Na OWM Milan Italia.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara wa nchini Italia kuja Tanzania kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali kwa kuwa Tanzania ina malighafi za kutosha pamoja na uwepo wa masoko ya uhakika kutokana na eneo la kijiografia.
Ameyasema hayo leo Oktoba 19, 2023 wakati akizungumza katika Jukwaa la Tatu la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Italia lilifanyika Palazzo Regione Lombardia, Milan nchini Italia. Waziri Mkuu yuko nchini Italia akimuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani ulioanza Oktoba 16 hadi Oktoba 20, 2023, Rome nchini Italia.
“Msisitizo wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mkakati wa Serikali ni kuwahamasisha wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa mbalimbali nchini waje kuwekeza katika ujenzi na kuzalisha bidhaa hizo nchini ili zipatikane kwa wingi na kwa urahisi.”Amesema Waziri Mkuu Majliwa.
Majaliwa ametaja baadhi ya maeneo ambayo wawekezaji hao wanaweza kuja kuwekeza katika sekta za madini, kilimo, mawasiliano, mifugo, uvuvi, utalii na afya hivyo amewakaribisha wafanyabiashara hao na wawekezaji watumie fursa hiyo na kuwekeza nchini.
Majaliwa amesema kwa sasa Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa, barabara, viwanja vya ndege na nishati ya uhakika ili kurahisisha shughuli mbalimbali zikiwemo za uwekezaji.
Taasisi hizo ni pamoja Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) ambao viongozi wake walipata fursa ya kutaja fursa za uwekezaji zilizopo nchini pamoja na namna ya kuwawezesha kuyafikia maeneo hayo.