WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ubora wa ujenzi wa kituo cha forodha cha Sirari kilichopo kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya.
Kufuatia hali hiyo amemtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) afike ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma akiwa na mkandarasi aliyejenga kituo hicho.
“Serikali haiwezi kuvumilia ujenzi wa hovyo kiasi hiki, namtaka Kamishna wa TRA aje ofisini kwangu Januari 25, 2018 pamoja na mkandarasi aliyejenga kituo hiki akiwa na nyaraka zote za ujenzi wa jengo hilo.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Januari 17, 2018) mara baada ya kumaliza kukagua kituo hicho kilichopo wilayani Tarime, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mara.
Waziri Mkuu amesema hajaridhishwa na ujenzi huo kwa kuwa upo chini ya kiwango. Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2011 na kukamilika mwaka 2014.
Waziri Mkuu amejionea mwenyewe kuta za jengo hilo zikiwa na nyufa nyingi kuanzia ukutani hadi sakafuni na pia rangi za baadhi ya kuta zikiwa zimebanduka.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi wa wilaya hiyo kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa kuzingatia sheria na wajiepusha na biashara za magendo.
Waziri Mkuu amesema magendo yanaikosesha Serikali mapato, hivyo bidhaa yoyote itakayokamatwa ikiingizwa nchini kwa njia za magendo itataifishwa pamoja na chombo cha usafiri kilichotumika.
Pia Waziri Mkuu ametembelea shule ya Sekondari ya Wasichana ya Borega, ambapo amewasisiza wananchi wasimamie elimu ya watoto wa kike ili wafikie malengo yao.
Amesema Serikali imeweka sheria kali kwa yeyote atakayekatisha masomo kwa watoto wa kike iwe kwa kumpa ujauzito au kumoa, adhabu yake ni kifungo cha miaka 30 jela.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wanafunzi hao wasome kwa bidii ili waweze kutimiza ndoto zao na kamwe wasijihusishe katika mambo ambayo hayahusiani na masomo.