Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa idara na taasisi zote za Serikali watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia sheria hususan katika huduma wanazozitoa na miradi wanayoisimamia ili kuiepusha Serikali kuingia katika migogoro ambayo inaweza kuepukika.
“Watendaji wote wa Serikali zingatieni sheria, taratibu na kanuni tulizojiwekea kwenye utekelezaji wa majukumu yetu ikiwemo usimamizi wa mikataba na makubaliano mbalimbali tunayoingia ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima inayoweza kutokea ndani ya Serikali na kusababisha kufunguliwa kwa mashauri ya madai na usuluhishi.“
Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 5, 2023) katika Maadhimisho ya Miaka Mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Uzinduzi wa Mafunzo kwa Mawakili wa Serikali katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Amewasisitiza Mawakili hao wawe wabunifu katika kuishauri Serikali ipasavyo kuhusu mashauri yaliyopo.
Waziri Mkuu amesema Mawakili wa Serikali wamepewa dhamana kubwa ya kuitetea Serikali katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi, hivyo waongeze bidii na juhudi katika utendaji kazi na wafanye kazi kwa uzalendo, weledi na uadilifu.
“Serikali kwa upande wake itaendelea kuitengea bajeti ya kutosha Ofisi hii kwa kadri rasilimali zitakavyoruhusu. Vilevile, itaendelea kuipatia rasilimali watu ya kutosha sambamba na kuwezesha upatikanaji wa mafunzo kwenye maeneo ya kimkakati kama vile mafuta na gesi, uwekezaji, sheria za anga na madini.“
Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuendelea kujenga mazingira shindani ya kuvutia wawekezaji, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Wizara, Idara na taasisi za Serikali itatue migogoro kwa njia ya majadiliano na maridhiano.
Mheshimiwa Majaliwa amesema faida ya kutatua migogoro kwa njia ya majadiliano ni pamoja na kupunguza gharama, kuokoa muda na kulinda mahusiano ya kibiashara na kidiplomasia. “Nisisitize kuwa, bado Serikali yetu inahitaji wawakezaji katika kuchangia ukuaji wa haraka wa uchumi na pato la Taifa.“
“Wizara, Idara na Taasisi za Serikali fanyeni kazi kwa karibu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi yanayohusu Serikali kwani ndiyo yenye mamlaka ya kisheria ya kusimamia mashauri yanayohusu Serikali na Taasisi zake ndani na nje ya nchi.“
Pia,Waziri Mkuu ametoa msisitizo kwa taasisi zote za umma zenye Mawakili wa Serikali kuzingatia suala la utatuzi wa kero za wananchi ili kupunguza mlundikano wa mashauri ambayo hayana ulazima wa kufikishwa Mahakamani hususan katika kipindi hiki cha miaka mitatu ambacho Wizara ya Katiba na Sheria inatekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Msaada wa Kisheria nchini kote “Mama Samia Legal Aid Campaign”
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema katika kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo ambayo inafanya kazi kwa weledi imeweza kuisaidia Serikali kuokoa zaidi ya shilingi trilioni saba kutokana na kutatua baadhi ya mogogoro kwa njia ya usuluhishi.
Naye, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende amesema baada ya uzinduzi huo wanatarajia kuendesha mafunzo ya siku tatu kwa Mawakili wa Serikali zaidi ya 600 ili kuwaongezea ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.