Mwanzo ni mtihani, mwanzo mgumu, lakini lisilowezekana linawezekana. Mwanzo wa ngoma ni lele, mambo yote makubwa huanzia madogo.
Mwandishi wa vitabu vya hadithi wa Uingereza, John Creasy, alipata barua 753 za kukataa kuchapisha vitabu vyake na wachapishaji wa vitabu kabla ya vitabu vyake 564 kuchapishwa.
Methali ya Kiswahili inasema ukweli wote: “Mwanzo huwa na usiri, ikawa mkaragazo.” Kila mwanzo wa jambo huwa mgumu lakini baadaye jambo hilo huwa jepesi. Mkaragazo ni mvua inayonyesha kwa wingi. Mvua ianzapo kunyesha huanza polepole kisha hunyesha kwa wingi.
Mwanzo umepambwa na kushindwa. “Kushindwa mara nyingi ni saa ya giza ya alfajiri inayotangulia mapambazuko ya siku ya mafanikio,” alisema Leigh Mitchell Hodges.
Maisha ya mchezaji wa mpira wa kikapu, Michael Jordan, yanabainisha ukweli huo. Alikosea kufunga mara 9,000. Alipoteza michezo 300. Alisema: “Nimeshindwa mara nyingi maishani ndiyo sababu ninafanikiwa.”
Baba wa uchimbaji mafuta, Edwin L. Drake, aliambiwa mwaka 1859: “Unataka kuchimba mafuta? Unamaanisha kuchimba ardhi ukitafuta mafuta utakuwa umerukwa akili!”
Kilichofuata ni historia, bwana huyo hakusikiliza maneno ya kukatisha tamaa. Katika yote unahitaji matumaini. Ni kweli alivyosema Louise Phillipe: “Giza linapokuwa nene, nyota inaangaza sana.”
Shujaa wa ufundi wa kuongea, Winston Churchill, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza alishindwa akiwa darasa la sita. Ilimchukua miaka mitatu kumaliza darasa la nane kwa sababu ya tatizo la kujifunza Kiingereza.
Lakini aliendelea kusoma sana mpaka siku moja alikaribishwa na Chuo Kikuu cha Oxford kutoa hotuba wakati wa ufunguzi wa mwaka wa masomo. Alishindwa kila uchaguzi alipogombea lakini aliweza kuchaguliwa kuwa waziri mkuu akiwa na umri wa miaka 62.
Katika kura za maoni zilizoendeshwa na Shirika la Habari BBC mwaka 2002 kubainisha Waingereza 100 mashuhuri, washiriki walimpigia kura Winston Churchill kama mtu mashuhuri kuzidi wote.
Lisilowezekana linawezekana, Marie Curie ni mwanamke wa kwanza mwanasayansi kupokea tuzo ya Nobel mara mbili. Ni kinara katika uwanja wa Kemia na Fizikia. Alizuiliwa alipotaka kujipatia elimu ya juu katika nchi yake ya Poland wakati huo ikiwa chini ya udhibiti wa Urusi.
Alihamia Paris, Ufaransa yeye pamoja na mume wake, Pierre Curie, walitumia muda wao mwingi kufanya utafiti. Kuna wakati ambao walikuwa hawana chakula kabisa. Waligundua Polonium na Radium.
Mwanamke huyo aliwahi kusema: “Maisha si rahisi kwetu sisi. Lazima tuwe na uvumilivu na juu ya yote kujiamini. Hakuna jambo lolote katika maisha linalopaswa kuogopwa, linapaswa kueleweka.”
Lisilowezekana linawezekana, Jina Henry Ford, halihitaji utambulisho katika sekta ya kutengeneza magari. Alikuwa mtoto wa mkulima. Alikulia shambani, labda angebaki akiwa mkulima kama si kupenda kwake magari.
Aliacha shule akiwa na umri wa miaka 15 ili kufanya kazi katika shamba la baba yake. Baadaye alihamia Detriot alipokuwa msaidizi katika duka la kuuza mashine wakati wa jioni ili kuweza kujikimu, alitengeneza saa zilizoharibika kwa vile posho aliyokuwa anapata ilikuwa haitoshi.
Aliingia katika biashara ya kutengeneza magari, alifilisika mwaka wake wa kwanza. Mwaka uliofuata kampuni yake ya pili ilikumbana na kushindwa vibaya sana. Lakini hakukata tama, alipigana vita vizuri.
Jina lake lilianza kujulikana nje ya mipaka ya Marekani, kilichobaki ni historia. Aliwahi kusema: “Mojawapo ya uvumbuzi mkubwa ambao mtu anaweza kufanya ni kugundua kuwa anaweza kufanya alilokuwa anaogopa kufanya.”
Methali ya Kiswahili yasema: “Mwanzo wa mkeka chane mbili.” Usidharau mwanzo wa jambo lolote lile.