Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Mafia
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ,ametoa agizo kwa wakuu wa wilaya nchini kuhakikisha wanashirikiana na mamlaka ya mapato (TRA) kusimamia na kufanya ukaguzi wa mashine za EFD endapo ni halisi na sio za maghumashi ili kuepusha upotevu wa mapato kwa Serikali na kuondoa kero kwa jamii.
Aidha ameiagiza wilaya ya Mafia na mkoa wa Pwani kuendelea na kuhamasisha wawekezaji kuwekeza katika uchumi wa bluu kisiwa cha Mafia ili kujiongezea mapato na uchumi.
Akifunga wiki ya Utalii na Uchumi wa bluu kisiwa cha Mafia, yaliyofanyika siku tatu, Majaliwa alielekeza wakuu wa wilaya pia kusimamia na kuimarisha mabaraza ya biashara kwenye maeneo yao ili suala la biashara lilete tija kwa wafanyabiashara na kupata faida.
“Hivi karibuni kumekuwa na changamoto za mitambo isiyo halali, hakikisheni kila unapokwenda kununua bidhaa mnakabidhiwa risiti Tena zilizo halali,
“Nyie wakuu wa wilaya ni wenyeviti wa mabaraza haya ,kaeni kwenye vikao vya mapato kwenye maeneo yenu, fanyeni ukaguzi ili kubaini kama mitambo ya EFD ni halisi ambazo sio za maghumashi kwani zinapoteza mapato ya Serikali na kuleta usumbufu kwa wananchi”.
Alitaka waendelee kusimamia Sera na sheria za nchi ili kusiwe na kero kwa wafanyabiashara na wananchi.
Majaliwa aliwaasa na wananchi kujenga tabia ya kufanya utalii wa ndani kwani Serikali imepunguza gharama za utalii kwa wazawa.
Vilevile Waziri Mkuu ,ameutaka mkoa na wilaya kusaidia vijana na wajasiriamali kupata mafunzo ya biashara,ikiwemo namna ya kupata mikopo, kuendesha biashara zao ili waweze kuendesha biashara zao.
Akizungumzia tamasha na wiki ya utalii, Majaliwa anasema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga na bahari,Kisiwa cha Mafia Mkoani Pwani,ambapo imetenga Bilioni 9.5 ya kutengeneza kivuko kipya ,chenye uwezo wa kubeba mizigo ya tani 120 pamoja na abiria 500 kwa wakati mmoja.
Alieleza kwasasa mchakato wa ununuzi wa vifaa vya ujenzi unaendelea ili kazi ianze mara moja.
Majaliwa aliitaka wilaya na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kusimamia ujenzi na utengenezaji wa kivuko hicho kikamilike kwa wakati.
Katika kuinua uchumi wa Mafia Serikali inaboresha uwanja wa ndege Mafia kwa kuongeza mataa ili usafiri kuwa wa uhakika wakati wowote na kuongeza jengo la abiria liweze kufikia 200 kwa wakati mmoja .
Wakati huo huo, wanaendelea kupeleka Umeme wa Gridi ya Taifa kuanzia Nyamisati hadi Kilindoni na sasa ipo mbioni kumaliza changamoto ya umeme kuwa wa uhakika ambapo kati ya vijiji vya mkoa wa Pwani bado vijiji 13 ambavyo bado havina Umeme kati ya hivyo vitatu vipo Mafia.
Akizungumzia sekta ya kilimo amehimiza kilimo cha Mwani ,korosho na kuwaasa wananchi kisiwani humo kujikita na kilimo hicho na shughuli za uvuvi ambavyo vina tija katika masoko.
Sanjali na hayo, Majaliwa aliwataka vijana kuchangamkia fursa za kibishara ,kuendesha mahotel ya utalii na watalii sambamba na kujifunza lugha za kigeni ili kujipatia ajira.
Aliupongeza mkoa na wilaya kwa kufanikisha tamasha hilo na kutangaza vivutio vya Mafia na kuwashauri lisiishie hewani liwe endelevu kwa kila mwezi septemba ya kila mwaka.
Majaliwa alieleza, Mafia ni kisiwa ambacho kinasifika kwa mazalia ya samaki Duniani, kisiwa hiki kinachangia pato kubwa kupitia Uchumi wa bluu na Uvuvi.
Alifafanua kwa kipindi Cha mwaka 2020/2023 Mafia imeongeza watalii na kufikia 14,153 na mapato yatokanayo na utalii Bilioni 2.7 ,na kusema hili ni ongezeko kubwa.
“Ongezeko hili ni kubwa ,na ni matunda mazuri ya kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan katika Royal Tour, tumieni fursa hii tangazeni fursa zenu kupitia mifumo ya matangazo, na mchangamkie fursa za kufanya biashara”
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi , Alexander Mnyeti ,alisema wizara hiyo inaunga mkono juhudi za wilaya ya Mafia na mkoa kwani wanachagiza ukuaji wa uchumi wa bluu na sekta ya utalii.
Awali mbunge wa jimbo la Mafia Omary Kipanga aliishukuru Serikali kwa kipindi Cha miaka miwili na miezi nane imepeleka bilioni 45 kwa ajili ya miradi ya maendeleo Mafia.
Ameomba Rais afike Mafia kwani ni kilio na kiu ya wananchi hao .
Mkuu wa mkoa wa Pwani Alhaj Abubakari Kunenge, alieleza, tamasha hilo ni la siku tatu ,lilianza September 28 na tamati 30 ambapo washiriki walikuwa 71.
“Hili tunalofanya ni kutafsir kwa vitendo azma ya Rais kufungua wilaya ya Mafia katika uwekezaji wa uchumi wa bluu na utalii na tu kwa hili, Imani yetu mwaka mmoja matokeo chanya yataonekana “anasema Kunenge.