Hofu ya kushindwa isizidi furaha ya kushinda

 

Hofu ni mtihani. Hofu ya mwanamke ni hofu ya kutumiwa na baadaye kuachwa. Hofu ya mwanamume ni hofu ya kushindwa kwenye maisha. “Palipo na hofu hakuna furaha.” (Seneca). Anayeogopa kitu anakipa nguvu juu yake (methali ya Kimoorishi). Hofu ni adui wetu namba moja. Kuna hofu za aina nyingi. Kuna hofu ya mateso. Kuna hofu ya kushindwa. Kuna hofu kesho.  Kuna hofu ya kupoteza. “Usikubali hofu ya kupoteza kuwa kubwa sana kuzidi furaha ya kushinda,” alisema Robert Kiyosaki. Makazi ya hofu ni akilini, kwa vile hofu ni chaguo. “Wengi wetu hatuziishi ndoto zetu kwa sababu tunaziishi hofu zetu,” alisema Les Brown.

Usiogope ufufuko. Kuna watu wanaopenda mambo yakae ‘yamekufa,’ wanaogopa ‘ufufuko,’ wanaogopa dunia mpya, miundombinu mpya, reli mpya, barabara mpya, mipango mipya, mawazo mapya na maono mapya. Yesu alipokufa, kaburi lililindwa. Nani alishawahi kuona marehemu anawaogopesha walio hai? Walinzi waliwekwa kwa sababu waliogopa ‘ufufuko.’

Huko Ulaya kuna mtoto alikuwa anamfuga paka. Siku moja ilionekana paka huyo alikufa. Mtoto alipewa rambirambi na baba yake, mama yake, majirani na ndugu zake. Alifurahia rambirambi. Jirani yao daktari wa wanyama alipopitia nyumba hiyo mtoto alimwambia daktari habari za kifo cha paka wake. Daktari alipomtazama kwa makini paka aligundua hakufa bali amezirai. Alimpeleka kwenye kliniki yake. Alimtibu na kumrudisha kwa mtoto huyo. Mtoto huyo alikasirika na kusema: “Muue haraka, muue.” Alitaka kufurahia rambirambi, aliogopa “ufufuko.” Kuna njia za kushinda hofu.

Usiogope mambo makubwa. “Ukimuogopa mtu mnene unafikiri ni lini atakuwa mwembamba?” (Methali ya Wahaya). Kuna hofu ya kuogopa mambo makubwa; nyumba kubwa, mipango mikubwa, cheo kikubwa, mashamba makubwa, miji mikubwa, muujiza mkubwa, duka kubwa, kutaja machache, mtu mkubwa. Kuna ambao wanaogopa kumuomba Mungu mambo makubwa.

Kuna mtu aliyekwenda kanisani kuomba nauli ya kutoka Dodoma hadi Dar es Salaam kiasi cha shilingi 25,000. Aliomba kwa sauti ya juu. Kanisani palikuwepo tajiri aliyeingia humo kwa lengo la kuomba Mungu amsaidie aweze kupata milioni hamsini.

Aliposikia huyo anaomba shilingi 25,000, alitoa kiasi hicho cha fedha mfukoni na kumpatia na kumwambia atoke kanisani. Yeye alianza kuomba hivi: “Mwenyezi Mungu niko hapa peke yangu naomba milioni hamsini.” Usiogope kuomba makubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Atakupaje? Yeye anajua. Fanya zuri unaloweza kufanya mengine mwachie Mungu.

Kwanza fanya zuri unaloogopa kufanya. Eleanor Roosevelt alisema: “Hofu ni hisia inayodhoofisha sana. Nilipigana nayo na kuishinda kwa kuwasaidia watu ambao walikuwa na hali mbaya sana kunizidi. Naamini mtu yeyote anaweza kushinda hofu kwa kufanya mambo anayoogopa kufanya ili mradi anaendelea kuyafanya mpaka anapata rekodi ya uzoefu wenye mafanikio nyuma yake.”

Pili, fikiria mambo makubwa ya kuogopesha uliyoyapitia na kujiambia: “Nimepitia jambo hili la kuogofya. Naweza nikapitia jambo jingine lijalo.” (Eleanor Roosevelt). Tatu, kuwa na ujasiri. “Ujasiri si kutokuwepo kwa hofu; bali ni uamuzi kuwa jambo jingine ni muhimu kuliko hofu,” alisema  Ambrose Redmoon.

Ogopa ni ngao pia. (Methali ya Kiswahili).

Ngao ni chombo cha kujikinga kutokana na mfumo wa adui kwenye vita. Kuna wakati woga unahitajika. Kuna wakati ujasiri haufai. Huwezi kuingiza mkono kwenye kinywa cha simba wa mwituni, ukijiambia kuwa wewe ni jasiri. Lazima kuogopa maambukizi ya magonjwa.