Na Daniel Limbe, JamhuriMwsia,Chato
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Kassim Majaliwa, amewataka wakazi wa mkoa wa Geita kujikita kwenye sekta ya uvuvi ili kuongeza ajira na kuinua vipato vyao.
Aidha amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejikita kusogeza karibu miradi ya maendeleo ili kuwapa fursa za kiuchumi wananchi wake huku akiwasisitizia kufanya kazi kwa bidii.
Alikuwa kwenye uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi mkubwa wa kisasa wa soko la samaki lilipo wilayani Chato mkoani humo.
Hata hivyo amedai kukamilika kwa ujenzi wa soko hilo utasaidia kuinua uchumi wa wananchi,wilaya na taifa kwa ujumla na kwamba wafanyabishara kutoka nchi za Kongo na Burundi wanatarajiwa kutumia soko hilo kununua mazao ya samaki.
Na kwamba hatua hiyo itaimarisha mahusiano ya nchi wanachama wa Afrika mashariki lengo likiwa ni kuinua uchumi wa wananchi na kupunguza umaskini wa vipato.
Awali msimamizi mkuu wa mradi wa ujenzi wa soko hilo,mhandisi George Kwandu,akizungumza kwa niaba ya Katibu mkuu wa wizara ya Mifugo na Uvuvi,amesema miradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2024.
Kwamba soko hilo litahusisha ufungaji wa mitambo ya kukausha samaki na jengo la uzalishaji barafu ambayo pia itauzwa kwa wavuvi wengine wanaojihusisha na uongezaji thamani ya mazao vya uvuvi.
Kadhalika Kwandu amesema, soko hilo litakuwa na uwezo wa kukausha tani 10 za samaki aina ya dagaa na samaki wengine kuhifadhiwa kwa zaidi ya saa 240 pasipo kuharibika.