………………………………………………………………………………………………………………………
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa wa Mheshimiwa Rais wa awamu ya nane wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi jumla ya miradi 215 imesajiliwa kupitia Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3.26.
“Miradi yote hii inatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 13,000. Mafanikio haya yote kwa kipindi hiki kifupi, yamechangiwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane zikiwemo sera na mipango madhubuti iliyowekwa na Chama cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2020.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatano, Jaruari 11, 2023) baada ya kuzindua mradi wa hoteli ya Kilindini yenye hadhi ya nyota tano inayomilikiwa na kampuni ya KILINDINI COMPANY LIMITED iliyoko katika kijiji cha Pwanimchangani wilaya ya Kaskazini A ikiwa ni sehemu ya matukio muhimu yaliyojumuishwa katika maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 59 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar.
Amesema wananchi wana kila sababu ya kuyaenzi mapinduzi hayo kwa sababu ndicho chombo kilichowavusha kutoka katika gharika za kutawaliwa na kubaguliwa katika nchi yao. “Kwa mnasaba huo, sherehe hizi za kuadhimisha Mapinduzi matukufu ya Zanzibar zinakua ni sehemu ya historia muhimu kwani zinatukumbusha jinsi ambavyo wakulima na wafanyakazi wanyonge walivyokataa madhila ya kubaguliwa na kunyanyaswa.”
“Kukusanyika kwetu hapa katika kijiji cha Pwani Mchangani ni kielelezo kingine cha uwepo wa amani na usalama katika nchi yetu. Uwepo wa amani na usalama umekuwa chachu katika kuvutia wawekezaji wengi wa kigeni na hivyo, kuvifanya visiwa vyetu vya Unguja na Pemba kuwa sehemu sahihi ya kuwekeza mitaji yao.”
Amesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt.Mwinyi wanao mkakati endelevu wa kukuza sekta ya uwekezaji nchini ikiwemo kushirikisha sekta binafsi nchini na kuvutia mitaji kutoka nje kwa lengo kuhakikisha nchi zetu zinakuwa na uchumi imara
“Ninapenda kutumia fursa hii kuwapongeza wamiliki kwa kuichagua Zanzibar kuwa sehemu ya kuwekeza mradi huu mkubwa. Binafsi, ninaamini kuwa uamuzi huu wa kuwekeza hapa nchini umetokana na uzuri wa visiwa vyetu pamoja na imani kubwa”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZIPA, Shariff Shariff amesema mradi huo unaomilikiwa na wawekezaji wanne ambao ni Elias Micheal na Rabih Micheal kutoka Italia pamoja Monica Seavendra Perez na Osca Seavendra Perez kutoka Uhispania umegharimu dola za Kimarekani milioni 13 sawa na shilingi bilioni 30. Hoteli imeajiri watumishi 62 kati yake 59 ni Watanzania.
Awali, Katibu Mkuu wa Afisi ya Rais anayeshughulikia Uchumi na Uwekezaji, Habiba Omar alisema tangu kuasisiwa kwa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar jumla ya miradi 1,225 imesajiliwa kupitia ZIPA ikiwa na thamani ya dola za Kimarekani bilioni 16.4. Kati ya miradi hiyo 452 sawa na asilimia 37 ni miradi ya hoteli, ambapo hoteli 38 zina hadhi ya nyota tano.