Mafanikio yanategemea mtazamo. Kushinda kunategemea mtazamo. Furaha inategemea mtazamo. Shukrani inategemea mtazamo. Umaskini unategemea mtazamo. Utajiri unategemea mtazamo. Amani inategemea mtazamo.
“Mtazamo ni jambo dogo lakini linafanya tofauti kubwa,” alisema Winston Churchill. Kinachowatofautisha wavumilivu na waliokata tamaa ni jambo dogo linaloitwa mtazamo. “Nyuki hunyonya asali kutoka maua yenye uchungu sana.” (Methali ya Kiingereza).
Nyuki ana mtazamo chanya. Kwenye maua yenye uchungu anaona asali. Mwenye mtazamo hasi atahisi ukakasi wa maua yenye uchungu sana.
“Watu wawili wanatazama nje kupitia madirisha yale yale, mmoja anaona matope mwingine anaona nyota.” (Frederick Langbridge).
Mtazamo chanya unakufanya uone nyota, na mtazamo hasi unamfanya mwingine aone matope. Kwenye matatizo mwenye mtazamo chanya anaona fursa. Mwenye mtazamo hasi anaona balaa. “Mtazamo ni chaguo. Furaha ni chaguo. Wema ni chaguo. Kutegemea mazuri ni chaguo. Ukarimu ni chaguo. Heshima ni chaguo. Kwa lolote unalolifanya chagua kwa hekima,” alisema Roy T. Bennet.
Umeshikilia kikombe cha kahawa. Mtu anatingisha mkono wako au anakugonga kahawa inamwagika.
Kwa nini kahawa imemwagika na si vinginevyo? Kwa sababu mtu amekugonga. Wakati mwingine si jibu sahihi. Kahawa imemwagika na si vinginevyo kwa sababu kwenye kikombe palikuwamo kahawa tu na si chai.
Pangekuwamo chai, chai ingemwagika. Kilichomo kwenye kikombe ndicho kitamwagika. Maisha yakikutingisha, jambo gani litatokea? Kilichomo ndani mwako kitatoka nje. Kwenye kikombe kuna nini? Maisha yanakupa kikombe, unaamua unajaza nini? Kilichomo moyoni kikifurika kinatoka nje ya moyo.
Moyoni jaza mawazo chanya. Wazo lolote ambalo linaleta mwanga lifikirie. Wazo lolote ambalo ni wazo taka achana nalo. Wazo lolote ambalo ni wazo mgando achana nalo. Wazo lolote ambalo ni wazo giza achana nalo.
“Ndugu, yaliyo kweli, matukufu, adili, yaliyo matakatifu, ya kupendeza na ya sifa njema, yote yanayohusiana na ukamilifu, tena masifu, hayo yafikirieni hasa.” (Wafilipi 4:8). Mawazo ya upendo ni mawazo safi.
“Palipo na upendo, hakuna giza (Methali ya Burundi). Mawazo ya kusaidia wengine ni mawazo safi. “Lengo letu la kwanza katika maisha haya ni kuwasaidia wengine. Kama huwezi kuwasaidia wengine usiwaumize,” alisema Dalailama.
Kuna profesa aliyetembelewa na wanafunzi wake wa zamani. Walikuwa na wake zao au waume zao na watoto. Walimweleza wanavyokuwa na msongo wa mawazo kazini.
Walimweleza kuwa wanakabili mateso. Aliwakaribisha kunywa kahawa. Ilikuwa imewekwa kwenye vikombe mbalimbali: vya rangi ya dhahabu, vya plastiki, vya udongo kutaja aina chache. Walipigana vikumbo kuchukua vya rangi ya dhahabu. Aliwaambia kuwa kama walivyopigana vikumbo kuchukua vikombe vya dhahabu, hili ndilo linawaletea msongo wa mawazo hata kazini. Jambo dogo linalowatofautisha hapa ni mtazamo. Hoja si rangi ya kikombe bali kilichomo. Hoja si aina ya kazi au cheo bali kilichomo. “Kinywa …huyanena yaujazayo moyo wake.” (Mt. 12: 34). Chunga sana moyoni unajaza nini?
Wahaya wana methali isemayo: “Akaijwire kabira.” (Kilichojaa hufurika). Moyo ukijaa ukarimu, ukarimu utafurika. Moyo ukijaa mawazo ya sadaka, sadaka itafurika. Moyo ukijaa mawazo ya hisani, hisani itafurika.
Moyo ukijaa hasira, hasira itafurika. Upendo ukijaa moyoni, upendo utafurika. Barua kutoka moyoni inaweza kusomwa usoni. Ni methali ya Kiswahili.
Uso wa mtu unaonyesha kilichomo moyoni. Maneno yako ni madirisha ya moyo wako. Lililo moyoni ulimi huiba. “Kinywa hutaja yanayofurika moyoni.” (Mathayo 12: 34).
Ukisema: “Asante” shukrani imefurika moyoni. Ukisema: “Nakupenda” upendo umefurika moyoni. “Mtu mwema hutoa mema katika hazina njema ya moyo wake, na mtu mwovu hutoa maovu katika hazina mbovu ya moyo wake; kwa maana kutoka kinywa chake hunena yafurikayo moyoni.” (Luka 6: 45).