Kamanda Mambosasa akionyesha sare za mtuhumiwa anayefahamika kwa jina la Said Selemani (17) mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Fahari iliyopo Goba kwa kosa la kukutwa na sare za JWTZ (Kombat). Anayeonekana pichani.

 

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 28/11/2017 na tarehe 30/11/2017 askari walifanya oparesheni maalum ambayo ilifanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa watatu ambao wanajihusisha na matukio ya uporaji na mauaji mbalimbali katika jiji la Dar es salaam.

Baada ya mahojiano watuhumiwa hao walikubali kuonyesha silaha moja aina ya AK.47, Magazine mbili (2) na risasi 57 ambayo walikuwa wameificha kwenye kichaka karibu na eneo la Ubungo Mawasiliano,pia walionyesha na pikipiki mbili aina ya Boxer zenye namba za usajili MC 757 BCT rangi nyekundu na MC 946 BSE rangi nyeusi ambazo walizipora katika matukio mbalimbali.

Pia walipohojiwa zaidi walisema wanazo silaha nyingine ambazo wamezificha kwenye kichaka eneo la Ununio na wako tayari kwenda kuonyesha silaha hizo,walipofika huko wakati wakishuka kwenye gari jambazi mmoja raia wa Burundi aliyefahamika kwa jina la FANUEL LUCHUNDA KAMANA@MRUNDI alimvamia askari kwa lengo la kumpora silaha huku wenzake wawili wakijaribu kutoroka na ndipo walijeruhiwa
kwa risasi.

Majambazi hao waliwahishwa katika hospitali ya Mwananyamala ili kupatiwa matibabu na ndipo madaktari wakabaini kuwa tayari wameishafariki dunia. Miili hiyo imehifadhiwa hospitalini hapo kwa hatua za uchunguzi wa kitaalamu, Aidha majambazi hao walikiri kufanya matukio kadhaa ya uporaji na mauaji likiwemo tukio la mauaji huko Kunduchi Mtongani la tarehe 19/11/2017 ambapo huwaua madereva bodaboda na kupora pikipiki zao na kuziuza kwa TSHS.800, 000/=. Majambazi wengine waliofariki ni GALLUS MARANDU CLEMENT (31) na FREDRICK WILBORD ACHOLO mkazi wa Gongo la Mboto.

KUKAMATWA KWA GARI MOJA NA RADIO CALL ZILIZOKUWA ZIKITUMIWA NA MAJAMBAZI KATIKA MATUKIO MBALIMBALI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 29/11/2017 majira ya 1100hrs huko maeneo ya Mbezi Msumi lilifanikiwa kukamata gari moja aina ya Toyota Ipsum lenye namba za usajili T.142 CNF rangi ya “silver”, Radio
call moja aina ya Motorola ya mawasiliano,kamba za katani na vipande viwili vya nondo vilivyokuwa vikitumiwa na kundi la majambazi wapatao watano(5) waliokuwa wamevamia katika nyumba ya ERICK MKWEMWA.

Awali majambazi hao wapatao watano walifika katika nyumba hiyo na kujitambulisha kuwa wao ni maofisa wa Polisi waliofika hapo kwa ajili ya kufanya upekuzi lakini badala yake waliwaweka chini ya ulinzi familia hiyo
na kuwafunga kamba mikononi,miguuni kisha kuwaziba na plasta mdomoni na hatimaye majirani wa eneo hilo walitilia mashaka kitendo hicho na kuamua kuizingira nyumba hiyo huku wakitoa upepo matairi ya gari.

Aidha majambazi hao walipobaini kitendo hicho walianza kukimbia huku wakifukuzwa na wananchi ambapo wawili kati yao walikamatwa na kuanza kushambuliwa kwa kupigwa fimbo/mawe na hatimaye walifariki
dunia huku wengine watatu wakifanikiwa kutoroka. Miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili huku msako mkali ukiendelea ili kuwakamata majambazi wengine 3 waliokimbia.

KUKAMATWA KWA MTUHUMIWA MMOJA AKIWA NA SARE ZA JESHI LA WANANCHI TANZANIA
Jeshi la Polisi Kanda Maalum DSM linamshikilia mtu mmoja anayefahamika kwa jina la SAID SELEMANI (17) mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari FAHARI iliyopo Goba kwa kosa la kukutwa na sare za JWTZ
(Kombat).

Mwanafunzi huyo alikamatwa huko maeneo ya Mbezi CRDB bank akiwa amevaa sare hizo za JWTZ huku akivuta sigara hadharani na kufanya vitendo vingine ambavyo haviendani na maadili ya askari aliyevaa sare.

