Kushindwa ni mtihani, mambo magumu sana ya kushughulikia maishani ni kushindwa na kushinda. Ukishindwa ni mtihani, ukishinda ni mtihani.
Kuendeleza ushindi ni mtihani, kushikilia namba moja ni mtihani, kushikilia namba ya mwisho ni mtihani. Hoja si kushindwa bali lile mtu analofanya baada ya kushindwa.
Hakuna anayefanikiwa bila kushindwa, hakuna ambaye hufanikiwa kwa sababu ya kushindwa. “Tunaogopa kushindwa sana, kushindwa ni zoezi muhimu ili kufanikiwa,” alisema Charles F. Kettering.
Kujaribu na ukashindwa si uvivu, uvivu ni kutojaribu. Kushindwa ni vijilia ya kushinda. Kukosa njia ni kujua njia. Kushindwa ni fursa ya kuanza tena ukiwa na hekima kuliko mwanzoni.
Mwanzo mgumu, hata wanaoanza taratibu wanaweza kushinda. Jogoo wanaowika kuna wakati yalikuwa mayai. Charles Darwin, mwanasayansi alifanya vibaya sana darasani mpaka mwalimu wake alimwambia: “Utakuwa aibu kwa familia.”
Kusema kweli mwanasayansi huyu baadaye aliiletea heshima familia. Mwandishi mashuhuri Gilbert Chesterton hakuweza kusoma mpaka alipokuwa darasa la tatu. Mmojawapo wa walimu wake alimwambia: “Tukifungua kichwa chako hatutakuta ubongo, lakini tutakuta rundo la mafuta meupe.” Baadaye Gilbert Chesterton aliandika vitabu vingi.
Wazazi wa Albert Einstein, mwenye akili nyingi walikuwa na wasiwasi sana juu ya matokeo yake mabaya shuleni.
Alikuwa mzuri sana katika somo la Hisabati tu. Mwalimu wake alimwambia kuacha shule akisema: “Einstein hautakuwa mtu wa maana.” Albert Einstein alishindwa mtihani wa kuingia chuo kikuu.
Einstein aliandika jina lake vizuri na kuwa mtu mashuhuri. Henry Ford alisahau kuweka gia ya kurudi nyuma kwenye gari aliloliunda, mwanzo mgumu. Usimhukumu vibaya mtu yeyote ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu.
Fikiria kushinda, usifikirie kushindwa, kwenye biashara, ofisini, kazini, nyumbani, mtaani, badili kufikiri kushindwa kuwe kufikiria kushinda. Unapokabili hali ngumu ya maisha fikiria kushinda.
Unapofilisika fikiria kushinda, fursa inapokujia fikiria kuwa unaweza kuifaidi na si kufikiria haina chochote. Unapolikabili tatizo fikiria kuwa limebeba zawadi.
Acha mawazo ya kushinda yatawale akili yako. Kiwango chako cha kufanikiwa kinaendana na kiwango chako cha kufikiria na kuamini. Fikiria makubwa na amini makubwa.
Kuna mzazi ambaye alimsindikiza mtoto wake shuleni. Alipokuwa anamkabidhi kwa walimu aliwaambia: “Mtoto huyu atakuwa taa ya darasa.” Mtihani wa muhula wa kwanza alikuwa wa mwisho.
Mwalimu mmoja alisema: “Baba yake alitwambia atakuwa taa ya darasa, sasa amekuwa wa mwisho.” Mwalimu mwingine alitania: “Gari huwa na taa za nyuma, bado mwanafunzi ni taa ya darasa, anaangaza kwa nyuma.”
Lakini mwanafunzi huyu alipofika kidato cha nne alikuwa anakuwa wa kwanza kwenye mitihani ya kila mwezi na mtihani wa taifa wa kidato cha nne katika darasa lao alikuwa wa kwanza. Baba wa mzazi alifikiria makubwa na kuamini makubwa na alipanda mbegu hiyo akilini mwa mtoto wake.
Kushindwa ni kuchelewa na si kukwama kabisa. Kushindwa si mwisho wa barabara bali ni kona kwenye barabara.
“Mungu anatuacha tushindwe katika mambo ambayo si muhimu ili tuweze kushinda katika mambo ambayo ni muhimu,” alisema Henrietta C. Mears. Kushindwa ni somo katika mtaala wa Mungu.
Mtume Petro aliposhindwa vibaya sana kwa kumkana Yesu Kristo baadaye alipewa cheo kikubwa sana. Kushindwa ni zana anayoitumia Mungu kutuandaa kwa ajili ya mafanikio makubwa.
Kushindwa ni giza linalotangulia mapambazuko. Kushindwa ni utangulizi wa kushinda. Lisilowezekana linawezekana.