala lilijengwa mwaka 2003 likiwa umbali wa kilometa 7 katikati ya mji na mashine ya kusuma maji ikiwa umbali wa kilometa 5. Hata hivyo, halifanyi kazi kwa sasa baada ya sehemu ya tuta linalozunguka bwawa hilo kubomolewa na mafuriko mwaka 2012 na 2013.
Mhandisi huyo anasema idadi ya mabwawa yaliyoharibika ni 11, hadi Januari 2015 mabwawa matatu ya Kwenkambala, Kang’ata na Kideleko yametengewa zaidi ya Sh 161 milioni kwa ajili ya ukarabati na kazi inaendelea.
Anasema kisima kirefu cha Nderema ambacho kilichimbwa kabla ya nchi kupata uhuru, bado kinafanya kazi hadi sasa na kinategemewa na wananchi wengi japokuwa kinatoa maji ya chumvi.
“Tumewahamasisha wananchi kuvuna maji ya mvua kwa mujibu wa sheria ndogo tulizotunga ikiwa ni pamoja na kuezeka nyumba kwa mabati na kuweka mantanki ya kuhifadhia maji kwa matumizi ya majumbani, mashuleni, zahanati na taasisi mbalimbali,” anasema.
Shirika la World Vision
Shirika lisilo la kiserikali la World Vision limeanzisha miradi mbalimbali ya maji wilayani humo ikiwamo ya uvunaji wa maji ya mvua katika majengo ya shule na vituo vya afya.
Katika taarifa ya Mhandisi wa Maji wilayani humo, shirika limejenga mabwawa mawili ya kuhifadhia maji katika Kijiji cha Suwa na yote yamekamilika. Ujenzi huo ulianza mwaka 2013 hadi 2014, ambako bwawa la Wimba limegharimu Sh milioni 90.2 na Kwekona Sh milioni 63. Shirika hilo lilitoa fedha, kutafuta na kuwalipa wazabuni na huku kazi ya kusimamia ujenzi ikifanywa na ofisi Mhandisi wa Maji.
Miradi ya Benki ya Dunia
Kwa mujibu wa Macha, miradi ya maji inayoendelea wilayani humo ni katika vijiji vitatu vya Manga, Kwandugwa na Malezi ambako zabuni tayari zimetangazwa.
Amekanusha madai ya wizi wa fedha zilizotolewa na Benki ya Dunia zaidi ya Sh bilioni 300 kwa ajili ya kuanzisha miradi ya maji wilayani humo.
Anasema kabla ya kuanza mradi unaosimamiwa na Benki ya Dunia sharti lao la kwanza ni lazima uwe na Mhandisi Mshauri na pia huwezi kujenga miundombinu kabla ya kuchimba kisima.
Anasema kutokana na maelekezo ya Benki hiyo, uchimbaji wa kisima ni lazima uanze mwaka huo huo wa kwanza wa mradi, jambo ambalo si rahisi kwa watu waliokosa uaminifu kuingiza ufisadi kwenye miradi hiyo.
Hospitali ya wilaya
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni, Dk. Awe William, anasema kukabiliana na tatizo la maji hospitalini hapo wameamua kuchimba kisima cha maji ambacho kinatosheleza mahitaji kwa asilimia ndogo.
Dk. William anasema pamoja changamoto ya maji inayoikabili hospitali hiyo, hawajawahi kusitisha huduma. Hata hivyo, maji yanayopatika yana chumvi. Pamoja na hayo anasema maji kutoka mamlaka ya maji ya HTM yalikuwa na gharama kubwa na pia kutokidhi mahitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli mbalimbali hospitalini hapo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Huddi Shehadi, anasema tatizo la maji ni kubwa na yanayopatikana si salama hivyo wananchi wanapaswa kuchemsha maji hayo kabla ya kunywa.
“Wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapa kutokana na matumizi maji yasiyo salama, ikiwa ni pamoja na kuugua homa za matumbo na magonjwa ya ngozi hadi Desemba mwaka 2013 walifikia asilimia 4.3 kutoka vituo vyote vya afya wilayani hapa,” anasema.
Anasema wananchi wengi wanaougua magonjwa kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama hawatibiwi katika zahanati ama vituo vya afya wilayani humo na wanaopatiwa matibabu ni ambao hali zao zinakuwa ni mbaya, vinginevyo wengi hujitibia nyumbani.
Mbunge wa Handeni
Mbunge wa Jimbo la Handeni, Dk. Abdallah Kigoda, alipotafutwa na JAMHURI kuelezea ufumbuzi wa tatizo la maji kwa wananchi wake, hakupatikana na alipotumiwa ujumbe mfupi (sms) katika simu yake ya kiganjani alidai yuko kwenye vikao.
Hata mwandishi alipokwenda wizarani katika Wizara ya Viwanda na Biashara ambako ni waziri wa wizara hiyo, aliambiwa ana ratiba ngumu wasingeweza kuonana naye.
Waziri wa maji
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, naye alipotafutwa ofisini kwake hakupatikana. Uchunguzi huu umefanywa kwa ufadhili wa Mfuko wa Vyombo vya Habari Tanzania (TMF) wanaovijengea vyombo vya habari nchini uwezo wa kufanya uchunguzi.