Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametembelea kiwanda cha kutengeneza dawa za binadamu cha Cure Afya kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kushuhudia uzalishaji wa dawa kwenye kiwanda hicho chenye thamani ya takribani shilingi bilioni 50, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuhakikisha wawekezaji wanapata faida kutokana na shughuli zao.

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya utoleaji huduma za afya nchini, na sasa tunahitaji kupata dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuendelea kuongeza nguvu kwenye utoaji huduma, hivyo uwekezaji huu una tija kwa Taifa letu,” amesema.

Kadhalika, Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji hao kuendelea kutengeneza dawa zilizo katika ubora unaokubalika katika viwango vya kimataifa kwenye utoaji wa huduma za tiba.

Waziri Mkuu Majaliwa amewataka watumishi wa kiwanda hicho kufanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na weledi ili kumsaidia mwekezaji huyo kupata faida kutokana na uwekezaji wake.

Katika hatua nyingine, Majaliwa ametembelea eneo la Dege, Wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam kukagua utekelezaji wa agizo alilolitoa la uwekaji wa taa za barabarani wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani humo Oktoba.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni Erasto Kiwale amesema kuwa mpaka sasa taa 67 zimeshawekwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kazi inaendelea.