Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha mifumo na miuondombinu ya mifumo ili kuboresha ufanisi wa utoaji huduma, utendaji kazi na kupunguza urasimu unaokwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.

Ameyasema hayo jana usiku (Jumatatu, Septemba 25, 2023) wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji Mahali Pamoja; Mwongozo wa Kuwasajili Watoa Huduma za Ushauri kwa Wawekezaji pamoja na Kampeni ya Uhamasishaji Uwekezaji kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu Kassim akikagua mabanda, kwenye Uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa kuhudumia Wawekezaji, Mwongozo wa Usajili kwa Watoa Huduma za Ushauri kwa Wawekezaji (TeIW – Tanzania Electronic Investment Widow) katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.  jijini Dar es Salaam Septemba 26, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

“Kituo cha uwekezaji kimekuwa kikifanya maboresho mbalimbali ili kuongeza kasi ya kutoa huduma. Matokeo ya jitihada zote hizo za kuongeza ufanisi ni pamoja na kuanza kutumika kwa mfumo wa kuhudumia wawekezaji mahali pamoja (Tanzania Electronic Investment Window-TeIW),” amesema.

Amesema kuanza kutumika kwa mfumo huo ni matokeo ya utekelezaji wa mpango wa maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji nchini unaojumuisha maboresho ya sheria, sera na mifumo ya utendaji kazi katika kuhamasisha uwekezaji.

Alisema Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimeandaa mwongozo mahsusi wa kusajili Watoa Huduma za Ushauri kwa Wawekezaji ambao umeorodhesha aina za huduma zinatozotolewa na watoa huduma kwa wawekezaji, vigezo vya kuwa mtoa huduma kwa wawekezaji, utaratibu wa kuwasilisha maombi ya kuwa mtoa huduma kwa wawekezaji, mafunzo kwa watoa huduma na ufuatiliaji na tathmini ya watoa huduma hao.

Amesema mwongozo huo umeandaliwa ili kusaidia wawekezaji kufikia malengo yao ya kusajili miradi kituoni hapo na kupata vibali vingine kutoka taasisi, idara na Wakala wa Serikali (MDAs) zilizopo katika eneo la mahali pamoja la utoaji huduma (One Stop Facilitation Centre) kulingana na matakwa ya sheria zinazosimamia utoaji wa vibali na leseni husika.

“Ninawapongeza TIC kwa maono ya kuwa na mwongozo mzuri wa kusajili Watoa Huduma za Ushauri kwa Wawekezaji (Investors’ Service Providers). Naamini mwongozo huu utarahisisha upatikanaji wa vibali kwenye taasisi zilizopo katika eneo la huduma na kuwezesha wawekezaji kufikia malengo yao ya kusajili miradi katika Kituo cha Uwekezaji.”

Aliwapongeza kwa kuanzisha kampeni ya kuhamasisha uwekezaji Tanzania inayolenga kuvutia uwekezaji nchini hadi kufikia dola za Kimarekani bilioni 10 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030. “Haya ni maono makubwa, yanahitaji mikakati madhubuti ili kuyafanikisha,” amesisitiza.

“Nimeelezwa kuwa matokeo ya kuimarika kwa mifumo ya utoaji huduma katika kipindi cha mwezi mmoja tu, yameongeza idadi ya miradi inayosajiliwa kutoka 25 mwezi Aprili, 2023 na kufikia miradi 52 mwezi Mei, 2023.

Waziri Mkuu alisema kutokana na mafanikio yaliyopatikana ndani ya muda mfupi, ana imani mfumo huo umesaidia kupunguza mlolongo wa maombi kupitia mifumo mbalimbali na kuwezesha upatikanaji wa huduma kwenye dirisha la mahali pamoja kwa njia ya mtandao bila kufika TIC; kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuwezesha utoaji wa huduma kwa weledi.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na walioshiriki uzinduzi huo, Waziri wa Nchi (OR- Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo alisema kutungwa kwa sheria mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022, kumefanikisha utoaji wa vivutio maalum kwa wawekezaji mahiri maalum (special strategic investors).

“Tangu kupitishwa kwa sheria hiyo, tumeweza kutoa vivutio kwenye miradi mikubwa 16 ambayo inaendelea vizuri kikiwemo kiwanda cha kutengeneza vioo cha Mkuranga ambacho kilizinduliwa hivi majuzi na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Waziri Mkuu Kassim akizungumza kwenye Uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa kuhudumia Wawekezaji, Mwongozo wa Usajili kwa Watoa Huduma za Ushauri kwa Wawekezaji (TeIW – Tanzania Electronic Investment Widow) katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.  jijini Dar es Salaam Septemba 26, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Naye Mkurugenzi Mkazi wa Trade Mark Africa, Bi. Monica Hangi alisema amefurahi kushuhudia uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Kuhudumia Wawekezaji kwani anaamini utasaidia kupunguza siku za maombi ya wawekezaji ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali.

“Miaka miwili iliyopita, tulikuwa na mwekezaji ambaye alihitaji kutembea kwenye taasisi 12 ili apate vibali anavyostahili na aweze kuwekeza ndani ya nchi. Pia alihitaji kujaza fomu zaidi ya 50 kwa mkono, na akikosea kidogo anaanza upya. Hii ilikuwa inapoteza fursa nyingi na ilichosha wawekezaji.”

“Lakini leo ninayo furaha kubwa kuona kwamba tumepata mfumo unaoweza kupunguza siku na tunatarajia kwa kupunguza siku, tunaweza kuvutia wawekezaji wengi katika nchi yetu. Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali na taasisi za Serikali kuboresha huduma kwa wawekezaji. Ninawapongeza sana TIC kwa hatua hii,” alisema.

Waziri Mkuu Kassim, akikabidhiwa tuzo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Nchi (OR- Mipango na Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, wakati alipokagua mabanda, kwenye Uzinduzi wa Mfumo wa Kielektroniki wa kuhudumia Wawekezaji, Mwongozo wa Usajili kwa Watoa Huduma za Ushauri kwa Wawekezaji (TeIW – Tanzania Electronic Investment Widow) katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.  jijini Dar es Salaam Septemba 26, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)