Katika mahojiano ya awali kijana huyo alijitambulisha ni askari toka kikosi cha 501 KJ kilichopo Lugalo jijini Dsm,baada ya kubanwa zaidi alikiri kupata uniform hizo toka kwa rafiki zake anaokuwa nao sehemu mbalimbali.

Aidha alipopekuliwa katika begi la mgongoni alilokuwa nalo alikutwa na kofia nyingine moja pamoja na kitambulisho namba DFF 7001A cha familia ya askari chenye namba 1231 ambacho ni cha mtoto wa askari wa JWTZ
MT 65640 Private GABRIEL KIHWILI wa 501 KJ kikiwa na picha ya mtoto wake ELIA GABRIEL

Uchunguzi bado unaendelea ili kuwapata rafiki zake hao ambao
inadhaniwa kuwa huwa wanashirikiana katika kufanya matukio ya kihalifu.

KUUWAWA KWA JAMBAZI SUGU ANAYETUMIA BASTOLA FEKI KUPORA PIKIPIKI

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 30/11/2017 majira ya 2250 hrs huko maeneo ya Buza Sigara lilifanikiwa kukamata silaha moja aina ya Bastola ambayo imetengenezwa kienyeji (bastola feki) iliyokuwa
inatumiwa na jambazi sugu katika matukio ya uporaji wa pikipiki.

Awali jambazi huyo alimkodi dereva pikipiki ili ampeleke maeneo ya Msitu wa Jeshi huko Buza lakini ghafla walipofika maeneo hayo jambazi huyo alitoa bastola yake iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na baruti na kumuamuru
dereva ashuke na kumuachia pikipiki,baada ya kushuka dereva alipiga kelele kuomba msaada na ndipo wananchi walijitokeza na kuanza kumpiga kwa mawe huku wengine wakimkata mapanga jambazi huyo.

Askari walipata taarifa na walipofika eneo hilo walimkuta jambazi huyo akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake na ndipo walimkimbiza katika hospitali ya Temeke kwa ajili ya matibabu na muda mfupi baadae alifariki dunia.
Aidha marehemu huyo anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka (25-30) na mwili wake umehifadhiwa katika hospitali ya Temeke kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kitaalamu.

KUPATIKANA KWA BAJAJI YA WIZI
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dsm mnamo tarehe 20/11/2017 lilifanikiwa kukamata bajaji moja aina ya TVS yenye namba za usajili MC 473 BMM

rangi ya blue iliyoibwa mnamo tarehe 10/4/2017 huko Kigamboni Mjimwema nyumbani kwa CHANDRA KANDRI.
Baada ya askari kupata taarifa ya kupotea kwa bajaji hiyo ufuatiliaji ulianza
mara moja na ndipo Bajaji hiyo ilipatikana huko Sumbawanga mkoani

Rukwa ikiwa imetelekezwa na watu wasiojulikana baada ya kushindwa kufanya zoezi la kubadilisha umiliki wake.
POLISI KANDA MAALUM DSM KIKOSI CHA USALAMA BARABARANI
KUANZIA TAREHE 25.11.2017 HADI TAREHE 04.12.2017 KIMEFANIKIWA KUKUSANYA TSH 1,007,610,000/=KWA TOZO ZA MAKOSA YA USALAMA BARABARANI
Jeshi la Polisi kanda maalum Dar es salaam kupitia Kikosi chake cha
Usalama barabarani kinaendelea na oparesheni ya ukamataji wa makosa ya
Usalama Barabarani kwa kipindi cha kuanzia tarehe 24.11.2017 hadi tarehe
04.12.2017 kama ifuatavyo:-
1. Idadi ya magari yaliyokamatwa – 32,471
2. Idadi ya Pikipiki zilizokamatwa – 1,145
3. Daladala zilizokamatwa -10,752
4. Magari mengine (binafsi na malori) -21,719
5. Bodaboda waliofikishwa Mahakamani
kwa makosa ya kutovaa helmet na kupakia mishikaki -55
Jumla ya Makosa yaliyokamatwa – 33,587
6. Fedha za Tozo zilizopatikana – 1,007,610,000 /=

Aidha wananchi wanatangaziwa kutumia namba 41.59.7.174/tms kwa simu zao za mikonononi zenye uwezo wa internet kwa kutumia Browser ya google kwa maulizo ya faini zilizoandikwa kwa mashine za kielektroniki
Traffic Management Systems (TMS). Vile vile madereva wanaaswa kulipa faini ndani ya muda wa siku saba(7) ili kuepukana na usumbufu wa kukamatwa pamoja na ongezeko la tozo za faini.
LAZARO.B.MAMBOSASA – SACP KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM