Nani ataomboleza utakapoaga dunia?

 

Kifo ni mtihani. Kuna aliyesema dunia ni mahali pa hatari sana, hautoki ukiwa hai. Hadithi inapokuwa nzuri kwenye gazeti wanaikatisha na kuandika itaendelea toleo lijalo. Mtu anapoaga dunia ni Mungu anakatisha hadithi ya maisha yake, ni kama anaandika kuwa hadithi yake itaendelea toleo lijalo.

Hasara kubwa si kifo, bali kinachokufa ndani mwetu. “Kifo si hasara kubwa sana katika maisha yetu. Hasara kubwa sana ni kile kinachokufa ndani mwetu wakati tunaishi,” alisema Norman Cousins, mtunga insha na mhariri wa Jarida la Amerika (1912 – 1990). Wakati tunaishi kuna mambo ambayo yanaweza kufa kama shauku, moyo wa kutoa, moyo wa kujitoa, uchaji kwa Mungu, utii, usafi wa moyo. Vikifa ni hasara kubwa.

“Jambo baya sana maishani si kwamba tunakufa, bali kile kinachokufa ndani ya mtu wakati anaishi,” alisema Albert Schweitzer. Jambo baya sana ni matumaini kufa wakati unaishi, utu kufa wakati unaishi, ukarimu kufa wakati unaishi, moyo wa kutendea wengine mema kufa wakati unaishi, mtazamo chanya kufa wakati unaishi na moyo wa kazi kufa wakati unaishi.

Huku ni kufa mara mbili kama mkaa. Mara ya kwanza ni tunu na fadhila moyoni mwako kufa. Na mara ya pili ni kuaga dunia. Hayo yakishasemwa kifo kinabaki kuwa mtihani. Takwimu juu ya kifo ni za kutisha. Kati ya watu elfu moja, elfu moja wote wataaga dunia. Kifo ni mtihani. Mtoto anapozaliwa analia, watu wanafurahi. Mtu anapokufa watu wanalia.

Kuna methali ya Ujerumani isemayo hastahili kuishi anayeishi kwa ajili yake tu. Ukiwafia wengine, unakifanya kifo kiwe zawadi kwa wengine. Kwa namna hiyo utakapoaga dunia watu wengi wataomboleza. Kuomboleza kunahusisha na kukuombea na kukupendekeza kwa Mungu.

“Ni baraka kufia jambo fulani, sababu unaweza kwa urahisi kufia bure,” alisema Andrew Young. Kuwafia wengine hakuhitaji kujipendelea. Mtu anayejipendelea hafikiri kama kuna wengine duniani, anajiona kitinda mimba duniani.

Kuna hadithi juu ya mtu aliyekuwa kwenye kitanda cha mauti. Aliwaambia waliomzunguka: “Nilifia masomo ya kidato cha nne, nikashinda mtihani. Nilifia masomo ya kidato cha sita, nikashinda mtihani. Nilifia masomo ya chuo kikuu, nikashinda. Nilipooa, niliifia familia. Baadaye niliwafia watoto wapate maisha mazuri. Nilifia mambo mengi kama kusemwa vizuri, kuwapendeza watu lakini nilisahau kuishi.” Ndugu msomaji, unafia nini? Usisahau kuishi.

Ukiacha umeandika wosia, kifo chako kinakuwa zawadi na si sababu ya malumbano. Ukiwaachia urithi wa elimu watoto wako, kifo chako kinakuwa zawadi. Juu ya kufanya vifo vyetu viwe zawadi, Henri J. M. Nouwen, mwandishi wa vitabu alikuwa na haya ya kusema: “Namna gani tunafanya vifo vyetu zawadi kwa wengine? Mara nyingi maisha ya watu yanaharibiwa, yanadhuriwa au kuwa na majeraha maisha yao yote kwa vifo vya jamaa au marafiki zao. Lazima tufanye tuwezalo ili kukwepa. Tunapokuwa hatarini kupoteza uhai tunalowaambia walioko karibu nasi, iwe kwa kusema au kuandika ni muhimu. Tunapowashukuru, kuwaomba msamaha kwa makosa yetu na kuwasamehe kwa ya kwao na kuwaonyesha nia ya kutaka waendelee na maisha yao bila kusutwa na dhamiri lakini wakikumbuka neema za maisha yetu, basi vifo vyetu vinakuwa zawadi kweli.”