Athari za kupunguza maeneo ya Hifadhi

Mchanganuo wa faida za maeneo yaliyohifadhiwa na zile za ufugaji yanaonesha wazi kuwa hifadhi ya maliasili ni sekta muhimu, pana na mtambuka. 

Sekta hii ndio msingi wa kuwapo kwa maendeleo ya sekta nyingine nyingi za kilimo, mifugo, uvuvi, umwagiliaji, nishati, viwanda na ustawi wa binadamu. 

Profesa Maghembe anasema Maliasili si sekta tegemezi, bali inahitaji kuimarishwa ili kuendelea kuwa mhimili wa kusaidia maendeleo ya sekta nyingine na uwepo wa uhai wa viumbe hai. 

“Kwa mfano, ni dhahiri kwamba maendeleo ya mifugo yatakuwa hatarini endapo maeneo yaliyohifadhiwa yataendelea kumegwa au kuharibiwa kwani mifugo itakosa maji,” anasema. 

Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 32.4 ya eneo la Tanzania limehifadhiwa na hifadhi hizi zimetawanyika katika maeneo mbalimbali. 

“Kwa kuzingatia ukubwa wa nchi yetu, ni muhimu maeneo haya yaendelee kuhifadhiwa kwa ukubwa uliopo ili kutoa huduma za Kiikolojia (Ecosystem services) kama vile maji ambayo ni muhimu kwa kilimo na mifugo na matumizi mengine. 

“Ni vigumu huduma hizi nyeti kupatikana kwa wingi na ubora unaotakiwa bila kuhifadhiwa kwa mifumo ya kiikolojia (Landscape approach) kama ilivyo sasa, na kwa kiasi kikubwa mipaka ya maeneo haya wakati yanaanzishwa ilizingatia hitaji hili,” anasema Profesa Maghembe.

Anasema sekta ya Maliasili inafanya vizuri kiuhifadhi na inatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi yetu. 

“Sekta ya maliasili pia inategemewa sana na sekta nyingine ikiwemo kilimo na mifugo kwa mchango wake wa huduma za kiikolojia. Imeonekana kuwa kuna wimbi kubwa la mifugo kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa kisheria.  

“Tatizo hili limekuwa likiongezeka hasa katika miaka mitano ya karibuni (2010 hadi 2015). Maeneo yanayovamiwa ni pamoja na yale yenye hadhi ya juu kiuhifadhi kama vile Hifadhi Asilia (Nature Reserves), Hifadhi za Taifa (National Parks) na maeneo ya Urithi wa Dunia (World Heritage Sites). 

“Uvamizi huu, si tu kwamba unahatarisha ustawi wa maeneo haya na kutishia ustawi wa utalii kwa ujumla wake, bali pia unakaribisha jangwa na kutoweka kwa maisha ya viumbe hai. 

“Tatizo linalojitokeza kulingana na mchanganuo huu si hasa la upungufu wa ardhi kama inavyodhaniwa, bali ni kuwa kuna ufugaji huria ambao haufuati miongozo ya kitaalamu kwa mujibu wa sera, sheria, taratibu na miongozo ya sekta ya mifugo. 

“Kwa mazingira haya, ipo haja ya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na sheria zilizopo kwa manufaa ya sekta za uhifadhi na ufugaji,” anasisitiza Profesa Maghembe.

 

Hali ilivyo

Pamoja uamuzi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuanzisha Operesheni Taifisha Mifugo katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa hali ni mbaya katika Mapori yote ya Akiba, Mapori Tengefu, Maeneo ya Jumuiya (WMA) na Hifadhi za Taifa.

Mathalani, katika Pori Tengefu la Lake Natron, Mapori ya Akiba ya  

Maswa, Moyowosi, Mwiba (WMA), Ugala na Uvinza; hali ni mbaya mno. 

Maelfu ya ng’ombe wameingizwa katika mapori hayo, huku shughuli za ujangili, ukataji miti kwa ajili ya mbao, uvuvi haramu na ukataji miti kwa ajili ya mkaa vikiwa vimeshamiri.

Katika mapori ya Ugalla na Moyowosi, kuna mamia ya raia kutoka Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo walioweka makazi yao ndani na kuvuna rasilimali za Tanzania, huku wakiwa wanajihami kwa silaha za kisasa.

Mwaka 2014 pekee, majangili 304 yalikamatwa katika mapori hayo; ikiwa ni mbali na wengine 18 waliokamatwa wakiwa wameua tembo. Watu 283 walikamatwa wakikata miti na kupasua mbao, watu sita walikuwa wakilina asali; wavuvi haramu 142 walikamatwa.

Pia watu 881 walikamatwa kwa kuingia bila ruhusa katika mapori hayo; wachunga mifugo 853 walitiwa mbaroni; na wachoma mkaa 81 walikamatwa. Bunduki 49 zilikamatwa kwa mwaka huo pekee. Juma ya watu wote waliokamatwa kwa mwaka huo kwa kuingia kwenye mapori hayo kinyume cha sheria kwa lengo la kufanya uhalifu mbalimbali ni 2,617.

Katika Pori la Akiba la Moyowosi; majangili wengi wanaokamatwa wanatoka Burundi na DRC. Mwaka 2013 pekee zilikamatwa bunduki 163. Matumizi ya silaha katika Pori hili, kama yalivyo mengine ni makubwa, na inakuwa vigumu kwa askari wanyamapori wa Serikali na wale wa kampuni za uwindaji wa kitalii wasio na silaha kukabiliana nao.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2006, tembo 108 waliuawa katika mapori ya Moyowosi na Uvinza; rekodi inayotajwa kuwa ni ndogo ikilinganishwa na hali halisi. 

Ujangili wa wanyamapori na samaki vinatajwa kushamiri Kusini mwa Moyowosi hadi katika Ziwa Nyamagoma. Majangili wameanzisha kambi ndani ya eneo oevu wakikausha nyama na samaki na kupeleka katika masoko ya ndani na mengine ya nje ya nchi. Kukabiliana na majangili katika eneo hilo kunahitaji nguvu za kijeshi kutokana na jiografia ya eneo hilo kutofikika kirahisi.

Mifugo inatajwa kuchukua eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba zaidi ya 200 za Moyowosi na kusababisha athari kubwa za kimazingira. Hali kama hiyo ipo pia kaatika Pori la Uvinza ambalo limevamiwa kwa kiwango cha kutisha.

Katika eneo la Natron ambalo wenyeji wake wengi ni wa kabila la Wamasai, hali ni mbaya baada ya wenyeji hao waliodhaniwa kuwa walinda wanyamapori, sasa kuwa miongoni mwa watuhumiwa wakuu wa ujangili wa tembo na wanyama wengine kama pundamilia ambao huwaua na kuchukua ngozi zinazouzwa nchi jirani.

Matukio mengine ya uharibifu wa uhifadhi ni biashara ya mkaa na kuni ambayo hupelekwa Kenya ambako kuna soko kubwa.

Kwa hali ilivyo, kuna kila sababu kwa wadau wote wa uhifadhi, kuungana kuhakikisha kuwa mifugo inaondolewa katika Mapori ya Akiba, kama njia ya kuyalinda dhidi ya uharibifu wa mazingira na majangili wanaotumia mwanya huo kuua wanyamapori. 

Hali katika mapori ni mbaya. Hatua za makusudi na za haraka zisipochukuliwa, Tanzania itapoteza urithi huu.