Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali haitodharau maoni na ushauri wanaoutoa kuhusu maeneo yenye hofu kwenye mradi wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali pamoja na wawakilishi wao ndani ya Bunge, kwani Serikali imejidhatiti kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi unaoendana na mahitaji ya sasa na kwa kuzingatia manufaa ya kijiografia ya nchi yetu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo Juni 20, 2023 katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya chuo cha International Evangelism Centre kilichoko Sakila jijini Arusha. Amesisitiza kwamba bandari haijauzwa, bali Serikali inataka kubadilisha muwekezaji ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi na tija zaidi.
Amesema pamoja na maboresho yaliyofanyika, hali ya utendaji wa Bandari ya Dar es Salaam imeendelea kuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na bandari shindani kikanda. Kwa mfano, wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es salaam ni siku tano ikilinganishwa na wastani siku moja na nusu kwa Bandari za Mombasa na Durban.
Amesema udhaifu huo uliopo katika bandari hiyo unasababisha meli kusubiri muda mrefu nangani na hivyo kuongeza gharama, kwa siku moja ni takriban Dola za Marekani 25,000, sawa na takriban shilingi milioni 58 kwa siku.
Waziri Mkuu amesema kitendo cha meli kutumia muda mrefu kupakia na kupakua shehena gatini kwa wastani wa siku tano ikilinganishwa na siku moja inayokubalika kimataifa kinasababisha meli kubwa kutokuja katika bandari ya Dar es Salaam.
Mheshimiwa Majaliwa amesema hali hiyo huikosesha nchi mapato ambayo yangeweza kutumika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini ambayo ingesaidia kukuza uchumi na kuboresha huduma za wananchi.
Waziri Mkuu amesema ili kutatua changamoto za bandari zilizopo na kuongeza ufanisi katika mapato, ajira na kuchagiza sekta nyingine za kiuchumi, Serikali ilifanya maamuzi ya kutafuta wawekezaji wapya wanao endana na dhima ya Serikali.
Amesema tarehe 10, Juni, 2023 Bunge liliridhia mkataba unaohusu makubaliano ya mahusiano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai (IGA) ili kuwezesha majadiliano ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Amesema miradi hiyo ni pamoja na ya uendelezaji na uboreshaji wa huduma za bandari nchini. “Kilichofanyika sasa ni kuwezesha tu baadaye kuwa na mikataba ya maeneo maalum ambayo itazingatia maslahi ya nchi kisheria na kibiashara bila kuathiri usalama Taifa.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema wakati wa kuingia mikataba utakapofika wataalamu wa uchumi nchini wataishauri Serikali kuhusu muda wa uendeshaji wa uwekezaji huo, hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na subra.