WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kwa kujenga miundombinu na kuongeza bajeti.
Aidha amezielekeza Halmashauri zote nchini kuweka mpango mahsusi wa ardhi kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji.
Majaliwa aliyasema hayo jijini hapa jana, wakati wa hafla ya utiaji saini wa mikataba ya ujenzi na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi ya umwagiliaji.
Alisema bajeti katika sekta ya umwagiliaji imeongezeka kwa asilimia 677 hadi kufikia sh. bilioni 361.5 mwaka 2023/2024 kutoka sh. bilioni 46.5 iliyotengwa kwa mwaka 2021/2022.
“Nitumie fursa hii kumpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji wa miradi ya umwagiliaji nchini,”alisema
Aliongeza kuwa:“Matarajio ya serikali ni kuona miradi inayotekelezwa itakamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa ili kuwezesha kutimia kwa azma ya Serikali ya kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika Pato la Taifa kutoka wastani wa asilimia 26 hadi asilimia 50 ifikapo mwaka 2030,”alifafanua.
Majaliwa aliwasisitiza Watendaji wote wanaohusika katika utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji wafanye kazi kwa ufanisi na wazingatie suala la uwazi pamoja na usimamizi mzuri wa fedha.
Alisisitiza kuwa fedha hizo ni kodi za wananchi wa Tanzania hivyo basi zitumike kuwanufaisha Watanzania wote.
“Wasimamizi wa miradi wahakikishe kuwa ubora wa miradi unalingana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa kwenye miradi hiyo,”alisema.
Aliongeza kuwa:”Wakandarasi na Wasimamizi wa miradi inayotekelezwa kwa force account, wahakikishe wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi walioko katika maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa na wahakikishe miradi inakamilika kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano yaliyopo,”.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema mikakati ya serikali ni kuanza kutumia maji ya ziwa Tanganyika katika miradi ya kilimo cha umwagiliaji ambapo hatua ya kwanza itaanza katika Mikoa ya katavi na Rukwa.
Alisema baada ya Bunge la bajeti kumalizika kutafanyika upembuzi wa kina na yakinifu ili maji hayo yasafirishwe hadi Simiyu ambapo kuna ukame na Tabora.
“Baada ya Bunge la bajeti kukamilika tunatarajia kuanza kuyatumia maji ya ziwa Tanganyika katika shughuli za kilimo na uzuri mitambo tunayo naamini Jambo hili litafanikiwa,”alisema
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Raymond Mndolwa alisema hafla hiyo ni kwa ajili ya utiaji sahihi wa mikataba 24 ambayo kati yake 14 ya ujenzi kwa kutumia wakandarasi yenye thamani ya sh. bilioni 248.7, miradi sita ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kutumia Washauri Elekezi yenye thamani ya sh. bilioni 9.35.
Alitaja miradi mingine minne itatekelezwa kwa kutumia wataalam wa ndani kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji yenye thamani ya sh.bilioni 16.95 ambayo itatekelezwa kwa utaratibu wa Force Account.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alisema serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia ametoa fedha zaidi ya sh.bilioni 67 kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji ambayo yatahudumia ekari zaidi ya 35,000.
“Mabwawa haya ni muhimu kwa Mkoa wa Dodoma kwasababu asilimia 72 ya wananchi wanaishi kwa kutegemea kilimo hivyo yataenda kufanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo na kuinua pato la Taifa na mwananchi mmoja mmoja,”alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa amesema miradi mingi ya Umwagiliaji inatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, hivyo kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa skimu zinazoendelea kujengwa katika kipindi cha mwaka 2022/2023 – 2023/2024 kutaongeza eneo la Umwagiliaji kufikia Hekta 983,465.46 sawa na asilimia 81.9 na kufanya eneo la Umwagiliaji kufikia Hekta 1,200,000 ifikapo mwaka 2025 ambapo pia kutaongeza ajira 1,352,127.