Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameunda tume ya watu 14 ambayo itachakata kero na mapendekezo ya wafanya biashara wa soko la kimataifa la Kariakoo.
Ameunda tume hiyo leo Jumatano (Mei 17, 2023) wakati alipozungumza na wafanya biashara wa soko hilo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam. Tume hiyo ambayo imepewa siku 14 kuja na mapedekezo ya kutatua changamoto za wafanyabiashara, itakuwa na watendaji saba kutoka Serikalini na saba kutoka Jumuiya ya wafanyabiashara.
Kwa upande wa Serikali, Waziri Mkuu amewataja Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Katibu Mkuu Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna wa Kodi za Ndani wa TRA, Kamishna wa Sera wa TRA.
Kwa Upande wa Wafanyabiashara ni Mwenyekiti wa Taifa wa wafanyabiashara, Mwenyekiti wa wafanyabiashara Kariakoo, na Wafanyabiashara wengine ni Ismail Masoud Kutoka Tanga, Fred Ngajiro (Vunja Bei) Awadh Mpandira, Salome Mgaya (Mama Bonge), na Omari Hussein kutoka Zanzibar.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anathamini sekta ya biashara na ameagiza kufanya maboresho kuanzia wafanyabiashara wadogo hadi wakubwa ili kukuza sekta hiyo.
“Serikali yetu ya awamu ya sita chini ya Rais wetu, itaendelea kuimarisha biashara zenu, kilio chenu tumekisikia, na ndiyo maana nimerudi tena kwa maelekezo ya Rais wetu, naomba muone nia ya dhati ya Serikali yenu kwamba mfanye biashara zenu na mpate mafanikio”.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ameiagiza kamati aliyounda kufanya mapitio ya madai ya wafanya biashara ambao mizigo yao imekamatwa na kuwasilisha mapendekezo kwa Kamishna wa TRA ili waone uwezekano wa kuiachia kwa kutengeneza unafuu kwa wafanyabiashara.
“Kamishna wa TRA, mizigo imekaa sana na mingine imeshuka thamani, uking’ang’ania ulipwe kodi ile ile hutapata chochote itaharibika, kaangalie utaratibu mwingine nafuu.”
Akihitimisha mazungumzo na wafanyabiashara hao, Mheshimiwa Majaliwa amewasihi wafanyabiashara hao kuendelea na biashara zao.
“Nawasihi mrudi kazini ili mkafanye biashara, kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan naomba mridhie kufungua maduka ili tunusuru soko la kimataifa liendelee kuwa na heshima yake.”