Maisha ni malengo. Hakuna maisha ya mkato. Ishi kwa malengo. Tusiishi kwa sababu tunaishi. Tuishi kwa malengo, kwa sababu Mungu ametuumba tuishi kwa malengo. Ungana na Henry James kuamini maneno haya; “Ni muda mwafaka wa kuishi maisha ambayo umeyafikiria kwa muda mrefu.’’

Binadamu wengi wanaishi ni kwa sababu wanaishi. Hawaishi kwa malengo. Tunaishi maisha yasiyo na utafiti. Tunapenda majibu mepesi kwa maswali magumu. Karne ya 21 siyo karne ya kutafuta miujiza makanisani. Siyo karne ya kutafuta ushirikina kwa waganga wa kienyeji ili kutajirika.

Si karne ya ubabe wa kimadaraka. Si karne ya wizi wa mali za umma. Si karne ya dharau na kebehi. Hii ni karne ya utafiti, ugunduzi na ushindani katika nyanja zote zinazomhusu binadamu kama vile teknolojia inayoendana na wakati na tafiti mbalimbali za kisomi. Kupanga ni kuchagua. Mwanafalsafa Benjamin Franklin anasema, “Ukishindwa kujiandaa, umejiandaa kushindwa.”

Hakuna anayepanga kushindwa ila wengi wanashindwa kupanga. Mwandishi Vicent Lombardi anasema, “Kila mtu anapenda kufanikiwa ila ni wachache wanaopenda kujiandaa kufanikiwa’’. Mantiki inatunong’oneza ukweli kwamba fikra zilizotufikisha katika mazingira tuliyomo kwa sasa na hali tuliyonayo leo, fikra hizo kwa uhalisia wake hazitaweza kututoa kwenye matatizo tuliyonayo kwa sasa.

Ukweli wa niyasemayo hapo juu alipata kuusema mwanafizikia wa Kijerumani, Albert Einstein [1879-1955], kwa maneno haya, “Hatuwezi kutatua matatizo kwa kutumia namna ile ile ya kufikiri tuliyotumia katika kuyaanzisha matatizo’’. Tunahitaji fikra tofouti. Tunahitaji fikra mbadala. Yatufaa kubadili gea sasa ili tuweze kuupanda mlima wa mafanikio kwa usalama, uhakika na weledi. Gea hiyo ni kuanza kuishi maisha kwa malengo.

Kuna methali ya Kifaransa inayosema hivi; “Yeye anayengoja kuvaa viatu vya marehemu anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu’’. 

Watanzania tusisubiri viatu vya marehemu. Kusubiri maendeleo yatokee pasipo kufanya kazi kwa bidii ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu. Kulalamika kwa kila jambo pasipo kubuni mbinu na mikakati ya kukuinua kiroho, kimaadili, kisiasa, kiafya na kiuchumi ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu.

Kukaa na ukimsubiri mwanaume mwenye pesa ajitokeze kukuoa ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu. Methali ya Kiswahili inaupambanua ukweli huo kwa maneno haya, “Mtegemea cha ndugu hufa maskini.’’ Mtu anayeweza kukuokoa wewe ni wewe. Ni wewe unayeweza kujiandikia historia nzuri au mbaya. Ni wewe unayeweza kuwa chachu ya mabadiliko au mhanga wa mabadiliko. Ishi kadri ya uwezo wako, usiishi kama watu wengine wanavyotaka uishi. Methali ya Kiswahili inatukumbusha maneno haya, “Miluzi mingi humpoteza mbwa’’.

Watu wengi walioshindwa kufanikiwa kimaisha, kiroho, kimaadili ni wale walioishi kadri ya watu walivyowapendekezea waishi. Usijaribu kuishi kwa kumfurahisha mwanadamu, ishi kwa kumfurahisha Mungu. Ukiishi kwa kumfurahisha mwanadamu, ipo siku huyo mwanadamu uliyeishi kwa kumfurahisha atakusaliti. Mhubiri wa Injili, Israel Ayivor, alipata kusema, “Yule aliyekusaidia kuzungumza mambo mabaya kuhusu mwenzako, ndiye atakayemsaidia mtu mwingine kuzungumza uovu juu yako’’. 

Maneno haya yana ukweli ndani yake. Yapo na si kwamba hayapo. Maisha hayaongozwi kwa mihemko na papara zisizo na dira. Maisha hayaongozwi kwa dhuluma. Maisha yanaongozwa kwa hekima, busara, maono na jitihada binafsi.

