Kampuni ya uchimbaji dhahabu ya Acacia, inatuhumiwa kutaka kumhonga Rais John Magufuli, Sh bilioni 300 ili aruhusu kusafirishwa kwa makontena 277 ya mchanga wa dhahabu aliyoyazuia katika Bandari ya Dar es Salaam, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.
Kiasi hicho cha fedha kinaweza kujenga barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 300, kwa uwiano wa kilomita moja kwa Sh bilioni moja. Umbali huo ni sawa na kutoka Dar es Salaam hadi Gairo mkoani Morogoro.
Fedha hizo ni zaidi ya bajeti ya kununua dawa za Bohari Kuu ya Dawa (MSD). Bajeti ya MSD ni Sh bilioni 200 kwa mwaka.
Aidha, fedha hizo kama zingeelekezwa shuleni, zingeweza kununua madawati milioni 3.3 na hivyo kumaliza uhaba wa vifaa hivyo katika shule za msingi na sekondari nchini kote.
Chanzo chetu ambacho hakikutaka kutajwa gazetini, kimesema baada ya Rais John Magufuli, kuzuia kusafirishwa kwa makontena hayo yenye makinikia, baadhi ya watu wenye uhusiano wa karibu na Acacia walianza kuhaha kujinasua. Jaribio kubwa likawa la kumfikia Rais. Hata hivyo, hawakufanikiwa.

“Hao jamaa wa Acacia wamekuwa wakijaribu kumfikia Rais Magufuli ili wamhonge Sh bilioni 300…hawakuweza kumfikia. Kitendo hicho kilimfanya Rais achukie zaidi, akaapa kuwatetea Watanzania wanyonge,” kimesema chanzo chetu.
Katika hotuba zake mbili za kupokea taarifa za kamati- ya kwanza iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma, na ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro- Rais Magufuli, alieleza mbinu zilizotumiwa na baadhi ya watu waliotaka ukweli ufichwe.
Rais alimtaja Mbunge wa Igunga, ambaye pia amewahi kuwa Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini Dk. Dalaly Kafumu, kuwa miongoni mwa waliojaribu kwa kila namna kuingilia kazi za tume hizo.
Rais Magufuli, Juni 12, mwaka huu wakati alipokea ripoti hiyo ya kamati ya pili, alieleza namna Dk. Kafumu alivyotaka kuighiribu Kamati ya Profesa Osoro ili ripoti yake ibadilishwe.
Pamoja naye, alimtaja daktari mmoja kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) aliyethubutu kuingilia kazi za Kamati ya awali kwa misingi ya kikabila.

Tuhuma dhidi ya Acacia zimekuja huku kukiwa na mazungumzo yanayoendelea kati ya Serikali na mwekezaji mwenye hisa asilimia 63.9, yaani kampuni ya Barrick Gold Corporation.
Mazungumzo hayo ni matokeo ya tuhuma zilizoibuliwa na kamati zote mbili zilizoundwa na Rais Magufuli kuchunguza sakata la mchanga wa dhahabu.
Wiki iliyopita, Rais Magufuli, alimkaribisha Ikulu Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Barrick Gold Corporation ya nchini Canada, Profesa John Thorton. Wawili hao walikubaliana kimsingi kwamba kuna nafasi ya mazugumzo kwa pande zote mbili.
Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi, na Balozi wa Canada hapa nchini, Ian Myles.
Alipotafutwa kuzungumzia suala hili, Makamu wa Rais wa Acacia Kanda ya Afrika, Deo Mwanyika, hakutaka kutoa maelezo kuhusu tuhuma zinazoikabilia Acacia, badala yake alitaka JAMHURI liwasiliane na Asa Mwaipopo, ambaye anashughulikia uhusiano wa kampuni ya Acacia na Serikali.

