Moyo uliovunjika usiuvunje
Moyo uliovunjika ni mtihani. Vitu vikivunjika vinaunganishwa, si jambo jepesi kuunganisha moyo uliovunjika na kupondeka. Christie Brinkley amesema: “Afadhali kuwa na mkono uliovunjika kuliko kuwa na moyo uliovunjika.” Moyo uliovunjika ni moyo wenye maumivu, usiuvunje.
“Maumivu hayaleti jambo jipya kila mara; yakipokewa vibaya yanasababisha ulevi, weu na kujiua,” amesema Madeleine L’Engle katika kitabu chake ‘Walking on Water.’
Machungu yajapo yapokee kwa mtazamo chanya. Moyo uliovunjika ni moyo unaovuja machozi, usiuvunje.
“Machozi ni maneno ambayo mdomo hauwezi kusema na moyo hauwezi kubeba,” amesema Joshua Wisenbaker. Mioyo iliyovunjika inaongea. Wakati ulimi unasema: “Sijambo,” vidole vinatuma ujumbe wa simu: “Sijambo,” moyo unaweza kuwa unasema: “Nimevunjika, nimepondeka.”
Mtu aliyevunjika moyo ni mwanzi uliopondeka, usiuvunje. Mwanzi uliopondeka unavunjika haraka. Mwanzi uliopondeka ni msemo unaosimama badala ya mtu dhaifu, aliyekata tamaa au mtu mwenye matatizo. Kumkejeli mtu aliyevunjika moyo hakusaidii. Kuzidi kumshutumu mtu aliyevunjika moyo hakusaidii. Popote palipo na talaka kuna moyo uliovunjika. Popote palipo na fitina kuna moyo uliovunjika. Popote palipo na msiba kuna moyo uliovunjika. Popote palipo na kukatishwa tamaa kuna moyo uliovunjika. Popote palipo na ndoto iliyovunjika kuna moyo uliovunjika. Popote mtu anapoaibishwa kuna moyo uliovunjika. Popote palipo na shukrani ya punda ni mateke kuna moyo uliovunjika. Ukisikia misemo kama: “Ninaotibu vidole ndio wanaiba viazi vyangu”, kuna moyo uliovunjika. Moyo uliovunjika ni moyo wenye sononeko, huzuni, taabu, simanzi na maumivu. Moyo uliovunjika ni moyo wenye vidonda. Ni moyo wenye kumbukumbu mbaya.
“Kila mara moyo wako unapovunjika, nyufa za mlango wa kutoka zinajitokeza kuelekea dunia mpya iliyojaa mwanzo mpya na fursa mpya,” amesema Patti Roberts. Ili kuganga moyo uliovunjika kwanza achia, usishikilie yaliyopita. Yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo. Achilia jambo ambalo linakuweka mbali na matumaini na upendo. Pili, samehe au omba msamaha. Kusamehe ni kuachia mfungwa utagundua mfungwa ni wewe. Unakuwa mfungwa wa chuki. Kama umekosa omba msamaha.
Tatu, mtu aliyevunjika moyo anahitaji huruma. Kuna hadithi juu ya mtu aliyeanguka kwenye shimo hakupata msaada haraka ingawa watu walikuwepo akawa analia. Mtu mwenye kutazama hualisia alisema: “Hilo ni shimo.” Mtu anayetegemea mazuri alisema: “Mambo yatakuwa mazuri zaidi.” Mtu anayetegemea mabaya yatokee alisema: “Mambo yatakuwa mabaya.”
Mwandishi wa habari alisema: “Itakulipa ukinielezea maisha ya shimoni yakoje.” Ofisa wa jiji alisema: “Je, ulipata kibali cha kukaa kwenye shimo?” Mwanahisabati alisema: “Nitapima urefu, upana na kina cha shimo.” Muhubiri alisema: “Kuna mambo ya kujifunza ya kiroho kuhusu shimo.” Mwenye huruma alisema: “Nipe mkono wako nikuvute.” Aliyevunjika moyo anahitaji kidole cha kumvuta na si kumnyoshea kidole.
Nne, orodhesha nguvu zako, mazuri yako, mema yako, rasilimali zako, mambo chanya yako au ya mwingine ambaye moyo wake umevunjika. Hesabu baraka, hesabu neema, hesabu mema. Tano, pita, nalo hilo litapita. Ndege inapoanza kupaa inapita kwenye dhoruba, haisimami, dhoruba nayo inapita. Ndege inapoaanza kutua inapita kwenye dhoruba, nayo dhoruba inapita. Haisimami. Katika magumu ya maisha, pita, usisimame nayo yatapita. Kipindi cha majonzi, pita nacho kitapita. Katika matatizo, pita, usisimame nayo yatapita.