Huwezi ukawa kama unavyotaka uwe kama hujawa na dhamira ya dhati ya kubadilika. George Benerd Shaw alipata kuandika haya, “Maendeleo hayawezekani bila mabadiliko ya fikra na wale ambao hawawezi kubadilika namna wanavyofikiri hawawezi kubadili chochote”. Stephen Richards anaamini kwamba “Namna yetu ya kufikiri inatengeneza matokeo mazuri au mabaya’’.

Ukosefu wa fikra sahihi na bainifu kwa maisha ya mwanadamu yeyote yule ni ugonjwa. Ni ugonjwa usioonekana kwa vipimo vya kisayansi lakini ni ugonjwa unaoua kwa haraka sana kuliko magonjwa mengine. Ni ugonjwa unaoonekana kwa vitendo na kwa uamuzi mbalimbali wa mhusika. Fikra sahihi zinaishi. Badilika kwanza. Badili mtazamo wako katika kufikiri. Badili mtazamo wako kwa kuupenda ukweli ulivyo na uhalisia wake. Badili mtazamo wako kwa kusoma tafiti za wasomi mbalimbali, vitabu, magazeti, na majarida mbalimbali. Lisilowezekana linawezekana kwa kubadili namna ya kufikiri. Maisha ni malengo. Baba wa kiroho, Sai Baba, alipata kuyatafsiri maisha kwa namna hii:

“Maisha ni wimbo, uimbe,

Maisha ni mchezo, ucheze,

Maisha ni changamoto, ikabili,

Maisha ni ndoto, ielewe,

Maisha ni sadaka, itoe,

Maisha ni upendo, ufaidi,

Maisha ni lengo, lifikie,

Maisha ni kengele, igonge,

Maisha ni barabara, ipite,

Maisha ni mti, upande.’’

Kwa hakika maisha ni wimbo, imba kadri ya uwezo wako. Maisha ni mchezo, cheza kadri uwezavyo. Maisha ni changamoto, kabiliana na changamoto unazokutana nazo katika maisha yako. Maisha ni ndoto, timiza ndoto ulizonazo katika maisha yako. 

Msanii wa nyimbo za ‘Hip-hop’ ambaye pia ni Mbunge wa Tanzania, Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Osmund Mbilinyi, katika kibao chake cha ‘Muziki na Maisha’ anatufundisha falsafa inayosema, “Maisha ni ubishi’’.

Maisha ni kuanguka na kuinuka. Ukianguka inuka. Ukianguka amini unaweza bado kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Virgil anasema, “Wanashinda wale wanaoamini wanashinda.’’ Mungu ni dereva wa maisha yetu. Tumwamini yeye na hakika tutashinda. Jinsi uyaonavyo maisha yako huumba maisha yako. Maisha tunayaona kama kitendawili kisicho na jibu kwa sababu tulio wengi tunaishi maisha yasiyo na malengo. Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kimazoea.

Kama unataka maisha yako yawe na mvuto mkubwa yape mhuri wa malengo. Maisha bila malengo ni kama suruali isiyo na zipu!. Katika filamu ya ‘’Chariotos of fire’’, mkimbiaji wa Olimpiki aitwaye Eric Liddell anasema, “Mungu aliniumba kwa malengo.’’ Kama anavyosema kwa ufasaha kabisa Ethel Waters kwamba, “Mungu haumbi takataka.’’

Kuna watu wanaofikiri kwamba wapo duniani kwa bahati mbaya. Sio kweli. Hapa duniani hakuna binadamu aliyeumbwa kwa bahati mbaya. Mchungaji Rick Warren anasema, “Hapo zamani kabla hujawa katika tumbo la mama yako ulikuwa katika mawazo ya Mungu’’. Kuzaliwa kwako hakukutokana na makosa wala bahati mbaya. Mungu hana sifa ya kukosea. Mungu hana sifa ya kubuni. Mungu ana sifa za uhakika. Mungu ana sifa ya umilele. Uko hai kwa sababu Mungu alitaka kukuumba ili uwe sehemu ya viumbe walioumbwa na Mwenyezi Mungu.

Upo ukweli unaopendwa kutumiwa na watu wengi sana, ukweli huo unasema hivi, “Kazi ya Mungu haina makosa.’’ Ni ukweli kwamba hujaumbwa kwa makosa wala kwa bahati nasibu. Mwanasayansi Albert Einstein anasema, “Mungu hachezi bahati nasibu’’. Mshairi Russel Kelfer anasema,‘’Wewe ni wewe kwa kusudi. Wewe ni sehemu ya mpango wa ajabu. Wewe ni wa thamani na chombo maalumu kikamilifu. Unaitwa mtu mwanaume au mwanamke maalumu wa Mungu’’. Biblia Takatifu inasema, ‘’Umeumbwa kwa namna ya ajabu.’’

 

>>ITAENDELEA