WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, upendo, umoja, mshikamano, kuhurumiana sambamba na kujiepusha na vitendo vinavyoashiria vurugu, uonevu na uvunjifu wa amani.
Pia amewasihi waimarishe malezi kuanzia ngazi ya familia ili kuepuka athari za mmomonyoko wa maadili nchini na kuhakikisha mienendo ya vijana na wanajamii wote inazingatia mila, desturi na tamaduni zetu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Juni 17, 2024) wakati wa hafla ya Baraza la Idd El-Adh’haa Kitaifa lililofanyika katika Msikiti wa Mfalme Mohamed VI Bakwata Makao Makuu, Kinondoni jijini Dar es Salaam.
“Ninawashukuru nyinyi na madhehebu yote ya dini kwa kuendelea kuiombea nchi yetu amani, mshikamano na utulivu. Amani tuliyo nayo, ndiyo chachu kubwa ya kufikia mafanikio ya maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.”
Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo kuwapongeza BAKWATA kwa mipango na uratibu mzuri wa shughuli za ibada ya Hijja kwa mahujaji wa Tanzania kwa mafanikio makubwa na Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati ili kuwezesha Waislamu kutekeleza nguzo hiyo muhimu. Pia ametoa wito kwa BAKWATA wasimamie weledi wa taasisi zote zinazowapeleka waislamu hija kama wanavyoratibu wao.
Awali, Katibu Mkuu wa Bakwata, Alhaj Nuhu Jabiri Mruma amewasihi waislamu na Watanzania kwa ujumla waendelee kujenga umoja bila kujali madhehebu yao ili waendelee kuilinda na kudumisha amani kwani bila amani hawaweza kupata fursa ya kufanya ibada na shughuli zingine za kimaendeleo.
Alhaj Mruma pamoja na mambo mengine amewasisitiza waislamu kutunza mazingira na kwamba BAKWATA inatarajia kuzindua zoezi la upandaji miti Juni 20, 2024, lengo likiwa ni kushirikiana na Serikali katika utunzaji wa mazingira kwani kufanya hivyo ni ibada.
Pia, Kiongozi huyo ametoa wito kwa Waislamu nchini kote kushiriki katika uchaguzi iwe kwa kuchaguliwa au kuchagua kwani ni haki yao kikatiba, hivyo amewataka waislamu kujitokeza kwa wingi muda utakapo wadia kuanzia hatua ya uboreshwaji wa daftari la mpiga kura kwani ni haki yao ya msingi kikatiba.