Matatizo ni mtihani. “Matatizo huzaa matatizo; lakini matatizo ni mazalio makubwa ya mafanikio. Mara chache mafanikio ya kweli, maendeleo ya kweli yanakuja kwa njia nyingine,” alisema Gerald Jaggers.
Matatizo ni fursa ya kupiga hatua mbele. Likabili tatizo, usilizunguke, usilikwepe. “Matatizo ya dunia yataendelea kuongezeka kama tunaendelea kuwafundisha watu namna ya kugundua matatizo badala ya kuwafundisha namna ya kuyatatua,” alisema O.A. Battista.
Binadamu ni mtatuzi wa matatizo. Matatizo yana suluhisho, kupokea tatizo bila chuki ni kupunguza makali yake. Kutolikwepa tatizo ni kupunguza makali yake, kubainisha tatizo ni kupunguza makali yake. Tatizo kubwa ni kutotatua tatizo. Matatizo ni mtihani.
Ndege inapoanza kupaa inapita kwenye dhoruba, haisimami, dhoruba nayo inapita. Ndege inapoanza kutua inapita kwenye dhoruba, nayo dhoruba inapita, haisimami. Pita, tatizo nalo linapita.
Wanandoa chini ya miaka mitano wanapoanza maisha ni kama ndege inayopaa, wanapita kwenye dhoruba. Wapite, kipindi hicho kinapita. Katika kipindi kigumu cha maisha, pita, usisimame nacho kitapita. Kipindi cha majonzi, pita nacho kitapita. Katika matatizo, pita, usisimame nayo yatapita.
Kipindi cha mitihani pita, nacho kitapita, kipindi cha kupanda kwa machozi, pita nacho kitapita. Unapozomewa kwa kutenda mema, pita, nalo hilo litapita. Unapoonewa wivu kwa mafanikio, pita nalo hilo litapita, unapopigiwa kelele ili kukatishwa tamaa pita, nalo hilo litapita.
“Mtu mmoja ambaye hasiti kutatua tatizo lake ni zaidi ya watu kumi na wawili ambao wanapendelea kuongelea suluhisho lake,” alisema O.A. Battista.
Matatizo yana suluhisho. Dk. Robert H. Shuller, katika kitabu chake, Tough Times Never Last, But Tough People Do anapendekeza kanuni kumi na mbili za kutatua matatizo ambayo yanaweza kuzifafanua katika maneno yangu kama ifuatavyo:
Kwanza, usidharau tatizo, mdharau mwiba mguu huota tende, ukidharau mwiba utachechemea. Tatizo ni kama kikohozi halifichiki. Usichukue mtazamo wa mbuni wa kuficha kichwa chini ya mchanga wakati miguu yote na mbawa vinaonekana nje.
Pili, usitie chumvi juu ya ukubwa wa tatizo. Kupata pancha si mwisho wa safari. Umepoteza kazi? Si mwisho wa dunia. Unaweza kuanza upya, unaweza kujiajiri.
“Ujumbe kutoka mwezini ni kuwa hakuna tatizo lolote linaweza kutazamwa kama halitatuliki,” alisema Norman Cousins. Binadamu baada ya kukanyaga mwezini ujumbe ni kuwa lisilowezekana linawezekana.
Tatu, usisubiri. Ngoja ngoja yaumiza matumbo. Jambo linalostahili kutendwa papo hapo lisipotendwa kwa wakati ufaao, hutia hasara. Liwezekanalo leo lisingoje kesho.
Watu wanaongoja wakati ufaao huishia kutofanya lolote. Nne, usiongeze ukubwa wa tatizo kwa kulaumu. Usipendekeze lawama, pendekeza suluhisho. Usilaumu wazazi wako, usilaumu serikali, usilaumu kampuni.
Usijihurumie, tano, angaza, tumia njia inayowezwa kuitwa, BTAF. Bainisha tatizo, tabiri tatizo lisipotatuliwa kitakachotokea. Likitatuliwa ni jambo gani litatokea, amua, fanyia kazi.
Sita, jitie moyo au tia moyo. Huwezi kumlazimisha farasi kunywa maji, lakini unaweza kumtia kiu. Jimotishe. Kila tatizo ni fursa. Kila tatizo limebeba zawadi.
Saba, tega. Weka kitu ili kinase. Mtu anapouliza, nifanye nini ili kupata kazi. Jibu, “namna gani unamtega panya?” Jibu la namna gani hilo?
Lina maana unapomtega panya unafikiria chakula apendacho, njia yake, saa zake za kutoka na mengine. Weka mitego mingi ya kupata kazi au pesa.
Nane, chumbia. Kama hauna kazi chumbia kazi kama kijana wa kiume anavyomchumbia msichana. Tafuta, omba, pendekeza, usikate tamaa. Tisa, badili balaa kuwa baraka. Katika miiba kuna maua, tafuta maua hayo ni yapi. Kumi, wasiliana.
Pata, maoni ya watu wengine. Kumi na moja, kuwa na mtazamo chanya. Kumi na mbili weka moyo wako wote na akili yako yote katika kutatua tatizo.