Kusubiri ni mtihani. Mtihani mgumu sana maishani ni kuwa na subira ya kungoja wakati muafaka.

“Ni vigumu kuwa na subira, lakini ni jambo baya mno kukosa zawadi za subira,” alisema Abu Bakr.

Subira hata kwa mtu mwema ina mpaka. Mvumilivu hula mbivu akivumilia sana anakula mbovu.

“Ufunguo wa kila kitu ni subira. Unapata kifaranga kwa kutotolewa na si kwa kuvunja yai,” alisema Arnold H. Glasow.

Kusubiri ni mtihani. Mtu anaweza kumzeesha mchumba wake akisubiri wakati muafaka wa kuoa. Kuna methali ya wahaya isemayo: Asemaye ngoja mali iongezeke hufa kabla hajaoa. Kwa mtazamo huo kusubiri ni mtihani. Nakubaliana na Reba McEntire aliyesema: “Usipoteze maisha yako yote ukisubiri kurudi kwenye mavumbi (kuzimuni).” Kijana ambaye hana ndoto yoyote, nia yoyote, mpango wowote ni kijana anayesubiri uzee.

Mjasiriamali Robert Kiyosaki alisema, “Wewe kama ni aina ya mtu ambaye anangoja kitu sahihi kitokee, unaweza kungoja muda mrefu. Ni kama kungoja taa ziwe kijani ukiwa mbali umbali wa maili tano ndipo uanze safari. Kuna mambo ambayo lazima uyafanyie kazi. Hata majibu ya sala lazima kushiriki mchakato wa majibu yake. “Hakuna kitu kitakujia kwa kukaa na kukisubiri,” alisema Zoe Kazan. Mafanikio hayaletwi kwenye sahani ya dhahabu, lazima uyatafute.

Lakini maisha kuna mambo yanahitaji fadhila ya subira. Mgeni aitwaye mzee cheupe alimhoji mtoto wa miaka minne juu ya kaka yake mdogo sana: “Anaweza kujilisha?” aliuliza mzee Cheupe. Mtoto wa miaka minne alijibu, “Hapana.” Aliulizwa tena, “Anaweza kutembea?” Alijibu, “Hapana.” Aliulizwa, “Anaweza kuzungumza?” Alijibu, “Hapana.” Basi mzee Cheupe alisema, “Hafai.” Mtoto huyo alimwambia, “Subiri akue.” Binadamu yeyote mpe muda. Mambo ambayo unatarajia kama hayatokei haraka kumbuka inamchukua mtoto miezi tisa tumboni mwa mama yake kuweza kuzaliwa. Ngoja ngoja huumiza matumbo. Na haraka haraka haina baraka. Wakati mwingine baraka zako kubwa zinakuja baada ya kungoja.

“Subira ni nguvu. Kusubiri siyo kutokuwepo kwa tendo; bali ni kungoja wakati muafaka, subira inangoja wakati muafaka kutenda, kwa kutumia kanuni sahihi na kwa namna sahihi,” alisema Askofu Fulton Sheen wa Marekani.

Kusubiri ni mtihani. Kuna mfalme ambaye alikuwa amezeeka bila ya kuwa na mtoto. Aliita vijana mia na kuwapa mitihani akitafuta atakayemrithi. Mwishowe walibaki vijana watatu. Walipelekwa kwenye uwanja wa mashindano ya kukimbia. Waliambiwa kuwa watakimbia waone nani zaidi. Lakini kabla ya kipyenga kupulizwa msimamizi wa mashindano alimwendea kila mmoja na kumnong’onezea sikioni. Ujumbe ulikuwa ni huu: “Usianze kukimbia mpaka upate ishara toka kwa mfalme.”

Kipyenga kilipulizwa na msimamizi wa mbio. Kijana mmoja alianza kukimbia. Na wa pili alifuata. Wa tatu alibaki amengoja ishara toka kwa mfalme. Mfalme hata hakumtazama. Macho yake yalikuwa kwenye vijana wawili. Walipoitimisha zoezi hilo aliwaita vijana wote watatu na kumpongeza ambaye hakukimbia. Alimuuliza wa kwanza: kwa nini ulikimbia? Alijibu, “Nilitaka kushinda na kuwa mfalme.” Alimuuliza wa pili: “Kwa nini ulikimbia.” Alijibu: “Niliona mwenzangu anakimbia.” Mfalme aliwaambia mtihani ulikuwa juu ya kusubiri. Aliyesubiri alifanywa mfalme. Unachokisubiri kinakusubiri ukifanyie kazi.

“Kila kitu unachokitaka kiko nje kinakusubiri uombe. Kila kitu unachokitaka kinakutaka wewe. Lakini lazima ufanye kitu ili ukipate,” alishauri Jules Renard.

Wakati unasubiri lazima ufanye kitu fulani. Huo ni mtazamo aliokuwa nao pia Padre Henri Nouwen wa Holland: “Kusubiri ni kipindi cha kujifunza. Tunaposubiri kwa muda mrefu zaidi, tunasikia zaidi juu yake tunayemgonjea.”

Tumia muda wa kusubiri kujifunza juu ya lile unalolisubiri.