Kutawala ulimi ni mtihani. Unapofungua mdomo kuzungumza ni kama unawafungulia watu albamu ya maisha yako, nao huo ni mtihani. Wataalamu wa mawasiliano wanatwambia kuwa mtu wa kawaida kwa wastani kwa siku anaweza kusema maneno ambayo yatajaa kurasa 20 zenye nafasi ya mstari mmoja. Ina maana kuwa midomo yetu yaweza kutoa maneno ya kujaza vitabu viwili vya kurasa 300 kila mwezi, vitabu 24 kila mwaka na vitabu 1,200 kwa muda wa miaka 50. Kuna methali isemayo: “Nilisema anamzidi Nilinyamaza.” Anayemuonya mwenzake ni bora kuliko ambaye anashindwa kumuonya mwenzake anapoona anafanya jambo ambalo si sahihi. Kumuonya mtu ni mtihani na kutomuonya ni mtihani. Mwanafalsafa wa zamani, Zeno, alisema: “Tuna masikio mawili na mdomo mmoja, hivyo tusikilize mara mbili ya tunavyoongea.”
Kuna watu ambao wanaongea sana. Kuna methali isemayo: “Mwenye kuzungumza maneno mengi hajui ni wakati gani amemtukana mama mkwe.” Katika maneno mengi ni rahisi kukosea. Kuna kijana aliyekwenda kwa mwanafalsafa wa Kigiriki, Socrates, kujifunza ufundi wa kuongea. Alipokaribishwa ajitambulishe aliongea maneno mengi sana mpaka Socrates alimwambia kuwa atamtoza karo mara mbili. Kijana alihoji: “Kwa nini kunitoza karo mara mbili?” Socrates alimjibu: “Lazima nikufundishe sayansi mbili: moja ni namna ya kunyamaza na nyingine ni namna ya kuongea.”
Ulimi hauna mfupa, lakini waweza kuvunja moyo. Mtume Mohammed, alisema: “Uzuri wa mtu upo ulimini mwake.” Kama mtu angekulipa shilingi milioni moja kwa kila neno zuri unaloongea na kukuomba umlipe shilingi milioni moja kwa kila neno baya unalosema, ungekuwa tajiri au maskini? Ulimi una nguvu ya kumuinua mtu kwa maneno, ulimi una nguvu ya kumwangusha mtu.
Lililo moyoni, ulimi huiba, hivyo pima maneno yako. Pima swali lako, pima jibu lako. Hariri maneno yako kabla ya kutoka mdomoni. “Usiruhusu ulimi wako utaje makosa ya wengine, na wewe una makosa yako; na watu wengine wana ndimi.” (Methali ya Kiarabu). Kuwa makini katika kutumia ulimi.
“Ufundishe ulimi wako kusema ‘sijui’, hivyo utapiga hatua,” alisema Maimonides. Kusema hivyo wakati mwingine kunapunguza majuto na majuto ni mjukuu. Ulimi unaweza kukufanya ujutie ulilolisema.
Maneno yana nguvu. “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi, na wao waupendao watakula matunda yake.” (Mithali 18:21). Umbeya ambao ni matunda ya ulimi ni ugaidi. Ulimi ni silaha ya maangamizi. “Moto na mapanga ni injini za maangamizi ya polepole zikilinganishwa na umbeya wa ulimi.” (Richard Steele). Kutumia ulimi upendavyo ni kujitia katika hatari. Mungu alijua kuwa ulimi unaweza kuleta uharibifu akaupa uzio wa meno na uzio wa mdomo.
“Maneno mema hayagharimu zaidi kuliko maneno mabaya. Basi, kwa nini hatutumii maneno mema?” Alihoji Shaaban Robert. Maneno mema ni heri wala si shari, yanaleta raha wala si karaha. Ulimi ukitumiwa vizuri waweza kujenga na ukitumiwa vibaya waweza kubomoa. Ulimi ukitumiwa vizuri waweza kuunganisha na ukitumiwa vibaya waweza kutenganisha.
Kuna mtu aliyeomba aletewa supu nzuri sana na baadaye supu mbaya sana. Awamu ya kwanza ya kuleta supu nzuri sana walileta supu ya nyama ya ulimi wa ngo’mbe. Awamu ya pili ya kuleta supu mbaya sana walileta pia supu ya ulimi wa ng’ombe. Mtu huyo aliuliza, “maana yake nini?”
Walimweleza kuwa awamu zote mbili walileta supu ya ulimi, walitaka kuonyesha ubaya wa ulimi na uzuri wa ulimi. Ulimi unalaani. Ulimi unabariki. Ulimi unasifia, ulimi unatukana. Yote yakiisha kusemwa, ukweli unabaki kutawala kuwa ulimi ni mtihani, lakini ufanye.