Maisha ni mtihani, uufanye
Ili mwanafunzi apande darasa kuna mtihani ambao atapewa ili aufanye, anaposhinda mtihani huo ndipo anapopata nafasi ya kupanda darasa, akishindwa anarudia darasa. Maisha vilevile yanatupa mitihani ambayo hatuna budi kuifanya. Anayekwepa mtihani wake hawezi kusonga mbele, maana yake anabaki pale alipo.
Kuna aliyewahi kusema, usiache kujifunza, maana maisha hayajawahi kuacha kufundisha, kwa maana hiyo maisha yanatupa mtihani ambao lazima tuufanye.
Kila hatua mpya inahitaji wewe mpya, namna yako ya kufikiri iwe mpya, mtazamo wako uwe mpya, utendaji wako uwe mpya, muda mwingine hata mtandao (watu) wako uwe mpya. Kwa namna hiyo, unaweza kuishinda mitihani ya maisha.
Kama ilivyo kwa mwanafunzi, kabla ya kuingia kwenye chumba cha mitihani lazima ajiandae, maisha yenye mitihani yanahitaji maandalizi makali. “Nipe saa 6 kukata mti, nitatumia saa nne, kunoa shoka,” alisema Abraham Lincoln. Huyu anatukumbusha umuhimu wa maandalizi.
Mtihani mkubwa aliokuwa nao Daudi ni kupambana na Goliathi pande la mtu. Ndugu zake waliona Goliathi ni pande la mtu na wakasema Daudi hawezi kupambana naye. Yeye Daudi aliona Goliathi ni mnene kiasi kwamba hawezi kukosa kumpiga.
Lakini tukumbuke kwamba Daudi alikuwa akirusha mawe enzi hizo akichunga kondoo wa baba yake. Hizo zilikuwa nyakati za maandalizi. Baadaye anakuja kumpiga Goliathi kwa staili yake ya kurusha mawe kwa kutumia kombeo. Anashinda anayejiandaa.
Kuna wanaosema “Jambo hili haliwezi kufanyika” na wengine wanaosema “Linaweza kufanyika.” Hao wa kwanza kuna namna fulani wanakwepa majukumu yao, watu wa pili wanafahamu wazi kwamba maisha yana mitihani inayopaswa kufanyika.
Watu wengi tunaowafahamu kuwa mashuhuri katika dunia hii ni watu waliopitia mitihani mingi lakini waliifanya na kuifaulu. “Mafanikio yoyote yanaambatana na mitihani. Mambo tusiyoyatarajia huja ghafla kwenye mambo tuliyoyajenga kwa miaka mingi. Kama tusipojenga kama yule mtu aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba imara, kazi zetu zitaharibika,” anasema Askofu Duncan Williams.
Mwamba imara anaouzungumzia Duncan Williams unatokana na mfano aliowahi kuutoa Yesu akielezea juu ya watu wawili waliojenga nyumba. Mmoja alijenga kwenye mwamba mgumu, mwingine akajenga kwenye mchanga. Wote wakamaliza ujenzi. Ipo wazi, wote walionekana kuwa bora. Nyumba zote zilionekana bora mpaka pale majaribio yalipokuja. Biblia inasema:
“Mvua zikashuka na mafuriko yakaja, na upepo ukavuma na kupiga kwenye zile nyumba.
Nyumba zote ziliwekwa kwenye majaribio makubwa.
Nyumba iliyokuwa imejengwa kwenye mwamba haikuanguka kwa sababu ilijengwa kwenye mwamba. Nyumba iliyojengwa kwenye mchanga ilianguka. Hebu tukae chini na kulipembua jambo hili kwa kina. Yule mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba inawezekana alikuwa na
spidi ndogo. Alihitaji kufanya kazi kwa bidii zote. Alihitaji kutumia pesa kupasua miamba kwenye baadhi ya maeneo ili kutengeneza njia ya msingi. Mtu ambaye anahitaji kujenga juu ya mwamba pia anahitaji ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mhandisi na msanifu majengo. Maisha hayana njia ya mkato.
Abraham Lincoln ni mmojawapo wa watu mashuhuri waliowahi kuishi katika dunia hii. Huyu alikuwa rais wa 16 wa Marekani. Kabla ya kuwa kiongozi wa nafasi hiyo ya juu, kuna mitihani
mingi aliipitia, kuna gharama nyingi alizilipa.
Akiwa na miaka 22, alianzisha biashara na ikafa. Akiwa na miaka 23, aligombea ubunge na akashindwa. Miaka miwili baada ya kushindwa kuanzisha biashara alianzisha biashara nyingine nayo ikashindwa pia. Hayo hayakuwa mawe ya kumaliza nia yake ya kufanikiwa. Akiwa na miaka 25, miaka miwili baada ya kugombea ubunge, aligombea ubunge na kushinda. Akiwa na miaka 26 pale ambapo taa ya kijani ilianza kumuwakia, alimpoteza mke wake ambaye wangeshirikishana matunda ya ubunge. Akiwa na miaka 27 alivunjika neva.
Akiwa na miaka 33, aligombea kuingia kwenye ‘congress’ na kushindwa. Miaka mitatu baadaye aligombea tena na kushinda. Miaka miwili baadaye kulikuwa na uchaguzi wa congress, aligombea na hakushinda. Akiwa na miaka 46 aligombea kuwa seneta na kushindwa. Mwaka uliofuata aligombea umakamu wa rais na kushindwa. Akiwa na miaka 51 alikuwa rais.
Kwenye maisha utakutana na mitihani. Kama ukijaribu na kushindwa, huo si mwisho wa dunia.
Hauwezi kujua kile unachoweza mpaka ujaribu, kama mwanzo haukufaulu, jaribu, jaribu na jaribu tena.