Akizungumza na JAMHURI, Mwaipopo amesema wamekuwa wakitoa taarifa zao kwa maandishi kuhusu mtiririko wa matukio yote, huku akisisitiza kuwa kama JAMHURI halijapata nakala, litazipata Jumatatu (jana).
“Ungekuja ofisini Jumatatu, ingekuwa jambo la afya…lakini umesema jambo lenyewe ni dogo tu…tumetoa statement zetu nyingi. Mtu anayetaka kumhonga mwenye mamlaka hawezi kubaki salama,” amesema Mwaipopo.
JAMHURI limemtafuta mmoja wa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Acacia, Balozi Juma Mwapachu, ili kupata ufafanuzi wa tuhuma hizo pamoja na msimamo wake katika ‘vita ya kiuchumi’.
“Siongei na magazeti,” ndilo limekuwa jibu la Balozi Mwapachu, ambaye pia ni mjumbe pekee Mwafrika kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Acacia.
Taarifa ya kamati ya pili, iliyokuwa chini ya Profesa Osoro, ilibainisha kuwa kampuni ya Acacia Mining Plc haikuwa na uhalali wa kisheria kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Kamati imebaini na kuthibitisha kwa mujibu wa nyaraka na maelezo kutoka Ofisi ya Msajili wa Makampuni (Brela) kuwa kampuni ya Acacia Mining Plc haikusajiliwa (incorporation) nchini Tanzania na wala haina hati ya utambuzi (certificate of compliance) kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, Sura ya 212,” inasomeka sehemu ya ripoti ya kamati hiyo.

Katika ripoti yake, Profesa Osoro, anasema kamati ilibaini kampuni ya Acacia Mining Plc, ambayo inajinasibisha kuwa mmiliki wa kampuni za Bulyanhulu Gold Mines Ltd, North Mara Gold Mine Ltd na Pangea Minerals Ltd, haikuwahi kuwasilisha nyaraka kuonyesha umiliki wa kampuni hizo.
“Kwa kuwa Acacia Mining Plc haina usajili wala utambuzi wa kisheria nchini Tanzania, haina sifa ya kupata leseni, kuchimba wala kufanya biashara ya madini nchini Tanzania. Hivyo basi, Kamati imebaini kuwa Acacia Mining Plc inafanya biashara ya madini hapa nchini kinyume cha sheria za nchi,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Mambo mengine yaliyogunduliwa na kamati hiyo ni pamoja na kampuni za Bulyanhulu Gold Mines Ltd na Pangea Minerals Ltd kuwa ndiyo wazalishaji na wauzaji wa makinikia nje ya nchi.
Kamati hiyo ilibainisha kwamba, kwa mujibu wa mikataba ya mauzo ya makinikia baina ya kampuni hizo na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi, makinikia husafirishwa kutoka Tanzania yakiwa yameshauzwa na hupelekwa nje kupitia bandari za Dar es Salaam na Tanga.

“Makinikia hayo hupelekwa nchi za China, Japani na Ujerumani yakiwa kwenye makontena yenye urefu wa futi 20 na wastani wa tani 20 kila moja. Wafanyabiashara wa makinikia ni makampuni ya Aurubis AG na Aurubis Bulgaria ADM, Mark Rich Co. Investment AG na Pan Pacific Copper Co. Limited kutoka nchi za Ujerumani, Uswisi na Australia,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.
Mei, mwaka huu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, alitoa tuhuma za wahujumu uchumi waliotaka kumhonga Rais Magufuli Sh bilioni 300.
Polepole alinukuliwa akisema fedha hizo zililenga kumshawishi Rais Magufuli kusitisha uchunguzi huo, huku akihoji masilahi ya hao waliotaka kumhonga na watu wanaofanya biashara ya kusafirisha makinikia hayo nje ya nchi.
“Kuna watu walitaka kumhonga Rais bilioni 300 ili kusitisha uchunguzi. Walitaka kuhonga bilioni 300 kwa ajili ya kusitisha uchunguzi huo, hivi wao wanapata fedha kiasi gani? Lakini Rais akawatolea nje, akasema subirini uchunguzi ukamilike. Tusimame naye na hakika tutashinda na historia itaandikwa kwamba tulisimama katika kulinda urithi wetu,” alinukuliwa Polepole.