Na Cresensia Kapinga, JamhuriMedia, Songea

Hali ya majeruhi wawili wa ajali ya gari iliyotokea juzi katika eneo la daraja la mto Njoka uliopo katika Kijiji cha Namatuhi Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma na kusababisha vifo vya watu 13 wameruhusiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 11,2023 Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Songea (HOMSO), Dkt. Magafu Majura amesema kuwa majeruhi hao awali walikuwa wamelazwa katika kituo cha Afya cha Mpitimbi na baadae walihamishiwa Hospitali ya Serikali ya Mkoa wa Songea kwa matibabu zaidi.

Dkt. Majura amewataja majeruhi hao kuwa ni Hamisi Hassani Mbawala mkazi wa Lizaboni Manispaa ya Songea na Christofa Pius Banda mkazi wa Majengo Manispaa ya Songea ambao waliletwa hospitalini hapo wakiwa na hali mbaya baada ya kufanyiwa uchunguzi Mbawala alionekana na michubuko midogo midogo sehemu za mwili wake alitibiwa na kurudi nyumbani.

Vilevile Banda baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu hakuwa na tatizo lolote ila alipata mshituko baada ya kupata ajali na alitibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Marco Chilya akiongea na waandishi wa habari amesema kuwa hali za majeruhi wanaendelea vizuri japokuwa awali majeruhi hao walilazwa katika kituo cha afya cha Mpitimbi ambako baadae walihamishiwa hospitali ya serikali ya Mkoa kwa matibabu zaidi.

Kamanda Chilya amefafanua kuwa miili ya watu 13 yote imeshatambuliwa na imeshachukuliwa na ndugu zao kwa mazishi isipokuwa mwili mmoja wa Christofa Msuya umebaki kwenye chumba cha kuhifadhia maiti kutokana na ndugu wa marehemu kupanga kusafirisha kesho kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro.

Baadhi ya wakazi wa Songea mjini wamepongeza jitihada zilizochukuliwa na Jeshi la Polisi na kikosi cha zimamoto na uokoaji pamoja na madaktari wa Hospitali hiyo za kuhakikisha kuwa miili yote imetolewa kwenye eneo la tukio kisha kuileta kwenye chumba cha kuhifadhia maiti na kusafirisha kwa ndugu zao kwa kutumia magari ya Jeshi la Polisi.