Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwaunga mkono wadau wa sekta binafsi katika jitihada zote za kuimarisha ustawi wa watoto wa Tanzania.
Amesema kuwa Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha kunakuwa na ustawi na afya ya mtoto sambamba na kuimarisha upatikanaji wa huduma za elimu kwa watoto wenye ulemavu hapa nchini.
Ameyasema hayo leo baada ya kushiriki mbio hizo za hisani zilizoandaliwa na benki ya Maendeleo zilizofanyika katika viwanja vya Farasi, Oysterbay jijini Dar es Salaam ambapo ameisisitiza jamii ishiriki katika ulinzi wa watoto wenye ulemavu kwa kutoa taarifa kuhusu matukio ya ukatili dhidi ya watoto hao.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imehakikisha hospitali zote za wilaya zinatoa huduma za watoto wachanga ikiwemo huduma ya mama kangaruu (Mother Kangaroo) kwenye vituo vya afya nchini. “Hii ni huduma maalum ya kutunza watoto njiti na wale waliozaliwa na uzito mdogo”
- Advertisement -Ad image
“Serikali inatekeleza utoaji wa huduma ya kumsaidia mtoto mwenye usonji ili aweze kuongea (speech therapy) pia kutoa huduma ya kumsaidia mtoto ili aweze kufanya matendo mbalimbali (occupational therapy)”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania kuweka utaratibu wa kufanya mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa sasa yamekuwa tishio kwa jamii yetu. “Jiungeni na vikundi vya mazoezi ili muweze kupata hamasa ya kufanya mazoezi”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka waandaaji wa mbio hizo waone namna bora ya kufikisha taarifa kwa umma kuhusu matunda ya mbio hizo ili jamii iweze kuhamasika na kuendelea kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio za hisani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo, Dkt. Ibrahim Mwangalaba amesema katika kusherehekea miaka 10 ya kuanzishwa kwa benki hiyo waliamua kuandaa mbizo za hisani kwa lengo la kutafuta shilingi milioni 200 kusaidia vituo viwili vyenye uhitaji maalumu.
“Lengo la Mbio hizo ni kukusanya fedha kwa ajili ya kukarabati majengo ya kituo cha kulea watoto wenye ulemavu wa akili maarufu kama “Mtoni Maalum” cha Dar es Salaam kinachohudumia watoto wenye mtindio wa ubongo, Down Syndrome na Usonji na kununua vifaa vya kusaidia watoto njiti kwenye hospitali ya KCMC iliyopo Moshi, Kilimanjaro.”