Kujipenda ni mtihani si ubinafsi, kujipenda si uchoyo, wala si kujipendelea, maana huwezi kumpenda mtu kama hujipendi. Kujipenda ni kujikubali, kujithamini na kujitambua.
Ushahidi kuwa watu wengi hawajipendi umejaa kama hewa, mtu anaweka vikombe vizuri vya chai kwa ajili ya wageni, yeye kila mara anatumia vikombe vilivyopasuka na vyenye mwanya, jambo hilo ni ushahidi wa kutojipenda.
Fundi seremala hana kiti kizuri cha kukalia wakati anawatengenezea wengine viti vizuri, jambo hilo ni ushahidi wa kutojipenda. Kumbuka adui wa mtu ni mtu na unaweza kuwa adui wa nafsi yako. Peter the Great alisema: “Nimeushinda ufalme lakini sijaweza kujishinda.”
Kuna baba fulani alikwenda shambani na kamba kwa ajili ya kujinyonga, mtoto wake baada ya kushinda bahati nasibu ya shilingi milioni hamsini alimtafuta baba yake kumpa habari njema.
Aliambiwa amekwenda shambani, alipofika shambani alimkuta anajiandaa kujinyonga, alimwambia habari njema ya ushindi na kuongeza kuwa kama ameamua kufanya hivyo atapewa mazishi mazuri, maana pesa ipo.
Baba huyo alimwambia mtoto wake: “Acha upumbavu, njoo ukate kamba hii twende tusherehekee ufufuko wangu.” Baba huyo kitendo alichotaka kukifanya alikuwa hajipendi, lakini huenda alikuwa ni mgonjwa kisaikolojia.
Kushughulika sana na kutokustahili kwako ni kutojipenda. Unastahili kujipenda, kama unawajali wengine si jambo baya kujijali. Swali namna gani ujipende? Socrates alisema: “Jijue.” Marcus Aurelius alisema: “Jitawale.” Kuna aliyesema: “Jitoe.” Yesu alisema: “Jikane mwenyewe.” Namna gani ujipende?
Kwanza, amua kuwa maisha yako ni maisha yako. “Siku nzuri sana ya maisha yako ni siku ambayo unaamua kuwa maisha yako ni yako. Hakuna kuomba msamaha au visingizio, hakuna wa kuegemea, kutegemea au kulaumu.
“Zawadi ni yako, ni safari ya kustaajabisha, na wewe peke yako ndiye unawajibika kwa ubora wake. Hii ni siku ambayo maisha yako yanaanza kweli,” alisema Bob Moawad.
Pili, jitunze. “Kujitunza si tendo la ubinafsi – ni utunzaji wa zawadi pekee niliyo nayo, zawadi ambayo niliwekwa dunia kuitoa kwa wengine,” alisema Parker Palmer. Utakavyokuwa ni zawadi yako kwa wengine.
Tatu, usijihukumu. “Ilinichukua muda mrefu kutojihukumu kupitia macho ya mtu mwingine,” alisema Sally Field. Acha kujilinganisha na wengine.
“Umekuwa ukijisema vibaya kwa miaka mingi, haikufanya kazi. Jaribu kujikubali na uone litakalotokea,” alisema Louise L. Hay. Sema maneno mazuri juu yako.
Nne, fikiria mafanikio yako, si kushindwa kwako. “Kuanzisha jambo la kujiheshimu kweli lazima kuwa makini kwenye mafanikio yetu na kusahau juu ya kushindwa na hasi katika maisha yetu,” alisema Denis Waitley.
Tano, jithamini. “Kama hujithamini, hutathamini muda wako. Na kama hutathamini muda wako, hutafanya lolote na muda wako,” alisema M. Scott Peck.
Sita, jiamini. “Kwa nini tuogope watu wanachofikiria juu yetu? Je, tuna imani zaidi na maoni yao kuliko maoni yetu?” alihoji Brigham Young.
Saba, jua kilichomo ndani yako ni kikubwa. “Kilichoko nyuma yako na kilichoko mbele yako ni mambo madogo ukilinganisha na kilichomo ndani yako,” alisema Ralph Waldo Emerson.
Nane, jitawale na jidhibiti, tawala hisia zako, tawala ulimi wako, tawala mawazo yako, hutakuwa na mjukuu anayeitwa majuto. “Kuwa mtumwa wa nafsi yako ni utumwa mbaya sana kati ya aina zote za utumwa,” alisema mwanafalsafa Seneca.
Kumbuka wewe ni mtu binafsi, kujitawala ni kuwa huru. Tisa, usiogope, fanya zuri unaloliogopa kufanya. Kumi, kuwa mwema kwako na kwa wengine. Ushauri mzuri unaowapa wengine na wewe uweke katika matendo. Jishauri.