Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza Wizara na Taasisi zote zinazohusika na maendeleo ya lugha ya kiswahili wawatumie vema wataalamu wa lugha hiyo waliopo nchini wakiwemo kutoka Vyuo Vikuu, Mabaraza ya Kiswahili na Vyama vya Kiswahili katika kukitangaza na kukibidhaisha kiswahili ili kitumike kama lugha ya ukombozi na kusaidia kuleta umajumui wa Afrika.
Pia,Majaliwa ametoa wito kwa balozi za Tanzania kuhakikisha zinaendeleza jitihada za kukuza na kufundisha Kiswahili katika ofisi za ubalozi na kuwashirikisha wadau wengine kama Diaspora na asasi nyingine zenye nia ya kukuza na kuendeleza Kiswahili.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Januari 25, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika mwaka 2022 iliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Tuzo hizo zinadhaminiwa na Kampuni ya Mabati ya ALAF Limited – Tanzania ikishirikiana na kampuni ya Mabati Rolling Mills ya Kenya, chini ya uratibu wa Chuo Kikuu cha Cornell cha nchini Marekani.
“Muda mrefu imekuwa ikizoeleka kwamba lugha ya kiswahili inatumika katika masuala ya kitaaluma. Lugha hii kwa sasa imeshavuka mawanda ya kitaaluma na inatumika katika nyanja za uchumi na biashara. Kwa kuzingatia ukweli huo leo tunashuhudia kwa macho yetu Kampuni ya ALAF ikitoa tuzo na ufadhili wa wanafunzi wanaosomea shahada ya umahiri katika Kiswahili.”
Waziri Mkuu amewasisitiza waalamu wa kiswahili wakikishe kwamba wanaweka mikakati thabiti ya kupenyeza lugha ya kiswahili nje ya nchi kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandika kamusi na vitabu vitakavyowasaidia watu kujifunza lugha hiyo adhimu. “Vilevile, sambazeni vijitabu vyenye misamiati muhimu kwa wasomaji wa awali wa lugha ya Kiswahili, viwekeni kwenye mitandao ili viweze kusomwa na watu wengi zaidi duniani.”
Pia, Majaliwa ameiagiza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo yenye dhamana ya lugha ya Kiswahili, ieendelee kuratibu vema na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakua na kuenea. “Tunataka Tanzania iendelee kuwa kinara wa maendeleo ya lugha ya Kiswahili, waunganisheni wadau wa Kiswahili ili waone kwa namna gani watashiriki katika utekelezaji wa Mkakati wa Kubidhaisha Kiswahili Kitaifa na Kimataifa.”
“Ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo yoyote hayawezi kufikiwa bila kuwekeza vya kutosha katika lugha. Nchi zilizoendelea zimepiga hatua kubwa ya maendeleo kwa kutumia lugha zao. Hivyo, ninaendelea kutoa wito kwa washiriki wote kila mmoja aweke dhamira ya kuwekeza katika lugha ya Kiswahili kwa maendeleo endelevu ya taifa letu.”
Amewahakikishia kwamba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu itaendelea kuwaunga mkono watu wote wenye nia ya dhati ya kuleta maendeleo ya Taifa pamoja na kuendelea kuunga mkono juhudi zote zenye lengo la kuendeleza nchi yetu na wananchi wake.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa tuzo hizo amesema tangu kuanzishwa kwake tayari waandishi 15 wameshinda na jumla ya waandishi 847 walijitokeza katika kuwania tuzo hiyo ambapo katika shindano la mwaka 2022 pekee walijitokeza waandishi 264 ikilinganishwa na waandishi 65 waliojitokeza mwaka 2015. “Hivyo basi, ni matumaini yangu kwamba shindano la mwaka 2023 litakuwa na idadi kubwa zaidi ya waandishi watakaothubutu.” Walioshika nafasi ya pili wamepata Dola za Marekani 2,500 na Dola za Marekani 5,000 kwa nafasi ya kwanza.
Amesema mbali na kampuni ya ALAF kudhamini tuzo hizo pia imeendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa Shahada ya Umahiri ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwamba hadi sasa wanafunzi 12 wamenufaika na ufadhili huo.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameupongeza uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuanza kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosoma Kiswahili kutoka nchi za nje za Bara la Afrika na ufadhili wao unahusisha vipengele vyote ikiwa ni pamoja na ada na fedha za kujikimu. “Hii ni hatua muhimu sana kwa maendeleo ya Lugha Kiswahili ndani na nje ya nchi.”
Amesema kitendo hicho kinaonesha ni kwa namna gani Serikali inatekeleza dhamira yake ya kuendeleza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania. “Kitendo hicho kimefuta ile dhana ya Watanzania kuwa wapokeaji wa ufadhili kutoka nchi mbalimbali. Tulizoea kuona Watanzania wanaomba ufadhili katika vyuo na nchi mbalimbali lakini sasa umefika wakati Tanzania inatoa ufadhili kwa nchi nyingine kuja kujifunza Kiswahili.”
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema katika kuendeleza ukuzaji wa lugha ya kiswahili, wizara inaendelea kufuatilia mchakato wa kujengwa kwa Chuo Kikuu cha Kiswahili na Stadi za Kiafrika, ambapo ujenzi wa chuo hicho utakuwa ni matunda ya jitihada za serikali ya awamu ya sita ambayo imekuwa ikisimamia kwa karibu maendeleo ya lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa wizara yao tayari imekwisha zindua Mfuko wa Utamaduni na Sanaa na umeanza kuwanufaisha wasanii na wanautamaduni wote wenye sifa na waliokidhi vigezo ikiwemo watunzi na wataalamu wa Lugha ya kiswahili nao ni moja ya wanufaika na mfuko huo ambao wameanza kupatiwa mikopo nafuu ili waweze kuiendeleza na kuikuza lugha hiyo.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya ALAF-Tanzania, Ashish Mistry alisema kila mwaka kampuni yao inatoa Dola za Kimarekani 50,000 kila mwaka kwa ajili ya kufanikisha utoaji tuzo hizo.
Pia kampuni hiyo imeweza kutoa udhamini wa wanafunzi 12 wa Shahada ya Umahiri (M.A) ya Kiswahili tangu kuanzishwa kwa tuzo hizo na wataendelea kufanya hivyo hadi mwaka 2025. Lengo la ALAF ni kuimarisha matumizi sambamba na kukitangaza Kiswahili barani Afrika na duniani kwa ujumla.