Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali itafanya uchunguzi kwa vyama vya Msingi vya Ushirika (AMCOS) wilayani mbozi mkoani Songwe na watakaobainika kuhusika na ubadhirifu wowote watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo baada ya Mbunge wa Jimbo la Mbozi, George Mwanisongole kuzilalamikia AMCOS za wilaya hiyo kuwanyonya wakulima wa kahawa na hivyo kuwafanya wauchukie ushirika.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumanne, Februari 14, 2023) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Mlowo wilayani Mbozi akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Songwe ya kukagua miradi ya maendeleo na mafanikio ambayo Serikali ya awamu ya sita imeyapata katika kipindi cha miaka miwili.

“Ushirika ni muhimu kwa maendeleo ya wakulima lakini wanahitajika wanaushirika waaminifu, hivyo tutakuja kufanya uchunguzi wa mwenendo wa AMCOS za Mbozi ili kubaini wabadhirifu na kuwachukulia hatua. Pia tutachunguza makato wanayokatwa.”

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbozi, Mwanisongole ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia takribani shilingi bilioni 10 kupelekwa katika jimbo hilo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka miwili.

Amesema miongoni mwa miradi hiyo ni ya maji yenye thamani ya shilingi bilioni 5.3, miradi ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mbili pamoja na vyumba vya madarasa shilingi bilioni tatu pamoja na shilingi bilioni 1.65 zilizotumika kwa ajili ya miradi ya sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa kituo cha afya, zahanati na jengo la mama na mtoto (Itaka).

Pia, mbunge huyo amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa kuridhia shilingi bilioni 150 kwenye ruzuku ya mbolea ambayo imekuwa mkombozi kwa wakulima ambao awali walikuwa wanauziwa mfuko mmoja wa mbolea kwa shilingi 130,000 na baada ya ruzuku bei imeshuka na sasa wananunua kwa shilingi 70,000.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Waziri Kindamba ahakikishe anawasimamia viongozi wa wilaya ya Momba akiwemo mkuu wa wilaya hiyo wahamie katika kituo chao cha kazi badala ya kukaa Tunduma.

Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali la kuwapeleka watendaji wilayani humo ni kusogeza huduma za jamii karibu na makazi ya wananchi, hivyo ni vema wakaishi katika vituo vyao vya kazi ili kutimiza lengo hilo.

“Watumishi wa Momba wanaoishi Tunduma wahamie hapa, kila mmoja awajibike kwa nafasi yake. Mmeletwa Momba wahudumieni wana-Momba na haya ndio matarajio ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia na siyo kuishi Tunduma halafu kazi mnafanya Momba.

Ametoa agizo hilo baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi jengo la utawala la halmashauri ya wilaya ya Momba linalojengwa katika kata ya Chitete kijiji cha Tindingoma kwa gharama ya shilingi bilioni 2.7.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godfrey Mollel amesema Serikali imepeleka shilingi bilioni 47 mkoani Songwe kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa hospitali ya mkoa, hospitali za halmashauri zikiwemo shilingi bilioni 3.7 zilizopelekwa wilayani Momba.