Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

WAZIRI Mkuu Kassimu Majaliwa ameridhishwa na maendeleo ya maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa katika uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.

Akikagua katika ziara yake ya siku moja maendeleo ya maandalizi hayo, ametoa maagizo ya kufanya maboresho kwenye maeneo ya uwanja utakapofanyika uzinduzi huo.

“Sina mashaka na maandalizi nategemea mbio za Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu kuwa bora kuliko mwaka jana na hii imetokana na ushirikiano wa viongozi ,”ameeleza.

Majaliwa amepongeza sekretarieti ya Mkoa wa Pwani na Wilaya kwa maandalizi waliyoyafanya ambayo yamefanya kusimamisha baadhi ya shughuli zao.

Amesema maboresho ya uwanja huo yaliyofanyika yameimarisha uwanja huo ambao hata mechi za ligi kuu zinaweza kufanyika hapo.

” Pia kwakua Tanzania tumepewa heshima ya kucheza mashindano ya CHAN Afrika ambayo yatafanyiika hapa mwezi wa nane na mahitaji ya viwanja ni mengi tutakuja kukagua hapa na CAF wakiridhika watatupa kibali kutumia kiwanja hiki,”

Vilevile Majaliwa amewataka wananchi kutoka maeneo mbalimbali kujitokeza kushiriki uzinduzi wa mbio hizo za Mwenge wa Uhuru kitaifa kuungana na Viongozi wa Wilaya na kitaifa watakaohudhuria.

Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete alisema upande wa maandalizi wanaenda vizuri ikiwemo kukamilisha maeneo ya uwanja huo.

Amesema kwenye miundombinu pia maboresho yamefanyika na vijana wa halaiki wameandaliwa vizuri na kwamba wako tayari kushiriki tukio hilo la uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru.

Ridhiwani amesema wageni pamoja na wananchi zaidi ya 22,000 wanatarajiwa kushiriki uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa utakaofanyika April 2 katika uwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.