Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Sekta ya madini ni nguzo muhimu katika uchumi wa Nchi, hivyo serikali itaendelea kuifungamanisha na sekta nyingine ikiwemo sekta ya viwanda kwa kuwakaribisha wawekezaji kuwekeza katika viwanda na hatimaye kukuza uchumi na kuleta Maendeleo.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini Tanzania, unaofanyika katika Kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuweza kusaidia shughuli za uongezaji thamani madini inaendelea kufanyika hapa nchini.

“Sekta ya madini nchini imekuwa hivyo serikali inaendelea kuboresha mazingira kwa wachimbaji wadogo ili ifikapo 2030 wachimbaji hao wawe wachimbaji wa kati ili waendelee kuchochea uchumi na kuchangia kwenye pato la taifa,” amesema.

Ameongeza kuwa wizara ya madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kufanya Utafiti katika maeneo mbalimbali nchini ili kubaini fursa za uwepo wa Madini yatakayotumika kwenye shughuli mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa mbolea katika sekta ya KILIMO na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo za urembo.

Aidha Majaliwa ametoa wito kwa m
wadau wa sekta ya madini kuhakikisha wanatumia Teknolojia rafiki kwa Mazingira ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa sehemu ya juhudi za mapambano ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi na si kuchangia uharibifu wa Mazingira.

Pia ameagiza idara ya Mazingira kushirikiana na wizara ya madini ili kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji madini haziathiri Mazingira.

“Tanzania inamadini muhimu yanayochimbwa katika maeneo mbalimbali hivyo suala la utunzaji Mazingira ni lazima lizingatiwe. Hivyo wadau wote wa sekta ya madini Wana wajibu wa kuzingatia miongozo ya Mazingira katika utekelezaji wa shughuli za uchimbaji madini ili kulinda Mazingira,” amesisisitiza.

Awali Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema mafanikio katika sekta ya madini yametokana na uongozi bora wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na kuwajali wachimbaji wote wadogo, wakati na wakubwa lakini pia kuongeza bajeti kutoka bilioni 89 mpaka bilioni 231.

“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawajali sana wachimbaji na ameelekeza mashine mbili za uchorongaji zipelekwe kwa wakinamama wachimbaji,” amesema Mavunde.

Amesema Serikali tayari imeshatunga sera ya kuongeza thamani madini ili kusaidia vijana wengi nchini kupata ajira lakini pia kukuza na kuongeza pato la Taifa.